
Mabango yanayoonyesha shukrani kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yamesimikwa kando ya barabara kuu inayoelekea uwanja wa ndege wa Beirut, yakionyesha shukrani za dhati kwa msimamo wa Iran wa kutaka kukomeshwa kikamilifu uchokozi wa Israel dhidi ya Lebanon, kama ilivyotajwa katika waraka wa makubaliano (MoU) uliosainiwa hivi karibuni kati ya Iran na Marekani.
Siku ya Jumapili, mabango yenye ujumbe wa shukrani kwa Iran yalionekana kando ya barabara kuu inayounganisha jiji la Beirut na uwanja wake wa ndege wa kimataifa, mojawapo ya njia zenye shughuli nyingi zaidi katika mji mkuu huo.
Mabango hayo yalikuwa na picha za Kiongozi shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, pamoja na Kiongozi wa sasa, Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei, yakifuatana na ujumbe: “Asante kwa Iran kwa uwaminifu.”
Kwa mujibu wa ripoti za ndani, mabango hayo yalikusudiwa kuonyesha shukrani kwa msisitizo wa Iran kuhusu kukomeshwa kwa vita vya Israel dhidi ya Lebanon katika waraka huo wa makubaliano.
Ali Ammar, mbunge wa kundi la bunge la Uaminifu kwa Muqawama (Upinzani), amesema Iran imekuwa ikiunga mkono daima harakati ya muqawama na kubaki mwaminifu kwa ahadi zake.
Ammar alisema: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imethibitisha dhamira yake ya kuunga mkono muqawama na imekuwa daima ikisimama pamoja nao.”
Jumapili iliyopita, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilitangaza kuwa waraka huo wa makubaliano ulikuwa umekamilishwa baada ya mfululizo wa mazungumzo makali kati ya Iran na Marekani.
Waraka huo ulisainiwa kwa njia ya kidijitali na kwa umbali na Rais wa Iran Masoud Pezeshkian pamoja na Rais wa Marekani, Donald Trump, katika saa za mapema za Alhamisi.
Iran na Marekani zinatarajiwa kufanya mfululizo wa mazungumzo katika kipindi cha siku 60 zijazo kwa lengo la kufikia makubaliano ya kina kuhusu masuala yenye utata kati yao.
Kwa mujibu wa waraka huo, vita katika nyanja zote, ikiwemo Lebanon, vilipaswa kusitishwa mara moja na kwa kudumu kuanzia Jumapili iliyopita.