Dar es Salaam. Serikali imeanza maandalizi ya ujenzi wa Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika katika Wilaya ya Kongwa, Mkoa wa Dodoma, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhifadhi historia ya mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi na demokrasia barani humo.

Hatua hiyo imetangazwa bungeni leo Jumatatu, Juni 22, 2026 na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda wakati akichangia hoja ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Makonda amesema tayari Serikali imetenga fedha kwa ajili ya mradi huo na imepata eneo la hekta saba litakalotumika kujenga kituo hicho, ambacho kitakuwa sehemu ya kumbukumbu ya historia ya ukombozi wa nchi mbalimbali za Afrika.

“Tunataka kizazi cha Afrika kijue kilikotoka. Tanzania ilitoa mchango mkubwa katika harakati za ukombozi wa bara hili na ni muhimu historia hiyo ikatunzwa na kufundishwa kwa vizazi vijavyo,” amesema.

Amesema mradi huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhifadhi maeneo yaliyokuwa kitovu cha harakati za ukombozi, ikiwemo Kongwa, ambayo ilitumika kama kambi ya wapigania uhuru wa Namibia na mataifa mengine ya Kusini mwa Afrika.

Makonda amesema Rais wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah, alipotembelea Kongwa hivi karibuni alieleza utayari wa nchi yake kushirikiana na Tanzania katika kuhifadhi historia hiyo.

Uwekezaji sekta ya michezo

Mbali na mradi huo, Makonda amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya michezo, akieleza kuwa michezo ni chanzo kikubwa cha ajira, umoja wa kitaifa na kuitangaza Tanzania kimataifa.

Amesema kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Michezo mwaka 2022 kupitia asilimia tano ya mapato yatokanayo na shughuli za kubashiri kumesaidia kuimarisha uwezo wa timu za taifa na kupunguza utegemezi wa misaada.

Kwa mujibu wa Makonda, Tanzania kwa sasa ina timu 15 za taifa katika ngazi mbalimbali za wanaume na wanawake, hali inayotoa matumaini ya mafanikio makubwa katika siku zijazo.

Ametaja mafanikio ya timu za vijana za chini ya miaka 17 na 20 zilizoshiriki mashindano ya kimataifa, akisema Serikali inalenga kuona Tanzania ikifuzu Kombe la Dunia ifikapo mwaka 2030.

“Safari ya kufuzu Kombe la Dunia tumeianza. Tuna vijana wenye vipaji na tunawekeza katika ngazi za chini ili kujenga timu imara ya taifa kwa miaka ijayo,” amesema.

Katika hatua nyingine, Makonda amesema Tanzania itaendelea kuimarisha nafasi yake kama kitovu cha lugha ya Kiswahili duniani kufuatia kutambuliwa kwa lugha hiyo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Amesema zaidi ya watu milioni 500 duniani wanatumia Kiswahili na kwamba Tanzania itaendelea kutumia lugha hiyo kama nyenzo ya kuimarisha umoja, utamaduni na ushirikiano wa kimataifa.

Pia amewahimiza Watanzania kujiandaa kutumia fursa za kiuchumi zitakazotokana na mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, akisema tukio hilo litafungua fursa katika sekta za utalii, usafiri, malazi na biashara mbalimbali.

“AFCON 2027 ni fursa kubwa ya kuitangaza Tanzania na kuongeza mapato kwa wananchi na taifa kwa ujumla,” amesema.

Michuango ya AFCON 2020 itafanyika Uganda, Kenya na Tanzania na tayari mataifa hayo yamekwisha kuanza maandalizi ikiwemo ujenzi wa viwanja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *