Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema imeanza kutekeleza hatua mbalimbali zinazogusa masuala yaliyomo katika muswada uliowasilishwa katika Bunge la Seneti la Marekani dhidi ya Tanzania, huku ikisisitiza mchakato wa muswada huo bado uko hatua za awali na huenda usifikie kuwa sheria.

Katika mawasiliano yake na Mwananchi leo, Jumapili, Juni 21, 2026, Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Elsie Kanza, amethibitisha Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Seneti la Marekani kupeleka muswada huo kwenye Bunge zima la Seneti kwa ajili ya kujadiliwa, akibainisha kuwa bado kuna hatua nyingi za kisheria kabla ya kufikia uamuzi wa mwisho.

“Ni kweli kuwa, katika hatua za awali, Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Seneti la Marekani imepeleka muswada dhidi ya Tanzania kwenye Bunge zima la Seneti kwa ajili ya kujadiliwa. Hata hivyo, ni vyema kufahamu kuwa muswada huo upo kwenye hatua za awali kabisa na mchakato bado ni mrefu,” amesema Balozi Kanza.

Kamati hiyo imepitisha muswada huo unaolenga kuimarisha usalama wa taifa la Marekani, kulinda masilahi yake duniani na kupitia upya uhusiano wa nchi hiyo na mataifa washirika duniani, ikiwemo Tanzania.

Muswada huo umeibua mjadala mpana kutokana na wasiwasi uliooneshwa na baadhi ya wabunge wa Marekani kuhusu masuala ya utawala, haki za binadamu na matukio yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 nchini Tanzania.

Juni 17, 2026, mwenyekiti wa kamati hiyo, Seneta Jim Risch, akishirikiana na Seneta Jeanne Shaheen, walitoa taarifa baada ya wajumbe wa kamati hiyo kukamilisha kikao kazi na kupitisha muswada huo kwa makubaliano ya vyama vyote viwili.

Miongoni mwa sheria zilizopitishwa na kamati hiyo ni pamoja na muswada wa S.4577 wa “Sheria ya Kupitia Upya Uhusiano wa Pande Mbili kati ya Marekani na Tanzania,” uliowasilishwa na maseneta Ted Cruz na Jeanne Shaheen.

Baada ya hatua hiyo, muswada huo sasa unakwenda kwenye Bunge la Seneti kupigiwa kura na, endapo utapitishwa, utakwenda kutiwa saini na Rais wa Marekani.

Mbali na muswada huo unaoigusa Tanzania, kamati hiyo imepitisha sheria nyingine, ikiwemo ile ya usalama nchini Sudan, sheria ya kulinda uhuru wa kidini duniani, kupambana na ukiukwaji wa haki za binadamu nchini China, pamoja na ya kuimarisha ushirikiano wa kiteknolojia na kiulinzi katika ukanda wa Indo-Pacific na Taiwan ili kulinda masilahi ya nchi hiyo duniani.

Hata hivyo, Balozi Kanza amesema mambo mengi yanayoelezwa katika muswada huo yameanza kufanyiwa kazi na Serikali ya Tanzania chini ya mwongozo wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwa mujibu wa balozi huyo, hatua hizo zilianza kwa kuundwa kwa Tume ya Kuchunguza Matukio ya Ghasia na Uvunjifu wa Amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Katika ripoti ya tume hiyo iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande, ambayo aliikabidhi kwa Rais Samia Aprili 23, 2026, ilionesha watu 518 waliuawa, kujeruhiwa na kuharibika kwa mali za umma na binafsi.

Amesema hatua nyingine ni kuundwa kwa Tume Maalumu ya Kuchunguza Makosa ya Jinai yaliyotokea katika kipindi hicho, huku Serikali ikiendelea kuandaa hatua nyingine za muda mrefu.

“Serikali pia inaendelea na michakato mingine itakayofuata, ikiwemo kuanzisha mchakato wa kupata Katiba mpya na Tume ya Maridhiano pamoja na kutekeleza mapendekezo mengine ya tume tajwa,” amesema Balozi Kanza.

Amesisitiza masuala mengi yanayorejelewa ndani ya muswada huo si mambo mapya kwa Serikali, kwani tayari yapo kwenye mpango wa utekelezaji uliopangwa.

“Masuala mengi yanayoelezwa kwenye muswada husika tayari Serikali inayafanyia kazi, na mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametoa ratiba ya mpangilio wa utekelezaji wa masuala hayo,” amesema.

Pamoja na mjadala unaoendelea kuhusu muswada huo, Balozi Kanza amesema jambo la msingi zaidi ni kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Marekani.

“Jambo la msingi katika yote yanayoendelea ni nia dhabiti ya Serikali ya Tanzania na Marekani kuendelea kushirikiana na kudumisha uhusiano baina yao kwa manufaa ya nchi hizo zenye urafiki wa kihistoria na watu wake,” amesema.

Amesema dhamira hiyo ilisisitizwa tena wakati wa ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, jijini Washington, D.C., ambako pande hizo zilijadiliana namna ya kuendeleza ushirikiano wa muda mrefu huku kila upande ukiendelea kufuatilia hatua za muswada huo ambao kwa sasa unasubiri hatua zaidi ndani ya Seneti ya Marekani.

Ulivyoanza

Muswada unaoihusu Tanzania uliwasilishwa Mei 20, 2026, ukihusishwa na matukio ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa Oktoba 29, 2025, ambapo Marekani ilieleza wasiwasi kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu na kudhoofika kwa misingi ya kidemokrasia.

Katika toleo lake la awali, muswada huo ulipendekeza tathmini ya kina ya uhusiano wa Marekani na Tanzania katika diplomasia, usalama, biashara na misaada ya maendeleo.

Pia, ulipendekeza kusitishwa kwa baadhi ya misaada ya usalama na maendeleo pamoja na kupitia upya ushirikiano wa kibiashara kupitia taasisi kama Millennium Challenge Corporation (MCC).

Aidha, ulifungua uwezekano wa vikwazo vya viza na kufungia mali kwa watu watakaobainika kuhusika na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, pamoja na kuhitaji tathmini ya uhusiano wa Tanzania na China na Russia.

Hata hivyo, kabla ya kupitishwa, Seneta Shaheen aliwasilisha marekebisho yaliyopunguza ukali wa baadhi ya vipengele, ikiwamo kuondolewa kwa pendekezo la kusitisha ushirikiano wa kijeshi kati ya Marekani na Tanzania.

Pia, marekebisho mapya yaliondoa masharti yaliyohusu misaada ya usalama, yakibakiza vikwazo vinavyohusu ufadhili wa maendeleo.

Muswada huo uliorekebishwa unaendelea kupendekeza kuzuiwa kwa ufadhili wa Shirika la Millennium Challenge Corporation (MCC) kwa Tanzania hadi masharti maalumu yaliyowekwa yatakapotekelezwa.

Mabadiliko mengine kabla ya muswada huo kupigiwa kura kwenye Bunge la Seneti ni kuingizwa kwa kifungu kinachoruhusu msamaha kwa kuzingatia masilahi ya taifa la Marekani.

Chini ya marekebisho hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani atakuwa na mamlaka ya kuondoa au kusamehe vikwazo vya misaada na uwekezaji ikiwa ataona hatua hiyo inalinda masilahi ya Marekani. Kifungu hicho hakikuwepo katika muswada wa awali.

Aidha, marekebisho hayo yamebadilisha mfumo wa vikwazo uliopendekezwa. Badala ya kuanzisha mfumo mpya wa vikwazo, muswada huo sasa unapendekeza matumizi ya sheria iliyopo ya Global Magnitsky kuwachukulia hatua watu binafsi watakaobainika kuhusika na ukiukwaji wa haki za binadamu au vitendo vya rushwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *