Vancouver, Canada. Misri imejiweka kwenye nafasi nzuri ya kutinga hatua ya 32 Bora ya Kombe la Dunia 2026 baada ya kuichapa New Zealand mabao 3-1 na kukaa kileleni mwa Kundi G.

Matokeo hayo yameifanya Misri kufikisha pointi nne baada ya mechi mbili, kufuatia sare ya 1-1 dhidi ya Ubelgiji kwenye mchezo wa kwanza. Wakati huo huo Iran na Ubelgiji zina pointi mbili kila mmoja baada ya kutoka sare tasa ya 0-0, huku New Zealand ikisalia mkiani ikiwa na pointi moja.

Kabla ya mechi za leo timu zote nne zilikuwa zimekusanya pointi moja moja baada ya mechi za kwanza, hali iliyofanya Kundi G kuwa moja ya makundi yenye ushindani mkubwa zaidi katika mashindano hayo.

Ushindi wa leo umewapa Mafarao nafasi ya kuamua hatima yao wenyewe katika mchezo wa mwisho dhidi ya Iran.

Mshambuliaji wa Misri, Mohamed Salah wakati akishangilia bao katika mechi ya Kombe la Dunia 2026 dhidi ya New Zealand. Picha na Mtandao

Katika mechi hiyo iliyochezwa Vancouver, New Zealand ndiyo ilianza kupata bao dakika ya 15 lililofungwa na Finn Surman bao lililodumu dakika zote 45 za kipindi cha kwanza.

Hata hivyo, Misri ilibadilika kipindi cha pili na dakika ya Mostafa Ziko alisawazisha kabla ya Mohamed Salah kuongeza la pili dakika ya 67, dakika 16 baadae Trezeguet aliandika bao la tatu lililozima kabisa matumaini ya New Zealand kupata ushindi.

Matokeo hayo yana maana kwamba Misri inahitaji sare dhidi ya Iran katika mechi ya mwisho ili kuwa kwenye nafasi nzuri ya kufuzu. Ushindi wowote dhidi ya Iran utaifanya timu hiyo kumaliza hatua ya makundi ikiwa kinara wa kundi.

Kwa upande wa Iran, sare dhidi ya Ubelgiji imewaweka hai kwenye mbio za kufuzu lakini sasa watalazimika kutafuta ushindi dhidi ya Misri.

Kipa Alireza Beiranvand alikuwa shujaa wa Iran baada ya kuokoa hatari nyingi na kuinyima Ubelgiji ushindi.

Baadhi ya wachezaji wa Misri wakishangilia baada ya kupata ushindi wa 3-1 dhidi ya New Zealand. Picha na Mtandao

Ubelgiji nayo imejikuta kwenye presha kubwa, kwani licha ya kuwa miongoni mwa timu zilizopewa nafasi kubwa kabla ya mashindano, imekusanya pointi mbili na sasa inalazimika kuifunga New Zealand katika mchezo wa mwisho ili kuboresha nafasi ya kusonga mbele.

Kwa hali ilivyo sasa, Kundi G bado halijatoa timu iliyofuzu wala iliyoaga mashindano. Hata hivyo, ushindi wa Misri umebadili kabisa hesabu za kundi hilo na kuifanya timu ya Mohamed Salah kuwa karibu zaidi na tiketi ya hatua ya mtoano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *