Mamlaka za Iraq zinajitayarisha kwa ajili ya kupokea mamilioni ya mazuwari wa Waislamu wanaoendelea kumiminika katika mji mtakatifu wa Karbala kwa ajili ya siku za Tasu’a na Ashura na kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (SAW), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (AS).

Shughuli hiyo ya kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Hussein (AS), hushika kasi zaidi kila mwaka tarehe 9 na 10 Mfunguo nne Muharram ikishirikisha mamilioni ya Waislamu kutoka maeneo mbalimbali ya dunia.  

Marasimu ya Siku ya Tasu’a yameanza jioni ya leo hapa nchini Iran ambapo mamilionii ya wananchi wamekusanyika misikitini na katika vituo na maeneo mbalimbali.

Waombolezaji katika kona zote za Iran wametangaza kwa sauti kubwa utiifu wao kwa mapambano ya Karbala, huku wakijibari na kujiweka mbali na maadui wa Uislamu na wa Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad SAW.

Katika siku ya 9 ya mwezi Muharram, waombolezaji humkumbuka zaidi Abul Fadhl Abbas bin Ali (AS), ndugu yake Imam Hussein AS ambaye ndiye aliyekuwa mbeba bendera na kamanda wa jeshi la mtukufu huyo katika mapambano ya siku ya Ashura dhidi ya utawala dhalimu wa Yazid bin Muawiya.

Karbala, Iraq

Abul Fadhl alionesha ushujaa wa hali ya juu katika mapambano ya Karbala na kuwakumbusha watu ushujaa usio na kifani wa baba yake, Ali bin Abi Twalib (AS). Abul Fadhl Abbas aliuawa shahidi tarehe kumi Muharram baada ya kukatwa mikono miwili na maadui wa Watu wa Nyumba ya Mtume wetu Muhammad SAW ambao kinara wao alikuwa alikuwa Yazid bin Muawiyah.

Kilele cha maombolezo ya Muharram kitakuwa tarehe 10 siku inayojulikana kwa jila la Ashura ambapo Imam Hussein (AS) na watu wengine wa familia ya Mtume Muhammad na wafuasi wao waaminifu waliuawa kikatili baada ya mapambano ya kishujaa yaliyobakia hai katika historia ya wanadamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *