
Wazungu walitawaliwa na Waarabu. Vuguvugu la Koo ya Umayyad (Khalifa ya Umayyad), kutoka Saudi Arabia, iliangusha dola nyingi Mashariki ya Kati, ikakamata Peninsula ya Iberian, ambayo sasa ndiyo Hispania na Ureno. Yalikuwa matokeo yaliyojiri mwaka 711 Baada ya Kalenda (BK).
Vikosi vya Waarabu vikiongozwa na Tariq ibn Ziyad, vilivuka Mlango Bahari wa Gibraltar, mwanzoni mwa muongo wa pili, Karne ya Nane, wakauangusha Ufalme wa Visigothic (Visigothic King Roderic), na kuishikilia peninsula ambayo ni sehemu ya Hispania na Ufaransa leo.
Ottoman ni dola ya Waarabu iliyokuwa na misuli mikubwa na imara (the superpower), ulimwenguni. Ilitawala Bara la Asia, ikaingia Ulaya na kuwapigisha magoti Wazungu, wakafika mpaka Afrika. Kuanzia mwaka 1299 mpaka 1922, ni zaidi ya miaka 600 ya utawala wa Ottoman.
Nguvu ya Ottoman ilianzia Anatolia, ambayo ndiyo Uturuki ya sasa, ikaingia Balkans, ambayo ndiyo nchi za Albania, Bulgaria, Croatia, Bosnia na Herzegovina. Ottoman waliishika Ugiriki, Serbia, Hungary, na dola nyingine za Ulaya na Afrika.
Miaka 600 mpaka 800, ni tarakimu za Waarabu kuwatawala Wazungu. Hispania ilikaliwa na Waarabu kuanzia Karne ya Nane hadi miaka nane kabla ya kuanza Karne ya 16. Yaani, mwaka 1492, ndipo Sultani ya Granada ilianguka, baada ua kuzidiwa na Falme za Kikatoliki. Ni nyakati za Dola za Papa (Papal States).
Istanbul, ni mji ulioanzishwa mwaka 324 (Karne ya Nne). Awali uliitwa New Rome (Roma Mpya), lakini baadaye ukapewa jina la Constantinople. Ni kipindi cha utawala wa Constantine the Great. Ottoman iliitwaa Constantinople na kuifanya Uturuki kuwa ya Waarabu hadi leo.
Kuanzia Karne ya 15, baada ya Wazungu kuwaondosha Waarabu kwenye himaya zao, walianza kujipanga nao kuitawala dunia. Afrika, Amerika Kusini na Amerika Kaskazini, waliyaona ni mabara rahisi kuyashika.
Kwetu Afrika, Wareno walikuwa na kasi kubwa kuanzia Karne ya 15. Safari za baharia mpelelezi, Vasco da Gama, Bahari ya Hindi na kuzunguka Rasi ya Tumaini Jema, Bahari ya Atlantiki, yakafuata matokeo ya kujengwa kwa Ngome ya Mtakatifu George mwaka 1482. Ngome ya Mtakatifu George kwa sasa inaitwa Ngome ya Elmina, Ghana.
Miaka 101 baada ya Ngome ya Mtakatifu George (Elimina Castle), Wareno walijenga Ngome ya Yesu, Mombasa, kuanzia mwaka 1593 na kukamilika mwaka 1596. Ngome hizo zilianzishwa kwa utambulisho wa vituo vya biashara pwani za Bahari ya Hindi na Atlantiki, kisha zikawa vituo vikuu vya biashara ya usafirishaji wa watumwa.
Nimetanguliza muhtasari huo mrefu ili kujenga hoja na ifike sawasawa kuwa Wazungu walijifunza kutoka kutawaliwa na Waarabu, wakaona makosa na udhaifu wao, wakajisahihisha, wakajipanga, wakawafukuza Waarabu na kujitawala, hawakauishia hapo, wakaanza safari ya kuitawala dunia, na walifanikiwa.
Wazungu wamekuwa mbele kwa kujifunza haraka, kutoka kwa Waarabu, wakajiongeza kupitia utamaduni wao, wakaanza safari ya kuifanya dunia itambue kwamba wao (Wazungu), ndiyo jumuiya bora ulimwenguni. Ujenzi wa fikra kwamba wao ni bora huanzia mwanzoni kabisa wakati mtoto anapozaliwa. Analelewa na kukuzwa akitambua yeye ni mtu wa thamani ya daraja la kwanza duniani.
Imekuwa tofauti na Afrika. Waarabu na Wazungu wameitawala ardhi ya Afrika kwa nyakati tofauti. Haikuwezekana kuwaondosha kwa lazima, ni mpaka walipotaka wenyewe kuachia. Athari kubwa ambayo imebaki vichwani mwa Waafrika ni kutekwa na tamaduni za wakoloni.
Haikuwezekana kujifunza kwa Wazungu na Waarabu, kisha kujiongeza kupitia tamaduni asilia ili kuunda ustaarabu wa kipekee. Waafrika walichoamua ni kuona ustaarabu wa kikoloni ni bora, unaofaa kufuatwa bila kupunguza. Waafrika wamekuwa wafuasi wa kudumu wa Wakoloni.
Maeneo mengi, Wazungu wameteka. Yale ambayo Waarabu waliweka mizizi yao, Waafrika wamekuwa na Uarabu mwingi kuliko asili yao. Upande wa Wazungu ni mgawanyiko. Maeneo yaliyokaliwa na Ufaransa, wao huona Paris ni peponi. Waliotawaliwa na UK, London huitafsiri kama hija. Vivyo hivyo kwa Ubelgiji na Brussels.
Fikra hizohizo zimefanya kila kinachofanywa na Wazungu na Waarabu kipokelewe kwa mikono miwili Afrika, na kuona ndicho kinafaa kwa ustaarabu, fasheni na mitindo yote. Muziki wa kitamaduni Afrika, hauna thamani kwa Waafrika, ambao wamechagua kuona Wazungu ndiyo wanamuziki daraja la kwanza.
Filamu, mavazi, mpaka siasa, Waafrika wanaiga Wazungu. Demokrasia ya Wazungu, ndiyo inayofaa ulimwenguni. Waafrika wanapotofautiana kisiasa, wanakimbilia kuomba msaada kwa Wazungu, kwamba wenyewe ndiyo wenye uwezo mzuri wa kutatua migogoro. Wana busara kupita Waafrika.
Nchi za Afrika zinatengeneza bajeti kwa kutegemea misaada ya Wazungu. Unajiuliza, kwa nini nchi hazijipangii bajeti kulingana na mapato yao? Matokeo yake, katikati ya utekelezaji wa bajeti, wenye fedha zao wanagoma kutoa kwa sababu kuna mambo wanayataka, nchi ineshindwa kuyatekeleza. Utumwa wa bajeti.
Waafrika wanapoona uongozi wa nchi zao hautendi wanavyotaka, wanakimbilia kuomba misaada kwa Wazungu ili waendeshe vuguvugu za ndani, nje, na mitandaoni. Matokeo yake, Wazungu ndiyo wanakuwa waamuzi wa namna siasa za ndani ya nchi za Afrika ziendeshwe. Na wanatoa hifadhi ya makazi kwa wakimbizi wa kisiasa.
Wazungu wakisitisha misaada kwa nchi ya Afrika, kuna raia wa nchi husika wanashangilia. Ushangiliaji huo haumaanishi kwamba ni mwanzo wa kupambana kujitegemea, bali wanatafsiri kama uongozi uliopo madarakani unakuwa umekomolewa.
Nchi ya Ulaya ikifunga ubalozi kwenye nchi ya Afrika inakuwa pigo kwa nchi iliyofungiwa. Marekani wakisitisha visa zao kwa watu wa Afrika, inahesabika ni adhabu. Kuna namna lazima ufanyike ukombozi wa kifikra kwa Mwafrika. Kutawaliwa na Wazungu na Waarabu haikuwa jambo la fahari, mpaka kuona Wakoloni ni bora. Hapana.
Mwandishi wa kitabu “The African Origin of Civilization” – “Asili ya Ustaarabu Afrika”, Cheikh Anta Diop, ambaye ni raia wa Senegal, alipata kusema kuwa sababu Waafrika wanakuwa nyuma na kutukuza Wazungu ni kwa sababu serikali za Afrika haziwekezi kwenye utafiti, ili Waafrika wenyewe wajitambue vema.