Hai. Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Hassan Abbasi, amewataka watendaji wa viwanja vya ndege na wadau wa sekta ya utalii nchini kuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza na kuilinda taswira ya Tanzania kupitia huduma bora na mapokezi mazuri kwa wageni watakaowasili nchini wakati wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Dk Abbasi amesema hatua hiyo ni muhimu wakati Tanzania ikiendelea na maandalizi ya kuandaa na kushiriki mashindano hayo, akisisitiza kuwa huduma bora na ukarimu vitachangia kwa kiasi kikubwa kuijengea nchi taswira chanya mbele ya wageni wa kimataifa.
Ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na watendaji wa viwanja vya ndege pamoja na baadhi ya wadau wa sekta ya utalii nchini katika mafunzo ya utayari kwa watoa huduma katika mnyororo wa thamani wa utalii, yaliyofanyika katika ofisi za Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
“Mafunzo haya ni mwendelezo wa mkakati wa wizara yetu katika msimu wa utalii ambao umeanza, lakini pia tukio kubwa la AFCON. Wenzetu wa viwanja vya ndege ni mawakala wa kwanza na mabalozi wa kupokea wageni. Kabla mgeni hajafika Serengeti au Ngorongoro, taswira ya kwanza ya nchi anaipata hapa,” amesema Dk. Abbasi.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya maandalizi ya kuhakikisha Tanzania inanufaika kikamilifu na fursa ya kimataifa ya AFCON kwa kuitangaza nchi kwa njia chanya.
Baadhi ya watendaji wa viwanja vya ndege pamoja na baadhi ya wadau wa sekta ya utalii nchini wakiwa katika mafunzo ya utayari kwa watoa huduma katika mnyororo wa thamani wa utalii, yaliyofanyika katika ofisi za Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA). Picha na Janeth Joseph
“Tunataka kuhakikisha hatufanyi makosa ya hapa na pale yanayoweza kuharibu taswira ya nchi. Hii ni sehemu ya maandalizi ya AFCON,” amesema Dk. Abbasi.
Dk. Abbasi aliwataka watendaji hao kutambua nafasi yao muhimu kama “frontline” ya taifa katika kuwahudumia wageni, akisema wao ndio watu wa kwanza kukutana na wageni wanaowasili nchini.
“Tunaomba sana mtimize majukumu yenu kwa weledi. Mnafanya vizuri lakini zipo changamoto chache, na ndiyo maana tupo hapa kuhakikisha mnajitambua kuwa ninyi ni sehemu ya taswira ya nchi. Mkiwa frontline, mnaamua mgeni ataona Tanzania vipi,” amesema Dk Abbasi
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Ofisa Rasilimali Watu wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Godfrey Mwakilovele, amesema KIA inao ushirikiano mkubwa na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) pamoja na TANAPA kutokana na shughuli zake kuhusiana kwa karibu na sekta ya utalii.
“Tunaamini hili limekuja wakati mwafaka kwani tupo kwenye maandalizi ya AFCON. Tunatarajia kuwa na wageni na mashabiki takribani milioni 1.5. Wizara imetambua nafasi yetu muhimu katika sekta hii, ambapo mchango wa utalii kwenye pato la taifa ni mkubwa,” amesema Mwakilovele