Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya amesema ukimya wake katika siasa unasababishwa na mambo matatu, ukiwemo mwenendo wa sasa chama chake hicho, anaodai hauridhishi.

Sababu nyingine, mbunge huyo wa zamani wa Kaliua amesema anataka kujikita zaidi katika shughuli binafsi na majukumu ya kifamilia ikiwemo kumuuguza mama yake.

Sakaya ameeleza hayo baada ya ukimya wa takriban miezi minne tangu alipomaliza muda wake wa uongozi kwenye wadhifa wa naibu katibu mkuu wa CUF Tanzania Bara na mjumbe wa kamati ya uongozi wa chama hicho.

Hata hivyo, wakati Sakaya akieleza hayo, Mwenyekiti wa CUF, Mirambo Yusuf amesema hoja ya kwamba mwenendo wa chama hicho hauridhishi, si ya kweli.

“Moja ya majukumu ya chama cha upinzani ni kuangalia upungufu wa Serikali ili kuyaweka wazi. Kazi yetu ni kueleza sera mbadala ili wananchi wazipime na kutupa kura za kutosha katika uchaguzi, zitakazotupa ushindi wa dola, majimbo na kata,” amesema Mirambo, akisisitiza jukumu hilo wanalitekeleza.

Alichokisema Sakaya

Katika mazungumzo yake na Mwananchi, Sakaya amesema kwa sasa amempumzika kidogo shughuli za kisiasa, akijikita zaidi na kuangalia familia yake.

“Nimepunguza kidogo mambo ya siasa, ukizingatia mama yangu ana changamoto za kiafya, hivyo anahitaji uangalizi wa karibu.

“Muda mwingine mama yangu yupo hospitalini, nimeamua kutumia muda wangu mwingi kuwa karibu naye, mambo ya familia yamenibana kidogo,” ameeleza.

Sakaya amesema kwa nyakati tofauti amekuwa akienda katika hospitali mbalimbali jijini Dar es Salaam, ikiwemo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), hivyo anajikuta anashindwa kufanya shughuli zingine za kisiasa.

“Sijaacha siasa, lakini kwa sasa nimepumzika kidogo nikishughulikia mambo ya familia kwanza. Pale ninapoweza kufanya nafanya, lakini si kwa muda wote kama zamani,” amesema.

Sakaya ambaye mbali na ubunge wa jimbo pia aliwahi kuwa mbunge wa viti maalumu, amesema pale anapoweza kufanya shughuli fulani anashiriki lakini si kwenda katika mikutano ya hadhara na kuhutubia kama zamani.

Sababu nyingine

Sakaya amebainisha kuwa sababu nyingine iliyofanya kurudi nyuma kuwa ni mwenendo wa chama chake, akisema hauridhishi na kuwa sasa CUF si ile iliyokuwa ikitingisha miaka ya nyuma.

“CUF baada ya kuondolewa kwa viongozi waliokuwa wanatetea na wanapambana kwa masilahi ya wananchi, iliyokuwa inaisema Serikali, kuikosoa Serikali hamtaiona tena. Waliowekwa wamewekwa na system (mfumo) wanaambiwa semeni hiki semeni hiki, ile ya kusimama kidete kuongea vitu vyenye uhalisia haipo tena.

“Waliokuwepo wameshindwa kulifanya hilo, na hilo ni miongoni mwa vitu vilivyorudisha moyo wangu nyuma katika harakati za siasa,” amesema Sakaya.

Desemba 18 na 19, 2024, CUF ilifanya mkutano mkuu uliompa ushindi Profesa Lipumba kuendelea kukalia kiti lakini liibuka kundi la wananchama likalalamika kuwa haukukidhi matakwa ya Katiba inayoelekeza mshindi wa uenyekiti sharti apate zaidi ya nusu ya kura za wajumbe wa mkutano huo.

Februari 13, 2026, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ilibatilisha uchaguzi huo.

Februari 21, 2026, uchaguzi wa marudio ulifanyika. Lakini Profesa Lipumba hakuchukua fomu ya kuomba kuchaguliwa tena. Matokeo yalipotangazwa, nafasi ya Mwenyekiti ikachukuliwa na Mirambo Yusuf.

Sakaya, amedai kazi ya kwanza ya uongozi uliochukua madaraka baada ya kuondolewa kwa Profesa Lipumba, ilikuwa kuwashughulikia yeye na wenzake ambao walionekana kuwa upande fulani.

“Kwenye kikao chao kwanza walihakikisha Sakaya anatolewa kwenye nafasi yake, naibu katibu mkuu Zanzibar aliondolewa. Kila aliyehoji kutaka maelezo kuhusu hatua hizi alitolewa nje ya ukumbi,” amesema.

Aidha, Sakaya amejipambanua kuwa yeye ni mwanasiasa mwenye msimamo, asiyeyumbishwa akisimamia kile anachokiamini na anazungumza ukweli siku zote.

“Mimi kama kisu nasema kisu na sio uma, huwezi kuniambia hiki ni kisu halafu niseme uma. Kwa lugha nyepesi sina siasa ya unafiki ya kuambiwa sema hiki, sema kile, kufungwa mdomo siwezi, bora nikae pembeni nifanye mambo mengine,” amesema Sakaya.

Kwa mujibu wa Sakaya, mbali na kuwa karibu na masuala ya familia, kwa sababu anafanya shughuli nyingine inayomfanya kuwa ‘bize’, amemua kuwa mtazamaji kwa kile kinachoendelea ndani ya CUF.

Kauli ya Mirambo

Akijibu madai hayo ya Sakaya, Mirambo amesema hapendi kumjadili Sakaya badala yake anamtunzia heshima yake kiongozi huyo wa zamani.

“Mtu anaposema uongozi wa sasa haupo tayari kuwasemea wananchi, swali la kujiuliza yeye katuona tumesema wapi? Au wapi tumesema tofauti na utashi wa wananchi?” amesema.

Mirambo ameifananisha hatua hiyo na watu waliokaa na kutabiri, akisema yeye hajamzungumza kitu tofauti na mahitaji ya Watanzania au kuisifia Serikali.

“Mimi bado nipo vizuri katika upinzani na wao wanajua hilo. Wote wanajua nipo vizuri katika upinzani, tena nawazidi wao, tatizo sijapata sauti na sijawa mbunge kama wao,” amesema Mirambo.

Mirambo amesema si kweli kwamba uongozi mpya umewatimua baadhi ya watu waliokuwa wakimuunga mkono Profesa Lipumba, ndiyo maana hata katika safu ya uongozi aliyoiunda wamo viongozi waliokuwa wakimuunga mkono mwenyekiti huyo wa zamani.

“Kuna wenzangu katika uteuzi waliwapinga (viongozi wapya), lakini bado hadi sasa wamo kwenye ukurugenzi wa chama. Hata maofisa wa chama hawajabadilishwa, wote wapo, wasiokuwepo ni wale ambao walikuwa na ukakasi,” ameeleza Mirambo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *