
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, ameapa kukabiliana na jaribio lolote la kuyumbisha taifa wakati wa maandamano yaliyopangwa kufanywa wiki ijayo dhidi ya wahamiaji, huku wimbi la chuki dhidi ya wageni lizidi kuongezeka nchini humo.
Ni baada ya makundi yanayoongozwa na raia kutangaza Jumanne tarehe 30 Juni kama tarehe ya mwisho kwa wageni wasio na vibali kuondoka nchini Afrika Kusini na kutoa wito wa maandamano ya kitaifa dhidi ya uhamiaji haramu.
Kauli hiyo isiyo rasmi imezidisha hofu ya kuibuka tena machafuko yanayochochewa na chuki dhidi ya wageni ambayo yamesababisha vifo vya makumi ya watu.
“Hatutavumilia jaribio la mtu yeyote la kuivuruga nchi, iwe kwa maandamana au vinginevyo,” amesema Rais Ramaphosa.
“Vikosi vyetu vya usalama viko tayari, na wale wanaokiuka taratibu tunazoweka watakumbana na nguvu ya sheria,” amesema Cyril Ramaphosa katika Bunge la Juu.
Polisi ya Afrika Kusini imetangaza kuwa itaimarisha ulinzi kote nchini Juni 30 huku maafisa wa serikali wakizidisha juhudi za kuhakikisha utulivu.
Nchi hiyo imekuwa katika wakati mgumu kufuatia wiki kadhaa za machafuko ya chuki dhidi ya wageni (xenophobic) ambayo wakati mwingine yamesababisha vifo vya watu.
Kampeni ya kupinga wahamiaji nchini Afrika Kusini tayari imewalazimisha maelfu ya raia wa kigeni kurejea makwao, ikiwa ni pamoja na raia wa Ghana, Malawi, Msumbiji na Nigeria.
Kambi za muda zimeongezeka katika mji wa bandari wa Durban na mji mkuu wa kifedha, Johannesburg huku maelfu ya wageni wakisubiri usafiri wa kurudi katika nchi zao, jambo ambalo limefafanya makundi ya misaada ya kibinadamu kutoa onyo kuhusu mgogoro mkubwa wa binadamu.
Matukio ya ghasia yaliyopita yaliyowalenga raia wa kigeni wasio na vibali yamekuwa mabaya sana, na watu 62 waliuawa katika ghasia za mwaka wa 2008.
Ghasia za mwaka 2019 zilishuhudia makundi ya watu waliokuwa na silaha yakishambulia biashara zinazomilikiwa na wageni karibu na Johannesburg, na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 12.