Dar es Salaam. Serikali imesema Julai mwaka huu, bei ya mafuta inatarajiwa kushuka nchini, huku ndani ya wiki nne hadi 10 itashuka duniani kote.

Taarifa hiyo ya kupungua kwa bei ya mafuta, inatarajiwa kuleta ahueni kwa bei za bidhaa na huduma mbalimbali, zilizopanda tangu nishati hiyo ilipopanda bei.

Ongezeko la bei ya mafuta limeshuhudiwa tangu Machi mwaka huu, baada ya kutokea vita Mashariki ya Kati vilivyohusisha mataifa ya Marekani, Israel dhidi ya Iran.

Kupanda kwa bei hiyo, kulisababishwa na kufungwa kwa mlango wa bahari wa Hormuz, unaosafirisha asilimia 20 ya mafuta yote yanayouzwa duniani.

Ahueni hiyo, inatarajiwa kutokana na makubaliano ya mataifa hayo ya kusitisha mapigano, yaliyoambatana na kufunguliwa kwa mlango wa bahari wa Hormuz.

Taarifa ya ahueni ya bei hiyo, ilitolewa jana bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, wakati akitoa mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Bagamoyo, Subira Mgalu.

Mgalu, alitaka kujua lini Watanzania watarajie ahueni ya maisha kwa kushuka kwa bei ya mafuta.

Katika majibu yake, Ndejembi alisema kuanzia Julai mwaka huu, wananchi watashuhudia bei ya mafuta ikishuka nchini, huku duniani kote ikitarajiwa ndani ya wiki nane hadi 10.

Alisema pamoja na kupanda kwa bei ya nishati hiyo, lakini haikuwahi kukosekana nchini na hata gharama yake ni ndogo ukilinganisha na mataifa mengine ya Afrika Mashariki.

Kwa kuwa kuna makubaliano ya kusitisha mapigano Mashariki ya Kati, alisema bei ya mafuta imeshuka na kufikia dola 70, hivyo mamlaka nchini zinapaswa kuhakikisha ahueni hiyo inawagusa wananchi.

Alisema hadi sasa kuna meli zinaendelea kupakua mafuta na nyingine ziko njiani kuja Tanzania, hivyo wananchi wasiwe na hofu kwani uhaba wa nishati hiyo hautatokea tena.

Ahueni duniani

Ukiacha ahueni iliyotangazwa na Ndejembi, duniani nako mambo ni shwari, baada ya Iran na Marekani kuafikiana kusitisha mapigano.

Pia, pande hizo zimekubaliana kurejesha usalama wa mlango wa bahari wa Hormuz, ambao ni njia muhimu ya biashara duniani.

Makubaliano hayo yanahusisha kusitishwa kwa mashambulizi, kufunguliwa kwa Hormuz kwa meli za kibiashara kupitia njia maalumu zilizokubaliwa na kuendelea kwa mazungumzo kuhusu masuala mengine ya usalama wa kikanda.

Akizungumzia mwafaka huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi alisema njia ya Hormuz itabaki wazi kwa usafiri wa kibiashara kwa kipindi cha makubaliano ya kusitisha mapigano kitakachodumu kwa miezi miwili.

Hata hivyo, alisema usalama wa meli utafuata utaratibu ulioratibiwa na mamlaka husika.

Hormuz, hupitisha takribani asilimia 20 ya mafuta yote yanayouzwa duniani. Kufungwa au kutishiwa kwa njia hiyo kulisababisha hofu ya upungufu wa mafuta, hali iliyochochea kupanda kwa bei za nishati na bidhaa mbalimbali duniani.

Kabla ya vita, mafuta ghafi yalikuwa yakiuzwa kwa takribani Sh182,000 hadi Sh195,000 kwa pipa. Wakati wa vurugu hizo, bei zilipanda hadi zaidi ya Sh247,000 kwa pipa kutokana na hofu ya kukatika kwa usambazaji.

Hata hivyo, baada ya mwafaka wa kusitisha mapigano na kuanza kurejea kwa meli za mafuta kupitia Hormuz, bei zimeshuka tena hadi takribani Sh179,000 hadi Sh187,000 kwa pipa.

Kupungua kwa bei ya mafuta kunatarajiwa kuwa na athari chanya katika gharama za usafiri, uzalishaji wa viwandani na usafirishaji wa bidhaa.

Bidhaa zilizopanda kwa kasi wakati wa vita ni pamoja na mafuta ya petroli na dizeli, gesi asilia, mbolea, bidhaa za plastiki, bidhaa za ujenzi na huduma muhimu kutokana na kupanda kwa gharama za usafirishaji wa mizigo kwa njia ya bahari, kuongezeka kwa bima za meli na hatari za safari.

Hata hivyo, wataalamu wa uchumi wanasema kuwa nafuu hiyo inaweza kuchukua muda kuonekana kwa watumiaji wa mwisho kutokana na mikataba ya awali ya ununuzi wa mafuta na bidhaa zilizonunuliwa wakati wa gharama za juu na gharama nyingine za biashara.

Mtazamo wa kiuchumi

Akizungumzia matarajio ya ahueni hiyo, Mtaalamu wa Uchumi, Dk Hamis Mwinyimvua akizungumza na Mwananchi kwa simu jana alisema hilo litasababisha kushuka kwa bei za baadhi ya bidhaa zilizopanda kutokana na ongezeko la bei ya mafuta.

“Yule ambaye alikuwa anauza bidhaa bei ya juu kwa sababu amesafirisha na kuzalisha kwa bei kubwa, atapunguza kwa sababu kuna ushindani,” alisema.

Alisema kupungua kwa bei hizo, kutaongeza uwezo wa wananchi kununua na hilo litasisimua shughuli za kiuchumi na maendeleo.

Pia, alisema kushuka kwa bei hiyo ya mafuta kutapunguza hatari ya mfumuko wa bei, ambao pengine gharama zimebaki kama zilivyo sasa kwa muda mrefu hali ingekuwa mbaya baadaye.

Kwa upande wa nauli za usafiri wa umma, amesema abiria wasitarajia kupungua kwa nauli, kwa sababu mara nyingi hazipungui hata inapotokea bei ya mafuta imeshuka.

Lakini, alisema kama kuna ushindani mkubwa, baadhi ya waendeshaji wa magari hayo ya abiria wanashusha nauli ili kuvutia wateja zaidi, hivyo nafuu inaweza kupatikana hapo.

“Kama kuna ushindani hasa mabasi ile bei wanayopewa na Latra, mabasi yanaweza kushusha bei yenyewe. Hivyo kunaweza kuwa na unafuu fulani kwa abiria,” alisema Dk Mwinyimvua.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *