KIGOMA: Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma imetoa Sh milioni 608.9 kwa vikundi 53 vya wajasiriamali kupitia mpango wa mikopo ya 10% ya mapato yake, hatua inayowanufaisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Akizungumza Juni 26, 2026 wilayani humo katika hafla ya utoaji wa mikopo kwa robo ya tatu na ya nne ya mwaka wa fedha 2025/2026, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Hassan Rugwa, amesema mikopo hiyo inalenga kuwawezesha wanufaika kujiongezea kipato na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.


Aidha, Rugwa amewapongeza watumishi wa halmashauri hiyo wakiongozwa na mkurugenzi kwa usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato na matumizi, akibainisha kuwa fedha hizo zimekuwa zikielekezwa katika shughuli zilizokusudiwa, jambo linalodhihirisha mafanikio ya usimamizi huo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Charles Kadogo, amewataka wanufaika wa mikopo hiyo kuitumia kwa uangalifu na kurejesha kwa wakati ili kuwezesha wengine kunufaika katika siku zijazo.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaack Mwakisu, amesema anafurahishwa na ushirikiano mzuri kutoka kwa halmashauri hiyo katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali, yakiwemo ya usimamizi wa asilimia 10 ya mapato ya ndani, akisema yanatekelezwa kama ilivyokusudiwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, CPA Francis Kafuku, amesema ukusanyaji wa mapato ya ndani kupitia kodi mbalimbali unaendelea vizuri, akisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kutambua kuwa kodi wanazolipa hurudi kwao kupitia miradi ya maendeleo, hivyo kuendelea kushiriki kwa ajili ya maendeleo yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *