Dar es Salaam. Umetimia mwaka mmoja tangu staa wa Bongofleva, Mbosso aachie mradi wake wa kwanza tangu aondoke WCB Wasafi, lebo aliyofanya nayo kazi tangu 2018 hadi mapema 2025.
Mradi huo ni Extended Playlist (EP) yake ya pili, Room Number 3 (2025) ambayo ilitoka rasmi Juni 13 mwaka huo ikiwa na jumla ya nyimbo 7 ambazo hakushirikiana na msanii yeyote.
Room Number 3 EP ni mradi unaoonyesha safari ya muziki ya Mbosso na ukuaji wake ikiwakilishwa vipindi vitatu tofauti – kuanzia akiwa Yamoto Band, WCB Wasafi hadi Khan Music akiwa msanii huru kwa sasa.
Ndani ya mwezi mmoja tu, EP hiyo ilikuwa imesikilizwa zaidi ya mara milioni 50 katika majukwaa yote ya muziki mtandaoni (digital streaming) ikiwa ni mara ya kwanza kwa Mbosso kufikia namba hizo ndani ya muda huo.
Moja ya nyimbo zilizoipa sifa kubwa EP hiyo ni Pawa ambao umetayarisha na S2kizzy, mshindi wa Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2023 kama Mtayarishaji Bora wa Muziki wa Bongofleva ikiwa ni tuzo yake ya pili.
Siku chache zilizopita video ya wimbo huo iliyotoka Juni 19, 2025 ikiwa imeongozwa na Director Fole X mkoani Iringa, imefikia rekodi ya kutazamwa (views) YouTube mara milioni 74.1, hatua iliyoifanya Mbosso kuandika rekodi tatu za kipekee kama ifuatavyo.
Mosi, Hiyo ndio video pekee ya Mbosso na Bongofleva yote kwa ujumla kufikia namba hizo ndani ya mwaka mmoja tu, yaani siku 365. Hakuna wimbo wa Mbosso au wanamuziki yeyote wa Bongofleva uliowahi kufanya hivyo.
Hadi kufikia Desemba 31, 2025, Pawa ndio ilikuwa wimbo namba moja katika orodha ya video za Bongofleva zilizofanya vizuri zaidi YouTube kwa mwaka huo licha ya kutoka karibia katikati ya mwaka.
Pawa ilifuatiwa na video za nyimbo nyingine kama Nairobi (Marioo), Tete (Marioo), Furaha (Harmonize), Me Too (Abigail Chams), Salama (Barnaba), Looking For Love (Darassa), Jirani (Jay Melody), Amanda (Zuchu) na Katam (Diamond Platnumz).
Pili; Pawa umeweka rekodi ya kuwa wimbo wa Mbosso ambao video yake imetazamwa zaidi YouTube kwa muda wote, hivyo sasa hiyo ndio kazi yake namba moja katika mtandao huo ulioanza kufanya kazi Desemba 2015.
Hatua hiyo ni baada ya kuipita video ya wimbo, Baikoko (2021) ambao Mbosso alimshirikisha Diamond Platnumz, ambapo sasa umeshuka nafasi ya pili ukiwa umetazamwa mara milioni 73.8.
Kwa hiyo, mbali na Baikoko (2021), ndani ya mwaka mmoja Pawa (2025) imekuja kuzipita video za nyimbo nyingine maarufu za Mbosso kama Hodari (2018), Tamu (2019), Nadekezwa (2018), Amepotea (2023), Fall (2020) n.k.
Tatu, Mbosso anakuwa mwanamuziki wa kwanza aliyeondoka WCB Wasafi na kuweza kuutafuna mfupa mgumu uliowashinda wenzake wote walioachana na lebo hiyo, tena akifanya hivyo ndani ya mwaka mmoja tu.
Mfupa huo ni kitu gani hasa?, wanamuziki walioondoka WCB Wasafi wamekuwa wakibezwa na baadhi ya mashabiki na hata wadau kuwa wameshindwa kutengeneza nyimbo zinazopata namba kubwa kuzidi zile walizotoa wakiwa chini ya lebo hiyo.
Hilo limeonekana kwa Rich Mavoko, Harmonize, Rayvanny na Lava Lava, ambao hadi sasa video zao zilizotazamwa zaidi (most viewed) YouTube kwa muda wote ni zile walizoachia wakiwa bado chini ya WCB Wasafi.
Hata hivyo, Mbosso kupitia Pawa ni rasmi sasa amekivuka kiunzi hicho baada ya mwaka mmoja pekee wa mapambano, hatua inayozidi kumjengea heshima kubwa kama msanii wa kujitengenezea chini ya lebo yake binafsi ya Khan Music.
Pawa ni wimbo unaozungumzia nguvu kubwa iliyopo katika mapenzi ukielezea jinsi upendo unavyoweza kumzidi mtu kihisia. Katika utunzi Mbosso ametumia neno ‘Pawa’ (Power) kama mfano kuonyesha kwamba penzi la mtu anayempenda lina nguvu kiasi kwamba linamfanya ajihisi anapoteza nguvu zake.
Ni wimbo ulipokelewa vizuri ambapo ndani ya kipindi cha mwezi mmoja tangu ulipoachiwa ulisikilizwa (streams) zaidi ya mara milioni 20, zikiwa ni data kutoka katika mitandao yote ambapo unapatikana.
Ikumbukwe kwa mara ya kwanza Mbosso alipata umaarufu akiwa Yamoto Band baada ya kuachia wimbo wao, Ya Moto (2013) uliotengenezwa Vibe Records na Shirko, na kuanzia hapo jina lake limekuwa likijizolea sifa lukuki katika muziki.
Tayari ametoa albamu moja, Definition of Love (2021) pamoja na EP mbili, Khan (2022) na Room Number 3 (2025), huku akishinda tuzo mbili za muziki Tanzania (TMA) peke yake, na moja akiwa na Yamoto Band.