Katika taarifa yake, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeelezea misimamo iliyotangazwa katika taarifa ya pamoja ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani na mawaziri wenzake wa mambo ya nje wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi tarehe 25 Juni, kuwa ni ya uingiliaji, kutowajibika na ya kichochezi.

Taarifa ya Iran sambamba na kuashiria nafasi ya Marekani na baadhi ya tawala za Kiarabu za eneo katika hujuma ya hivi karibuni ya kijeshi dhidi ya Iran, imesisitiza kuwa usalama endelevu katika eneo la Asia Magharibi utapatikana tu kwa ushirikiano wa mataifa ya eneo hili na bila ya uingiliaji wa madola ya kigeni.

Majibu ya Iran kwa tamko la pamoja la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi na Marekani ni ukosoaji wa yaliyomo katika tamko hilo na muhtasari wa utaratibu mpya wa usalama katika eneo baada ya hujuma za Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran. Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, imekosoa vikali uwepo wa kijeshi wa Marekani na madai kuhusu mpango wa amani wa nyuklia wa Iran, uwezo wake wa makombora, Lango Bahari la Hormuz, makundi ya muqawama na maana halisi ya usalama wa eneo.

Mhimili muhimu zaidi wa majibu haya ni kuhojiwa madai ya Marekani kuhusu kuzidhaminia usalama nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi. Ikiashiria vita vya hivi karibuni, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa, kambi za kijeshi za Marekani sio tu kwamba hazijazidhaminia nchi hizo usalama, bali pia zimekuwa jukwaa la kutekelezwa hujuma za kijeshi dhidi ya Iran. Msimamo huu kwa kweli ni mwendelezo wa mtazamo uleule ambao Tehran imekuwa ikiusisitiza kwa miaka mingi, kwamba uwepo wa kijeshi wa nchi za nje ya eneo hili ndicho chanzo kikuu cha ukosefu wa usalama na utulivu katika Asia Magharibi, na kwamba usalama wa kanda unapaswa kudhaminiwa na serikali husika za eneo, na sio na vikosi vya kigeni.

Uchokozi wa kijeshi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran na majibu makali ya Iran kwa uchokozi huo yamethibitisha wazi kuwa mfumo wa “usalama wa kuazimwa” hauna dhamana yoyote ya kiusalama. Baadhi ya nchi za Kiarabu zimeweka rehani usalama wao chini ya mwavuli wa kijeshi wa Marekani katika miongo kadhaa iliyopita, lakini uzoefu wa vita vya karibuni umeonyesha kwamba utegemezi huu si tu haujazuia mapigano, bali umezigeuza nchi hizo, kambi za kijeshi, na miundombinu yazo kuwa sehemu ya mashine ya vita ya Marekani na utawala wa Kizayuni. Kivitendo, usalama ambao ulipaswa kuwa kizuizi kwa manufaa ya nchi hizi umezigeuza kuwa sehemu ya uwanja wa vita.

Hili ndilo jambo ambalo Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeliashiria na kusisitiza kuwa tawala za eneo hazipasi kuruhusu upande wa tatu kutumia ardhi na suhula zao kwa ajili ya kufanya uvamizi wa kijeshi dhidi ya majirani wao. Kwa mtazamo wa Tehran, baadhi ya tawala za Kiarabu, badala ya kuwa na mchango huru katika kudhaminbi usalama wa kikanda, zimekuwa ngao ya kimkakati ya Marekani. Ngao hii inatumikia zaidi maslahi ya kijiopolitiki ya Washington kuliko kulinda usalama wa mataifa ya Kiarabu.

Uzoefu wa uvamizi wa kijeshi wa hivi karibuni dhidi ya Iran umeonyesha kuwa nchi yoyote ambayo ardhi, anga, bandari au vituo vyake vinatumika kama jukwaa la operesheni za kijeshi za madola ya kigeni dhidi ya nchi jirani, bila shaka italazimika kulipa gharama za hatua hiyo ya kisaliti. Kwa sababu hiyo, onyo la Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran linapaswa kuchukuliwa kama wito wa kuangaliwa upya stratijia ya usalama ya mataifa ya Ghuba ya Uajemi, stratijia ambayo kwa miongo kadhaa imejikita katika kuitegemea kikamilifu Marekani katika kudhamini usalama wao.

Lengo jingine la jibu la Iran ni kujaribu kubadilisha mwelekeo wa mazungumzo ya nyuklia. Wakati Marekani na Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Ujemi kwa mara nyingine zinakariri madai ya zamani kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, makombora na ndege zisizo na rubani, Tehran inayachukulia madai haya kama mwendelezo wa mradi wa chuki dhidi ya Iran na kwa mara nyingine imesisitiza mpango wa kuundwa eneo lisilo na silaha za nyuklia katika Asia Magharibi. Msimamo huu kwa hakika unalenga kugeuza maoni ya umma kutoka mpango wa amani wa nyuklia wa Iran kuelekea kwenye maghala ya silaha za nyuklia za utawala wa Kizayuni, ambayo hayako chini ya usimamizi wowote wa kimataifa.

Katika sekta ya ulinzi, jibu la Iran pia liko wazi. Wizara ya Mambo ya Nje inasisitiza kuwa, uwezo wa makombora na ndege zisizo na rubani za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran si suala la majadiliano au mapatano. Uzoefu wa vita vya hivi karibuni umeonyesha, kwa mtazamo wa Tehran, kwamba uzuiaji wa kijeshi ni jambo muhimu sana katika kuzuia kuenea kwa uchokozi wa wavamizi na kuwatwisha gharama. Kwa hiyo, mashinikizo ya kupunguzwa uwezo huu, kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni juhudi za kuhatarisha usalama wake wa taifa.

Iran pia imepinga vikali lugha iliyotumika katika taarifa hiyo ya pamoja kuhusu muqawama wa Palestina na Lebanon. Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran huku ikipinga hatua ya kuyataja makundi ya muqawama kuwa ni “vikosi vya niaba vya Iran,” imesisitiza kuwa, nguvu pekee halisi ya niaba katika eneo hili ni utawala wa Kizayuni wa Israel unaoendeleza uvamizi na uchokozi katika eneo hili kwa uungaji mkono wa kisiasa, kijeshi na kifedha wa Marekani. Kwa mtazamo wa Tehran, mapambano ya ukombozi ya wananchi wa Palestina na Lebanon dhidi ya uvamizi ni haki halali inayowiana na misingi ya sheria za kimataifa na haki ya mataifa ya kujiamulia hatima yao.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia imewasilisha simulizi tofauti kuhusu suala zima la Lango Bahari la Hormuz. Kinyume na sisitizo la Marekani kuhusu uhuru usio na mipaka wa kupita meli katika eneo hili, Tehran imezibebesha Marekani, utawala wa Kizayuni na serikali zilizoshiriki katika uvamizi wa kijeshi dhidi ya Iran, dhima ya kuvurugwa usalama katika eneo. Iran pia inasisitiza kuwa, usimamizi wa njia hiyo ya kistratijia ya majini utafanyika kwa msingi wa makubaliano yaliyofikiwa katika maelewano ya kusimamisha vita na kwa ushirikiano wa mataifa ya pwani, na sio kwa matakwa ya madola ya kigeni.

Majibu ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa tamka la pamoja la Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi na Marekani yanaashiria mgangano uliopo kati ya mitazamo miwili tofauti kuhusu njia za kudhamini usalama wa Asia Magharibi. Mmoja unazungumzia kudhaminiwa usalama wa eneo kupitia muungano wa kijeshi na madola ya kigeni, pamoja na utegemezi wa moja kwa moja kwa Marekani, na wa pili unazungumzia kudhaminiwa usalama wa pamoja, kupitia ushirikiano wa kikanda, na kufutwa kabisa uingiliaji wa kigeni. Uzoefu wa vita vya kulazimishwa vya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran umedhihirisha ukweli kwamba usalama ulioazimwa sio tu hauleti usalama wa kudumu, bali pia unazigeuza nchi wenyeji kuwa ngao ya kistratijia kwa madola ya kigeni na sehemu ya medani ya vita. Kwa mtazamo huo, ujumbe mkuu wa jibu la Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ni kuzitaka serikali za Kiarabu kutazama upya mahesabu yao ya usalama na kuyaelekeza kwenye mfumo wa kieneo unaozingatia uwajibikaji wa pamoja, ujirani mwema na kutoyategemea madola ya kigeni katika kudhamini usalama wao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *