BAADA ya beki wa Taifa Stars, Haji Mnoga kuitumikia misimu miwili Salford City inayoshiriki League Two nchini England, nyota huyo amejiunga na Patro Eisden Maasmechelen inayoshiriki Ligi daraja la pili Ubelgiji maarufu kama Challenger Pro League.

Mnoga anajiunga katika klabu hiyo akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na Salford City ambayo alitumikia timu hiyo kwa misimu miwili mfululizo.

Hatua hiyo inamfanya Mnoga kuwa miongoni mwa wachezaji wachache kutoka Tanzania kucheza soka la kulipwa nchini Ubelgiji na kuongeza kitu katika karia yake.

MNOGA Pict

Mnoga anafuata nyayo za nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, ambaye aliwahi kucheza timu mbili tofauti akiwa kwa mkopo katika klabu ya Royal Antwerp FC aliyoitumikia msimu wa 2021/22 akifunga mabao matano kwenye mechi 32 alizocheza.

Msimu uliofuata Samatta ambaye kwa sasa anakipiga Le Havre ya Ufaransa, alijiunga na K.R.C. Genk ambako alicheza mechi 33 na kufunga mabao sita.

Mbali na Samatta nyota mwingine Mbongo ambaye aliwahi kuitumikia ligi ya Ubelgiji ni Novatus Miroshi anayekipiga Goztepe ya Uturiki, msimu wa 2022/24 aliitumikia Zulte Waregem.

MNOGA Pict

Hivyo Mnoga anaongeza idadi ya wachezaji kutoka Tanzania kukipiga kwenye ligi hiyo ambayo sasa ina mashabiki kutoka Bongo baada ya nyota huyo kusaini mkataba.

Uhamisho wa Mnoga unakuja baada ya kuwa na msimu mzuri akiwa na Salford City ambapo alikuwa sehemu ya kikosi kilichofika fainali ya kupambania kupanda daraja Play-Off ya League Two, ingawa kilishindwa kufuzu kupanda League One baada ya kupoteza mbele ya Notts County katika mchezo wa Wembley.

Sasa je kile alichokionyesha Mnoga England atakuwa na muendelezo kwenye Ligi ya Ubelgiji ambayo ipo kwenye orodha ya ligi 10 bora barani Ulaya kwa sasa.

MNOGA Pict

TAKWIMU ZAKE

Akiwa Salford City, Mnoga alicheza jumla ya mechi 33 za mashindano yote na kujitengenezea nafasi ya kwanza ndani ya kikosi hicho kutokana na kiwango chake cha utulivu na uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali za ulinzi.

Kabla ya mkataba wake kumalizika, kiwango chake kilivutia klabu kadhaa za England. Miongoni mwa timu zilizowahi kuonyesha nia ya kumhitaji ni Rotherham United, ambayo ilitajwa kuweka mezani dau la pauni 250,000 kwa ajili ya usajili wake, pamoja na Lincoln City, iliyokuwa ikifuatilia maendeleo yake.

Mnoga Pict

Beki huyo aliyewahi kupita kwenye akademi ya Portsmouth na kupata nafasi katika timu za vijana za England kabla ya kuamua kuitumikia Tanzania, alionyesha kiwango kizuri kilichomfanya kuwa sehemu muhimu ya kikosi hicho.

Akicheza kwa misimu miwili Salford, msimu huu Mnoga alicheza mechi 25 za ligi kwa dakika 1697 akitoa mchango wake katika safu ya ulinzi ya Salford City iliyokuwa ikisaka kurejea League One kwa mara ya kwanza tangu kushuka daraja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *