
Maandamano makubwa ya kupinga ukiukaji wa usitishaji vita Gaza yamefanyika nchini Sweden yakilaani pia jinai za Israel dhidi ya wananchi wa Palestina.
Mamia ya watu waliandamana huko Stockholm, mji mkuu wa Uswidi, siku ya Jumamosi kupinga kuendelea kwa mashambulizi ya Israeli kwenye Ukanda wa Gaza na vikwazo vilivyowekwa kwa kuingia kwa misaada ya kibinadamu kwenye ukanda huo.
Kulingana na Shirika la Habari la Quds (Qudsna), maandamano hayo yamefanyika kwa mwaliko wa mashirika kadhaa ya kiraia katika Uwanja wa Odenplan.
Washiriki, wakiwa na mabango, walilaani mashambulizi dhidi ya Gaza, mabomu dhidi ya shule na hospitali, na mauaji ya watoto wa Kipalestina.
Aidha waandamanaji hao wametaka kusitishwa mara moja mashambulizi hayo, kukomeshwa vikwazo vya kuingia chakula, na kuheshimu utawala wa Kizayuni makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosainiwa Oktoba 10, 2025.
Wakati huo huo mji mkuu wa Ireland, Dublin, umeshuhudia kufanyika kwa wakati mmoja shughuli mbalimbali za wananchi na matukio ya michezo yaliyolenga kuunga mkono Palestina na kupinga kuanzishwa uhusiano wa kimichezo na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Washiriki wa kampeni hiyo walisisitiza kuwa, hatua hiyo ni sehemu ya shinikizo la wananchi na wanamichezo la kushinikiza kusitishwa ushiriki wa timu za Israel katika mashindano ya kimataifa. Walisema kuwa, kuendelea ushiriki wa timu hizo huku vita dhidi ya Ukanda wa Gaza vikiendelea ni aina ya kuhalalisha kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa kivamizi, jambo ambalo wanapinga.