Mabingwa watetezi, Argentina wameendeleza ubabe wao kwenye Kombe la Dunia 2026 baada ya kuichapa Jordan mabao 3–1 katika mchezo wa mwisho wa Kundi J uliochezwa alfajiri ya Juni 28, 2026, huku nahodha wa kikosi hicho, Lionel Messi akiendeleza makali yake ya kucheka na nyavu.

Licha ya Argentina kufanya mabadiliko makubwa ya kikosi yaliyofanya Messi kuanzia benchi, lakini timu hiyo ilionesha ubora mkubwa na kumaliza hatua ya makundi ikiwa na asilimia 100 ya ushindi.

Dakika ya 19, Giovani Lo Celso aliipatia Argentina uongozi kwa mpira wa adhabu uliopigwa kwa umahiri mkubwa nje ya eneo la hatari.

Argentina iliendelea kushambulia kwa kasi na kupata bao la pili dakika ya 30 baada ya VAR kuamua penalti kufuatia faulo ndani ya boksi. Lautaro Martínez alifunga akiipa timu hiyo faida ya mabao 2–0 kabla ya mapumziko.

Jordan ilirudi kipindi cha pili ikiwa na mabadiliko mawili ya mapema yaliyoongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji.

Juhudi hizo zilizaa matunda dakika ya 55 kupitia Musa Al-Taamari aliyefunga bao baada ya krosi kutoka upande wa kushoto.

Hata hivyo, matumaini ya Jordan yalidumu kwa muda mfupi baada ya Messi kuingia dakika ya 60 na kubadilisha kabisa kasi ya mchezo, akipokelewa kwa shangwe kubwa kutoka kwa mashabiki.

Dakika za mwisho za mchezo, Messi alionyesha ubora wake kwa kufunga bao la tatu kupitia mpira wa adhabu uliopigwa kwa ustadi mkubwa, ukipita ukuta wa Jordan na kutinga wavuni.

Argentina ilidhibiti mchezo hadi mwisho na kuhakikisha inamaliza hatua ya makundi ikiwa kinara wa Kundi J ikikusanya pointi tisa.

Messi ametangazwa kuwa Mchezaji bora wa mechi hiyo na kumfanya kubeba tuzo tatu mfululizo, huku pia akifikisha mabao sita akiwa kinara wa ufungaji. Messi pia amefanikiwa kufunga kila mechi hatua ya makundi.

Nahodha huyo pia ameweka rekodi ya kufunga idadi ya mabao 11 katika mechi saba mfululizo za Fainali ya Kombe la Dunia.

Wakati huohuo, Argentina baada ya kufuzu hatua ya 32 Bora, sasa itakutana na Cape Verde ambayo yenyewe imefuzu kwa kukusanya pointi tatu pekee zilizotokana na sare zote ilipokuwa kundi H.

Kwa upande wa Jordan, ingawa imeondolewa baada ya kupoteza mechi zote tatu, imeacha alama kwa kufunga bao katika kila mchezo wao, jambo linaloonyesha maendeleo yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *