Arusha. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amemwagiza mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa barabara za kuelekea uwanja utakaotumika kwa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027 kuhakikisha kazi hiyo inafanyika usiku na mchana ili ikamilike kwa wakati.

Waziri huyo amesisitiza barabara hizo zenye urefu wa kilomita 13, zinazojumuisha kipande cha Moshono hadi Mzunguko wa Mrombo pamoja na Mbauda hadi Mzunguko wa Losinyai, zinapaswa kujengwa kwa viwango vya juu vya ubora ili ziweze kudumu kwa muda mrefu na kuendana na hadhi ya mashindano ya AFCON.

Ulega ametoa maelekezo hayo leo Jumapili, Juni 28, 2026 jijini Arusha wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Arusha mjini inayojulikana kama Mbauda Junction hadi Losinyai Junction, yenye urefu wa kilomita 7.0 inayojengwa kwa kiwango cha lami.

Maelekezo hayo yanakuja wakati Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi zitakazokuwa wenyeji wa michuano ya AFCON 2027 pamoja na nchi jirani za Afrika Mashariki za Kenya na Uganda.

“Nikirudi baada ya muda nataka kuona kazi inaendana na muda na thamani ya mradi, nataka kazi hii ifanyike usiku na mchana ili kuhakikisha wakati wataalamu wa AFCON watakapokuja kukagua miundombinu ikiwemo viwanja na barabara, miradi hii iwe imekamilika kwa kiwango kinachotakiwa,” amesema Ulega.

Aidha, Waziri huyo amewataka wakazi wa Arusha kuendelea kudumisha amani na utulivu wa nchi ili waweze kunufaika na fursa zitakazotokana na mashindano hayo.

“Naombeni mtunze amani ya nchi yetu bila vurugu wala migongano ili kila mwananchi, kuanzia wafanyabiashara wadogo hadi wakubwa, aweze kufaidika na matunda ya michuano hii,” amesema.

M’bunge wa Arusha mjini Paul Makonda akizungumzia utekelezaji wa mradi wa barabara za kuelekea uwanja utakaotumika katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027 mbele ya Waziri wa ujenzi Abdallah Ulega

Amesema changamoto zinazoweza kujitokeza zinapaswa kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo badala ya vitendo vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa Taifa.

“Kama kuna mambo hayaendi sawa, nendeni mkazungumze na viongozi husika, hakuna jambo lisiloweza kuzungumzwa, ni bora kutafuta suluhisho kwa mazungumzo kuliko kutishia kuharibu nchi yetu,” amesema.

Waziri Ulega pia amewahimiza wakazi wa Arusha kuwekeza katika miradi mbalimbali ili kunufaika na fursa za kiuchumi zinazotokana na maboresho ya miundombinu inayoendelea mkoani humo.

“Jengeni migahawa, maduka na hoteli ili muwe tayari kupokea wageni watakaokuja wakati wa mashindano,  Wageni hao watakuwa mabalozi wa utalii wetu na Taifa letu kwa ujumla, na tunatarajia kupokea idadi kubwa ya watu wakati na baada ya mashindano hayo,” amesema.

Awali, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Arusha, Reginald Massawe amesema mkataba wa mradi huo ulisainiwa Februari 11, 2025 kati ya Serikali na kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) kwa gharama ya Sh221 bilioni.

Amesema utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kufanyika kwa kipindi cha miezi 36 baada ya mkandarasi kukabidhiwa eneo la kazi Aprili 10, 2026 na unatarajiwa kukamilika Aprili 20, 2029.

Hata hivyo, Massawe amesema sehemu ya kilomita 13 inayohusisha barabara muhimu kuelekea AFCON itakamilishwa mapema kabla ya ukaguzi wa miundombinu ya mashindano hayo.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, Reginald Massawe, akimwelezea Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, mchoro wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Mbauda Junction hadi Losinyai Junction jijini Arusha wakati wa ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo, Juni 28, 2026.

“Katika mradi huu, barabara yenye urefu wa kilomita 13 zitaharakishwa na tunategemea zitakamilishwa kabla ya ukaguzi wa AFCON na zitakuwa na taa za barabarani pamoja na maeneo ya maegesho,” amesema.

Amesema kuwa barabara ya Moshono itajengwa kwa njia mbili huku kipande cha katikati ya jiji hadi Mrombo kikijengwa kwa njia nne.

Kwa upande wake, Mbunge wa Arusha Mjini, Paul Makonda amesema ujenzi wa barabara za njia nne utafungua fursa nyingi za kiuchumi na kuifanya Arusha kuwa kitovu muhimu cha biashara na uwekezaji.

“Kikubwa ni kuwapa ushirikiano viongozi wetu ili waweze kutimiza malengo ya kufungua fursa za kiuchumi kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa,” amesema Makonda ambaye pia ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Amesema maboresho ya miundombinu ikiwemo barabara, masoko, kumbi za mikutano na viwanja vya michezo yanalenga kuifanya Arusha kuwa mji wenye ushindani mkubwa wa kiuchumi na kivutio cha uwekezaji nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *