
Kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ya kuliagiza Jeshi la Polisi kutotoa ruhusa ya mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa, imekosolewa na wanasheria na wadau wa siasa kwa sababu haionekani kuwa na msingi wa kisheria na kikatiba.
Hatua hii ni kwa sababu ibara ya 20(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inampa kila mwananchi haki ya kukutana kwa amani, kutoa maoni na kushiriki shughuli za kisiasa kupitia vyama halali. Hiyo si zawadi ya Serikali, bali ni haki inayolindwa na Katiba.
Utetezi wa Katiba na sheria si suala la kisiasa bali ni msingi wa uhai wa taifa lolote linalojinasibu kuwa la kidemokrasia. Haki za msingi zinazotambuliwa na Katiba haziwezi kutolewa au kuondolewa kwa matakwa ya mtu, wadhifa au mazingira ya kisiasa.
Ndiyo maana uamuzi huu wa Serikali wa kusitisha mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa kwa hoja ya kulinda usalama wa nchi, umeibua maswali mazito kuhusu heshima kwa Katiba, utawala wa sheria na mipaka ya mamlaka ya viongozi wa umma, jambo ambalo nasi tunaungana nalo.
Ni jambo la kusikitisha kuona kwamba kila kunapotokea hofu ya kiusalama, suluhisho la kwanza linaonekana kuwa ni kubana uhuru wa wananchi badala ya kuimarisha uwezo wa vyombo vya dola kukabiliana na wahalifu husika. Serikali imeeleza kuwa kuna viashiria vya vurugu, watu wenye silaha na mipango ya kuvuruga amani. Kama ni hivyo, jukumu la Waziri wa Mambo ya Ndani si kuzuia mikutano ya kisiasa, bali kuhakikisha vyombo vya ulinzi na usalama vinawakamata wahusika na kuwafikisha mbele ya sheria.
Hatupingi wajibu wa Serikali kulinda usalama wa raia na mali zao, lakini usalama hauwezi kuwa sababu ya kudhoofisha haki za kikatiba. Huo ni mwelekeo hatari unaoweza kujenga utamaduni wa kutumia hofu au masilahi binafsi ya kisiasa kama kisingizio cha kupunguza uhuru wa wananchi. Taifa linapofika mahali ambapo haki za msingi zinaweza kusimamishwa kwa tamko la kiongozi mmoja, bila uamuzi wa mahakama au masharti yanayotambuliwa na sheria, msingi wa utawala wa sheria huanza kutikisika.
Historia ya Tanzania inaonyesha kwamba marufuku za jumla dhidi ya mikutano ya kisiasa hazijawahi kuondoa tofauti za kisiasa. Badala yake, zimeongeza malalamiko, kutokuaminiana na hisia kwamba sheria zinatumika kwa upendeleo.
Serikali ya awamu ya sita ilipopokea uongozi, moja ya hatua zilizopongezwa sana ilikuwa kurejesha uhuru wa mikutano ya kisiasa mwaka 2023. Hatua hiyo ilijenga matumaini kuwa nchi ilikuwa inarejea katika misingi ya maridhiano, mazungumzo na kuheshimu haki za kiraia. Ni jambo la kushangaza kuona safari hiyo ikianza kurudi tulikotoka katika awamu ya tano.
Kauli za wanasheria mbalimbali walionukuliwa na Mwananchi jana, zimeelekeza hoja moja muhimu kwamba hakuna sheria inayompa Waziri wa Mambo ya Ndani mamlaka ya kupiga marufuku mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa kwa tamko la jumla.
Sheria ya Polisi tayari imeweka utaratibu wa kutathmini kila mkutano kulingana na mazingira yake. Ikiwa mkutano mmoja una viashiria vya hatari unaweza kuzuiwa kwa misingi ya sheria. Lakini kuadhibu vyama vyote na wananchi wote kwa hofu ya matukio yanayodhaniwa kutokea ni kwenda mbali zaidi ya kile sheria ilichokusudia.
Demokrasia hustawi pale wananchi wanapopewa nafasi ya kusikilizana, kukosoana na kushindana kwa hoja. Kufunga majukwaa ya kisiasa hakuzuii mawazo ya wananchi; kunayahamishia sehemu zisizo rasmi ambako ni vigumu zaidi kuyasimamia. Taifa linahitaji lipumue kisiasa. Linahitaji wananchi waweze kukutana kwa amani, kutoa maoni yao na kuhoji viongozi bila kuonekana ni tishio kwa usalama wa nchi.
Tunamkumbusha Waziri wa Mambo ya Ndani kuwa dhamana aliyopewa ni kusimamia usalama wa nchi kwa mujibu wa Katiba na sheria, si kuamua ni lini wananchi watumie haki zao za kikatiba. Vilevile, vyombo vya dola vinapaswa kutekeleza wajibu wake kwa weledi, bila kuingizwa katika maamuzi yanayoweza kutafsiriwa kama ya kisiasa.