ILIPOISHIA

Wakwetu alipanda ghorofani kilikokuwa chumba cha Masumbuko. Akabisha mlango. Masumbuko akafungua mlango.

“Tumeshafika” James alimwambia Masumbuko.

“Mzee yuko wapi?”

“Yuko mkahawani, amenituma nikufuate”

“Haya twende”

Masumbuko akafunga mlango wakashuka ngazi na kuingia mgahawani.

SASA ENDELEA…

Waliketi kwenye meza aliyokuwa ameketi Wakwetu.

“Habari za tangu muda ule?” Masumbuko akamsalimia Wakwetu.

“Nzuri. Mngependa kula nini usiku huu?” Wakwetu aliwauliza.

Masumbuko na James wakatazamana. Mhudumu alikuwa ameshafika. Kila mmoja alimuagiza chakula alichokipenda. Wakwetu naye aliagiza chakula chake.

Chakula kilipoletwa walinawa mikono na kuanza kula. Wakwetu alikula chipsi na kuku. Masumbuko alikula ndizi kwa nyama na James alikula wali na kuku. Kila mmoja alikuwa na bilauri yake ya juisi.

“Vijana wangu, siku kama ya leo hamkuitarajia,” Wakwetu akawaambia Masumbuko na James wakati wakiendelea kula.

“Kweli, mimi sikutarajia kabisa kuwa kuna siku ningekutana tena na ndugu yangu,” James alisema.

“Mimi nilikuwa na matarajio, ingawa yalikuwa yakififia siku hadi siku,” Masumbuko naye alisema.

“Kuna kitu kimoja nataka kuwaambia, nadhani hamkifahamu.”

Vijana hao wawili ambao kisura walikuwa wameshabihiana walimtazama Wakwetu kwa shauku, wakisubiri kusikiliza hicho kitu ambacho Wakwetu alitaka kuwaambia.

“Binadamu hatakiwi kukata tamaa wakati wote. Masumbuko, umesema ulikuwa na matarajio lakini yakawa yanafifia siku hadi siku. Ulikosea. Ulitakiwa uendelee kuwa na matarajio yako ukimtegemea Mungu na ukiamini iko siku utakutana na ndugu yako kama ambavyo mmekutana,” Wakwetu aliwaambia.

“Ni kweli. Umetupa somo zuri. Binadamu hatakiwi kukata tamaa,” James akasema.

“Kwa kweli nilikosea. Leo ninaamini kuwa nilikosea. Namshukuru Mungu nimekutana na ndugu yangu niliyepotezana naye kwa miaka mingi.”

Wakati akisema hivyo, Masumbuko alikuwa akimtazama James, wakacheka.

Wakwetu naye akacheka.

“Ninaamini kuwa leo mna furaha kubwa sana, ndiyo maana nimewakutanisha pamoja katika chakula hiki cha usiku, mle pamoja, mzungumze na kufurahi huku mkiamini kuwa na mimi nina sehemu katika furaha yenu.”

Ile sentensi ya Wakwetu, “Na mimi nina sehemu katika furaha yenu,” hawakuielewa. Walijua kuwa mzee huyo alikuwa akifurahia kukutana kwao, lakini Wakwetu alikuwa na maana nyingine zaidi ambayo hakutaka kuwaambia.

“Kwa hiyo mnaamini kuwa wazazi wenu walifariki dunia?” Wakwetu aliwauliza.

James akabetua mabega.

“Hatuna uhakika. Maelezo tuliyopewa ni kuwa tulipelekwa katika kile kituo na mama mmoja wa Kiarabu, akaeleza kuwa alituchukua kutoka kwa bibi mmoja aliyekuwa akitulea ambaye baadaye alifariki dunia. Sasa habari za nyuma ya hapo kwamba wazazi wetu walikuwa wapi hazijulikani,” akasema.

“Lakini mna tamaa kwamba mnaweza kuwapata wazazi wenu?” Wakwetu aliwauliza huku akiwatazama kwa zamu.

“Kama ambavyo sisi wenyewe tumekutana, nadhani hata wazazi wetu tunaweza kuwagundua japokuwa baadaye sana,” James alisema.

Wakwetu akamtazama Masumbuko.

“Masumbuko, kwa upande wako unadhani mnaweza kuja kuwapata wazazi wenu?”

Masumbuko akatikisa kichwa.

“Sidhani, kwa sababu hata kumbukumbu zao hazipo. Tutawajuaje au wao watatujuaje? Ni sawa tukiamini kuwa wamekufa.”

“Masumbuko, umerudia tatizo lako la kukata tamaa mapema. Sasa hivi niliwapa somo kwamba binadamu hatakiwi kukata tamaa kama yuko hai.”

James na Masumbuko wakanyamaza kimya.

Wakwetu aliendelea kuwaeleza.

“Mnatakiwa muendelee kuwa na tamaa ya kuwapata wazazi wenu. Kama si wote wawili, mnaweza kumpata mzazi mmoja kwa sababu haikuthibitishwa kama wote walikufa au wako hai.”

“Basi nitakuwa na tamaa, lakini najiuliza tutakuja kuwagundua vipi au wao watatugundua vipi wakati walituacha watoto na sasa tumeshakuwa wakubwa?” Masumbuko akasema.

Wakwetu akamtazama James.

“James, unaweza kumjibu?”

James akatabasamu na kumtazama Masumbuko.

“Kwani sisi tumekutanaje wakati tuliachana tukiwa watoto na tumekutana tena tukiwa wakubwa, tena katika mazingira tusiyoyatarajia kukutana?” James akamuuliza Masumbuko.

“Naona kama imetokea bahati,” Masumbuko alijibu akionyesha kutokuwa na uhakika na jibu lake, halafu wote wakacheka.

“Basi tutegemee hiyo hiyo bahati,” James akasema baada ya kicheko.

“Mimi naamini kuwa mnaweza kumpata mmoja wa wazazi wenu muda si mrefu,” Wakwetu akawaambia.

“Tutafurahi sana,” James akasema.

“Masumbuko, ukija kumpata mmoja wa wazazi wako utakuwa na furaha ya kiasi gani?” Wakwetu akamuuliza Masumbuko.

“Furaha yangu siwezi kuielezea kwa leo.”

“Bila shaka itakuwa ni furaha kubwa sana.”

“Sana!”

Walipomaliza kula waliendelea kuzungumza hadi saa nne usiku.

“Sasa Masumbuko, nenda ukalale, sisi tunaondoka. Nitakupitia tena kesho asubuhi,” Wakwetu akamwambia Masumbuko.

“Nashukuru sana. Usiku mwema.”

James akaagana na Masumbuko kabla ya kuondoka na Wakwetu.

Safari hii Wakwetu alimuacha James aendeshe.

“Tuelekee wapi?”

“Twende nikakuache nyumbani kwako,” Wakwetu alimjibu James.

James akaendesha gari hilo hadi nyumbani anakoishi. Alisimamisha gari, akafungua mlango.

“Tuonane kesho,” akamwambia Wakwetu kabla ya kushuka.

“Sawa,” Wakwetu akamjibu huku akijisogeza kwenye usukani. Alitia gia na kuliondoa gari.

Alipofika nyumbani kwake aliliegesha gari, akaingia ndani. Alimkuta mke wake akitazama televisheni.

“Yuko wapi Majaliwa?” akamuuliza.

“Majaliwa ameshalala,” Sharifa alimjibu.

Wakwetu hakumwambia kitu kingine, aliingia chumbani mwake. Alivua nguo alizokuwa amevaa, akavaa teitei, vazi jepesi la nyumbani. Sharifa akaingia mle chumbani.

“Nimeshakuwekea chakula,” akamwambia.

“Hapana. Nimeshakula.”

Sharifa alishituka.

“Umekula wapi?”

“Nimekula hotelini, nilikuwa na wageni, nilikula nao.”

“Wageni hao walitoka wapi?”

“Ni wageni wangu wa kibiashara,” Wakwetu alimjibu Sharifa.

“Ndio uliokuwa nao tangu ulipoondoka?”

“Ndio.”

“Nilipoona unachelewa nilianza kupata wasiwasi kwa sababu si kawaida yako kuchelewa hivi.”

Wakwetu hakujibu kitu.

Usiku huo ulikuwa wa mawazo kwa wote wawili. Sharifa alikuwa akiwaza juu ya mabadiliko ya ghafla ya mume wake. Alikuwa na hakika kuwa mume wake alikuwa na kitu ndani ya moyo wake, kitu ambacho Sharifa alishindwa kukielewa. Mara kwa mara alikuwa akijiuliza Wakwetu amegundua kitu gani, lakini hakupata jibu.

Kwa upande wake Wakwetu alikuwa akiwaza juu ya Masumbuko na James pamoja na mwanawe Majaliwa. Palikuwa na fumbo lililokuwa likimpa fadhaa ambalo alijiambia kuwa kesho yake atalifumbua na kupata uhakika wa vijana hao.

Asubuhi kulipokucha Wakwetu alimchukua Majaliwa. Alimwambia kuna sehemu alitaka waende. Kwa vile James alikuwa ameshafika, aliwapakia pamoja kwenye gari, akaondoka nao.

Alikwenda nao kwenye ile hoteli aliyompangia chumba Masumbuko, akamuacha James hapo. Akaendelea na safari akiwa na Majaliwa hadi katika hospitali moja iliyokuwa ikichukua vipimo vya DNA kutoka kwenye damu.

Alishuka na Majaliwa na kuingia kwenye hospitali hiyo. Alimuacha Majaliwa nje ya chumba cha daktari, akaingia peke yake na kumuona daktari aliyekuwa akihusika na upimaji wa vipimo vya DNA.

Alimweleza tatizo lake la kutaka kufanyiwa kipimo hicho yeye na mwanawe Majaliwa ili kujua kama Majaliwa alikuwa mwanawe kweli.

Kipimo hicho huchunguza chembechembe za urithi kwenye damu na kutoa jibu hapo hapo.

Baada ya daktari kumsikiliza, Wakwetu alianza utaratibu huo. Daktari aliwachukua Wakwetu na Majaliwa kwenye chumba chake cha maabara na kuchukua damu ya Majaliwa. Majaliwa baada ya kutolewa damu, Wakwetu alimpa pesa ya nauli akamwambia arudi nyumbani.

Majaliwa akiwa ameshangazwa na kitendo hicho alitoka na kwenda kupanda daladala. Hakujua ni kwa nini Wakwetu alitaka achukuliwe damu wakati hajamwambia kuwa anaumwa.

Baada ya Majaliwa kuondoka, Wakwetu naye alichukuliwa damu. Damu ya Wakwetu na damu ya Majaliwa ilikwenda kufanyiwa vipimo. Wakwetu aliambiwa asubiri katika sehemu ya kusubiri majibu.

Baada ya kusubiri kwa karibu saa nzima, Wakwetu aliletewa bahasha iliyokuwa na majibu. Aliifungua pale pale na kuisoma. Majibu yalionyesha kuwa damu yake na damu ya Majaliwa zilikuwa zimekataana, jambo lililoonesha kuwa Majaliwa hakuwa mtoto wa Wakwetu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *