
Dar es Salaam. Tanzania imeanza kunufaika na ushirikiano mpya na wataalamu wa ubunifu kutoka Finland, unaolenga kuimarisha uwezo wa wabunifu na wajasiriamali wa teknolojia nchini, hatua inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali na kuongeza ushindani wa Taifa katika soko la kimataifa.
Mpango huo unawakutanisha washiriki 50 kutoka Tanzania katika mafunzo maalumu ya siku tano yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, yakilenga kuwajengea uwezo katika masuala ya ubunifu, ujasiriamali na namna ya kubadilisha mawazo ya kiteknolojia kuwa bidhaa na huduma zenye thamani ya kibiashara.
Mafunzo hayo yaliendeshwa na wataalamu kutoka Finland kwa uratibu wa Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Tanzania (ICTC), wakati Serikali ikiendelea kuweka mkazo katika matumizi ya teknolojia kama suluhisho la changamoto mbalimbali ikiwamo ukosefu wa ajira kwa vijana.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo Juni 22, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa ICTC, Dk Nkundwe Mwasaga, alisema dhamira ya Tanzania si kuzalisha watumiaji wa teknolojia pekee, bali wabunifu wenye uwezo wa kuunda suluhisho zinazoweza kushindana katika soko la dunia.
“Tunataka kuona ubunifu huu ukizalisha ajira kwa vijana wetu, ukiimarisha sekta mbalimbali za uchumi na kuongeza ushindani wa Tanzania kimataifa,” alisema.
Alieleza kuwa ubunifu ni moja ya nguzo muhimu katika safari ya mageuzi ya kidijitali nchini na una mchango mkubwa katika kufungua fursa ndani ya uchumi wa kidijitali.
“Tanzania ina idadi kubwa ya vijana wenye nguvu na ari ya kufanya kazi. Tunataka wawe wabunifu wa teknolojia, si watumiaji pekee. Ujuzi huu utawasaidia kuelewa namna ubunifu unavyoweza kuongeza thamani na kuchangia maendeleo ya uchumi,” alisema.
Kukuza malengo ya kidijitali
Mafunzo hayo yanatekelezwa chini ya mpango wa Digital4Tanzania (D4T), ushirikiano wa serikali kwa serikali unaoungwa mkono na Ujerumani, Finland na Estonia. Mpango huo unalenga kuimarisha mfumo wa kidijitali nchini kupitia uwekezaji katika maendeleo ya ujuzi, usalama wa mtandao, tafiti na ubunifu.
Katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, Tanzania imewekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu ya kidijitali ikiwamo upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, kuboresha huduma za simu na kuhamisha huduma mbalimbali za Serikali kwenye mifumo ya kidijitali.
Hata hivyo, wataalamu wanaeleza kuwa uwekezaji katika miundombinu pekee hautoshi bila kuwepo kwa ubunifu wa ndani unaoweza kutatua changamoto halisi za jamii.
Kwa mujibu wa Dk Mwasaga, mafunzo hayo yanaendana na nguzo tano za kimkakati zinazounda mustakabali wa kidijitali wa Tanzania ambazo ni usalama wa mtandao, maendeleo ya ujuzi wa kidijitali, miundombinu ya kisasa ya mawasiliano, uchumi wa kidijitali pamoja na tafiti na ubunifu.
Mojawapo ya maeneo yaliyojadiliwa ni ununuzi wa ubunifu (innovation procurement), mfumo unaotumika kwa mafanikio katika nchi zilizoendelea lakini bado ni mpya nchini Tanzania.
Mfumo huo unazipa taasisi za umma nafasi ya kununua suluhisho za ubunifu kutoka kwa kampuni changa na wabunifu vijana, hivyo kuunda soko la teknolojia zinazozalishwa nchini.
“Washiriki wakielewa mafanikio yaliyofikiwa Finland na mchango wa ubunifu katika ukuaji wa uchumi, watakuwa katika nafasi nzuri ya kuiga mifano hiyo hapa Tanzania,” alisema.
Aliongeza kuwa juhudi zinaendelea kuimarisha vituo vya ubunifu na programu za kulea biashara changa ili mawazo yenye uwezo kutoka kwa vijana wa Kitanzania, yaweze kukua na kuwa biashara kubwa zinazoweza kushindana ndani na nje ya Afrika Mashariki.
Somo kutoka Finland
Finland ni miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani katika elimu, ubunifu na maendeleo ya teknolojia. Taifa hilo linatambulika kwa mfumo wake imara wa kampuni changa za teknolojia na ushirikiano madhubuti kati ya Serikali, vyuo vikuu na sekta binafsi.
Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo, mtaalamu wa ubunifu kutoka Finland, Tiina Koivuniemi, aliwahimiza wabunifu wa Tanzania kuwa na ujasiri wa kujaribu mawazo mapya na kuamini uwezo wao.
“Faida kubwa ya programu hii ni kuwapa washiriki zana za vitendo za kusimamia ubunifu, kubadilishana uzoefu na kujenga mitandao ya kitaalamu itakayowezesha ushirikiano wa baadaye,” alisema.
Aliwataka vijana kutazama changamoto za jamii kwa mitazamo tofauti na kutokuwa na hofu ya kujaribu njia mpya.
“Mara nyingi ubunifu huanza pale watu wanapothubutu kuhoji njia zilizopo na kujaribu mawazo mapya. Tunataka wabunifu wa Tanzania wawe na ujasiri wa kufanya majaribio na kujifunza kupitia uzoefu huo,” alisema.
Fursa kwa kampuni changa
Washiriki wa mafunzo hayo walieleza kuwa mpango huo umekuja wakati mwafaka, hasa katika kipindi ambacho mazingira ya kampuni changa za teknolojia nchini yanaendelea kukua, licha ya changamoto za upatikanaji wa mitaji, ushauri wa kitaalamu na masoko.
Mwanzilishi wa ReinoLab, maabara ya kidijitali ya sayansi inayotumia akili unde (AI), Peace Bisake, alisema mafunzo hayo yatawapa wabunifu wa ndani fursa ya kujifunza viwango vya kimataifa na kuongeza uwezo wao wa kushindana katika soko la dunia.
“Uchumi wa kidijitali hauna mipaka. Kama tunataka ubunifu wa Tanzania utambulike kimataifa, tunahitaji kufahamu viwango vya dunia na mbinu bora za ubunifu,” alisema.
Kwa upande wake, mwanzilishi wa kampuni ya Paki Urban Limited, Rodrick Mshanga, alisema wabunifu wengi wana mawazo mazuri lakini hukosa ujuzi wa kuyageuza kuwa biashara zenye faida.
“Vijana wengi wanajua kutengeneza suluhisho, lakini wanakabiliwa na changamoto za kukuza biashara, kuvutia wawekezaji na kuweka bidhaa zao katika nafasi ya ushindani. Programu kama hizi zinasaidia kuziba pengo hilo,” alisema.