
Matumaini ya kukijenga upya Chama cha Wananchi (CUF) ili kirejee katika kasi na ubora wake wa awali, yanaendelea kufifia kutokana na kuandamwa na migogoro ya wanachama, huku viongozi wakishindwa kuifikia suluhu ya kudumu.
Chama hicho cha siasa ambacho hapo awali kilionekana kuwa jukwaa la kuaminika kwa wananchi na wadau wa siasa nchini, kwa sasa kinaendelea kugubikwa na sintofahamu, licha ya kupita miezi minne tu tangu kifanye uchaguzi uliompatia Yusuf Mirambo nafasi ya Mwenyekiti mpya.
Wiki iliyopita, viongozi 16 walitangaza kujiuzulu nafasi zao, ikiwa ni mwendelezo wa makundi, tangu Mirambo alipochaguliwa kukiongoza chama hicho Februari 22, 2026 baada ya aliyekuwa mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba kuvuliwa uongozi na wanachama.
Viongozi hao waliojiuzulu wanadai kutoridhishwa na mfumo wa uongozi uliopo madarakani wakidai kuna changamoto za kiuongozi, uamuzi wa juu pamoja na ukosefu wa ushirikishwaji wa kutosha katika masuala muhimu ya chama.
Hatua hiyo inamwekea Mwenyekiti Mirambo na chama hicho katika mtihani mkubwa ikizingatiwa kuwa imejitokeza miezi minne baada ya uchaguzi mkuu wa dharura uliofanyika Februari 22, 2026, uliomwingiza madarakani yeye pamoja na viongozi wengine.
Hata hivyo, uchaguzi huo uliomweka madarakani mwenyekiti huyo umekuwa ukipingwa na baadhi ya wanachama waliowasilisha malalamiko kwa Msajili wa Vyama vya Siasa wakidai ulikiuka taratibu za Katiba ya chama na hivyo unapaswa kubatilishwa.
Ingawa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amethibitisha kupokea malalamiko hayo kutoka kwa makada wa chama hicho, Othman Dunga na Romanus Mapunda, bado hajatoa uamuzi rasmi kuhusu suala hilo, jambo ambalo linazidi kukoleza moto.
Wakati wanachama wakisubiri uamuzi huo wa Msajili wa Vyama vya Siasa, makada 73 nao waliandamana wakitaka kupatiwa mrejesho wa malalamiko yao.
Hali hiyo inaashiria kuendelea kwa kutokuaminiana ndani ya uongozi wa sasa na kuzidisha dalili za migogoro ya ndani.
Migogoro hiyo ni mwendelezo wa changamoto ambazo zimeendelea kukikumba CUF kwa miaka mingi na kuibua maswali kuhusu mustakabali wa chama hicho tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992.
Miongoni mwa waliojiuzulu ni Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano kwa Umma, Mohamed Ngulangwa aliyehudumu kwa muda mrefu katika uongozi chini Profesa Lipumba pamoja na viongozi wengine 15 kutoka Zanzibar waliotangaza kuachia nyadhifa zao.
Ngulangwa afafanua
Akizungumzia uamuzi wake, Ngulangwa anasema aliamua kujiuzulu baada ya mwenyekiti wa chama kusitisha mkutano na waandishi wa habari aliokuwa ameuitisha kulaani kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi, iliyozuia vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara.
Anasema mkutano huo ulitekeleza maazimio ya Kamati ya Mashauriano ya Tanzania Bara iliyoongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Bara, Vedasto Ngombale Mwiru.
Kwa mujibu wa Ngulangwa, baada ya mwaliko kutumwa kwa vyombo vya habari na wanachama, Mirambo aliamuru mkutano huo usifanyike kwa maelezo kuwa ungeonekana kana kwamba Mwenyekiti hana mamlaka ndani ya chama.
“Ili kuitendea haki dhamira yangu, nimeamua kujiuzulu nafasi ya Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano kwa Umma ili nipate uhuru wa kusimamia ninachokiamini.
Hata hivyo, nitaendelea kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kupitia Kanda ya Pwani,” anasema.
Ngulangwa anaongeza kuwa CUF, badala ya kusonga mbele, linaendelea kudhoofika, jambo lililomfanya aamue kujiondoa kwenye nafasi yake ya uongozi ili kutoa nafasi ya kutafakari na kujikita katika shughuli nyingine.
Anasema migogoro ni jambo la kawaida katika taasisi yoyote, lakini mafanikio hutegemea namna inavyosimamiwa na kutatuliwa ili isiathiri maendeleo ya taasisi.
“Taasisi yoyote iliyokomaa haiwezi kukosa migogoro. Changamoto ni jinsi ya kuisimamia ili isitulete kwenye sintofahamu,” anasema.
Wachambuzi waonya
Mchambuzi wa siasa kutoka Zanzibar, Ali Maulid Juma anasema kuondoka kwa viongozi 16 kwa wakati mmoja ni pigo kubwa litakalodhoofisha utendaji wa chama.
Anasema hali hiyo inaashiria kipindi kigumu kwa CUF na inaweza kukiweka katika mazingira ya kupoteza ushawishi wake wa kisiasa iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.
“Chama kinadidimia na endapo hakitafanya mikakati ya mapema kinaweza kupotea kwa haraka zaidi katika ramani ya siasa na kubaki jina tu,” anasema.
Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa George Kahangwa anasema safari ya vyama vya siasa huhitaji uimara wa kiitikadi na rasilimali za kifedha. Bila hivyo, vyama vingi hukumbwa na migogoro na kudhoofika.
Anasema tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, baadhi ya vyama vya upinzani vilianza kwa nguvu lakini baadaye vikadhoofishwa na migogoro ya ndani.
Profesa Kahangwa anasema mazingira ya siasa za upinzani nchini ni magumu na wakati mwingine huathiriwa na ushawishi wa fedha kutoka nje ingawa viongozi wanapaswa kujitathmini ili kubaini chanzo halisi cha migogoro inayoendelea.
Anasema siasa za Tanzania upinzani una mazingira tofauti, ukiimarika penyeza rupia na ukiona migogoro inazidi kutawala ni wazi fedha iliyopenyezwa inazidi kufanya kazi yake kama ilivyokuwa kwa NCCR–Mageuzi hadi kikaja kugawika na wengine kuanzisha chama cha Tanzania Labour Paty (TLP), kilichobebwa na mtu mmoja lakini hakionekani katika ramani.
Mirambo atoa msimamo
Mwenyekiti wa chama hicho, Mirambo, anasema anapokea uamuzi wa viongozi waliojiuzulu kwa pamoja kama mtihani anaopaswa kuushinda ili kuendelea kukiimarisha chama.
“Wale ni wanachama ambao tumekuwa nao kwa muda mrefu na wamehudumu katika ngazi mbalimbali za uongozi. Tulipoingia kwenye uchaguzi mkuu wa dharura, baadhi yao walionyesha kutoridhishwa kutokana na sababu walizozieleza wazi,” anasema Mirambo.
Anasema sababu ya kwanza waliyoitoa ni kutokukubaliana na kuondoka madarakani kwa aliyekuwa mwenyekiti wa chama, Profesa Lipumba kwa kuwa walikuwa na imani na mapenzi naye.
Sababu nyingine ni kwamba walidai mchakato wa uchaguzi ulienda kwa haraka ilhali walitaka ufanyike kwa utaratibu zaidi. Sababu ya tatu ni kwamba walitaka mgombea wao wa nafasi ya uenyekiti ashinde, lakini kwa bahati mbaya hakupata kura za kutosha.
Kwa mujibu wa Mirambo, baada ya kushindwa kufikia malengo yao, viongozi hao walijitenga na shughuli za chama tangu Februari baada ya uchaguzi, hali iliyoashiria kutoridhika kwao kwa muda mrefu kabla ya kujiuzulu.
“Niliona walikuwa hawana hamasa kama awali. Tulijaribu kuzungumza nao, lakini walikuwa wamebeba mambo mengi moyoni. Hatimaye wamefikia hatua ya kufanya uamuzi huo. Sioni kama ni tatizo kubwa, bali tunafikiria namna ya kuzungumza nao ili tuendelee kujenga chama,” anasema.
Mirambo anasema viongozi hao walimweleza kuwa hawakuwa wakipata ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yao ndani ya chama, jambo lililosababisha mvutano kati yao na baadhi ya viongozi waliopo madarakani.
“Nasema wazi kwamba walishindwa kuelewa kuwa kiongozi mkuu wa chama ni mwenyekiti. Mimi binafsi sina tatizo na mwanachama yeyote. Walipaswa kuwa wavumilivu na kunipa nafasi ya kuonyesha namna ninavyotekeleza majukumu yangu pamoja nao,” anasema.
Mirambo anasema kwa kuwa chama ni taasisi, uongozi unaandaa mkakati wa kuzungumza na viongozi hao ili kubaini chanzo halisi cha uamuzi wao na kuona namna ya kurejesha mshikamano.
“Taasisi kubwa kama hii hukumbwa na changamoto za aina hii mara kwa mara. Kilicho muhimu ni kuweka mkakati wa kushawishi kizazi kipya kujiunga na chama, huku tukiwalinda wanachama tulionao ili chama kiendelee kustawi na kufikia malengo yake ya kushika dola,” anasema.
Mirambo anasema migogoro inayodaiwa kuendelea ndani ya chama haiathiri utendaji wake, akieleza kuwa waliojiondoa Zanzibar hawakuondoka kutokana na mgogoro, bali kutokana na sintofahamu.
“Sababu wanazozitoa ni kwamba wanashindwa kufanya kazi na baadhi ya viongozi, wanahisi hawajathaminiwa wala kupewa nafasi. Mimi siiti hali hiyo mgogoro, bali ni tofauti za mtazamo. Mgogoro ni pale ambapo kunakuwa na mvutano wa wazi kati ya pande mbili,” anasema.
Anasema hata kundi lililowasilisha malalamiko kwa Msajili wa Vyama vya Siasa halina mgogoro na chama, kwa kuwa uchaguzi ulifanyika kwa mujibu wa taratibu, isipokuwa wao hawakuridhishwa na matokeo.
“CUF ya sasa haina migogoro. Kinachokuwapo ni wanachama ambao wameamua kushindana na mazingira badala ya kushindana kwa hoja. Hatuna makundi yanayopingana, hivyo siwezi kusema kuna mgogoro. Hata hivyo, ninaendelea kufanya jitihada za kuzungumza nao ili kurejesha umoja,” anasema.
Mirambo anaeleza kuwa lengo ni kuwashawishi wanaotaka kukitumikia chama waendelee kufanya hivyo huku akisisitiza kuwa chama ni taasisi, si mali ya mtu mmoja.
“Tunahitaji kuzungumza nao. Wale wanaotaka kulitumikia chama waendelee, lakini wanaotaka kumtumikia mtu mmoja wanapaswa kuelewa kuwa chama ni taasisi inayopaswa kuheshimika kwa kufuata taratibu zake,” anasema.
Mirambo anasema anaamini changamoto anazokutana nazo zitapita kwa sababu msingi wa kujenga chama ni kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali.
Anatolea mfano Chama cha Mapinduzi (CCM), kilichowahi kupoteza wanachama wengi akiwamo Edward Lowassa alipojiunga na Chadema, lakini baadaye chama hicho kilifanikiwa kurejesha umoja wake.
“CCM ilifanya mazungumzo na Lowassa, ambaye baadaye alirejea nyumbani. Hata baadhi ya viongozi waliokuwa wameondoka pamoja naye walirudi na kuendelea na shughuli za chama,” anasema.
Mirambo anasema CUF, pia, imewahi kupitia migogoro mikubwa, ikiwamo ule wa mwaka 2016 uliomalizika mwaka 2019 uliowahusisha Profesa Lipumba na Maalim Seif.
“Mgogoro huo ulifanya wengi waamini kuwa CUF Zanzibar imekwisha. Hata hivyo, tuliweza kupata wabunge wawili kutoka Pemba, ambako ndiko alikotokea Maalim Seif. Hii inaonyesha kuwa taasisi ikijengwa vizuri si rahisi kufa,” anasema.
Mirambo anawataka wanachama wa chama hicho kuheshimu Katiba ya chama, akisema ndiyo mwongozo sahihi wa kuendesha shughuli zake badala ya kufuata hisia au matakwa ya watu binafsi.
“Lengo letu ni kujenga chama kitakachoweza kushika dola. Hatuwezi kufikia lengo hilo ikiwa tutakuwa tunashindwa kukubaliana au kuheshimiana. Tukishindwa kufanya hivyo, ni bora kuacha siasa,” anasema.
Pia, anasema chama hakina fedha za kuwagawa wanachama wala hakijawahi kupokea fedha kutoka kwa watu au taasisi kwa ajili ya kufanya hivyo.
“Kinachotokea ni kwamba baadhi ya vyama huwavutia wanachama wanaoonekana kuyumba kwa kuwapa fedha ili wahamie upande wao. Hali hiyo imekuwa ikitumika kama njia ya kurubuni wanachama,” anasema.