
Kiongozi ni kioo cha jamii yake. Jamii yoyote inategemea kuongozwa kwa busara na mifano chanya kutoka kwa viongozi wake. Jamii hiyo inachagua viongozi kutokana na sifa zinazoendana na tamaduni zao. Ndio maana wakawaita viongozi, yaani wabeba maono, sera na mikakati ya jamii.
Vinginevyo wangekaliwa kimabavu na watawala ambao hufanya mambo kwa ajili yao na wanaowahusu tu. Kiongozi wa jamii huitangulia jamii yake kwenye kila jambo. Ndiyo maana niseme ukweli, Mama ulipotangaza kupunguza ukubwa wa misafara yako ili kubana matumizi ya mafuta ulimgusa kila Mtanzania.
Tunaamini kuwa mzigo unaobebwa na wengi hupungua uzito, yaani machungu ya wote hayana maumivu makali kama ulivyo msiba wa peke yako. Lakini pia umeibua mjadala mpana huku uswahilini, kuhusu namna bora ya kukabiliana na uhaba wa nishati hiyo nchini.
Kwa kawaida ombi la mkuu ni amri kwa wadogo. Uamuzi wako unaonekana kuwa wa mfano unaolenga kuhamasisha uwajibikaji si tu kwa viongozi wa juu tu, bali pia kwa taasisi za serikali na wananchi kwa ujumla.
Katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa mafuta, bei kupanda, na hali ngumu ya maisha, hatua kama hizi zina umuhimu mkubwa sana.
Katika mijadala mbalimbali ya wananchi kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na majukwaa ya kisera, hoja moja imekuwa ikijitokeza mara kwa mara; kama wananchi wanaombwa kujisitiri katika matumizi ya mafuta na kubeba mzigo wa kupanda kwa gharama za maisha, basi viongozi nao wanapaswa kuonesha mfano kwa kupunguza matumizi ya anasa yanayobebwa na kodi za wananchi.
Moja ya maeneo yanayotajwa mara nyingi ni ununuzi wa magari ya kifahari kwa mawaziri, wabunge na viongozi wengine wa umma. Ingawa viongozi wanahitaji usafiri salama na wa kuaminika ili kutekeleza majukumu yao, si lazima kila kiongozi atumie gari la gharama kubwa lenye matumizi makubwa ya mafuta na gharama kubwa za matengenezo.
Katika mazingira ambayo Serikali inasisitiza nidhamu ya matumizi, unyenyekevu katika matumizi ya magari unaweza kuwa sehemu ya suluhisho. Wajenga hoja wamekuwa wakichambua tofauti ya magari ya kifahari na yasiyo ya kifahari.
Wengi wameeleza kuwa gharama za kuhudumia VX la Waziri, zinaweza kutosha kununua IST mpya kabisa. Wachumi wengi wamekuwa wakisisitiza kuwa matumizi ya kawaida ya Serikali yanapopunguzwa, fedha zinazookolewa zinaweza kuelekezwa kwenye uwekezaji wenye tija zaidi. Kipaumbele kinaweza kuwa katika kujenga barabara au kuongeza upatikanaji wa dawa na pembejeo za kilimo.
Vilevile, taasisi mbalimbali zinazofuatilia uwajibikaji wa fedha za umma zimeendelea kuhimiza matumizi yenye ufanisi na thamani halisi ya fedha. Hoja yao kubwa ni kwamba kila shilingi ya kodi inapaswa kutoa manufaa makubwa kwa wananchi.
Hivyo, kabla ya kufanya matumizi makubwa ya magari mapya au ya kifahari, ni muhimu kujiuliza kama fedha hizo zingeweza kutatua changamoto kubwa zaidi zinazowakabili Watanzania.
Wananchi wengi wanaounga mkono hatua za kubana matumizi wanaamini kuwa mfano wa viongozi una nguvu kubwa kuliko kauli.
Wanapoona viongozi wakipunguza misafara, kutumia magari yenye matumizi madogo ya mafuta au kuchelewesha ununuzi wa magari mapya yasiyo ya lazima, hujenga imani kuwa juhudi za kubana matumizi zinagusa kila mtu bila ubaguzi.
Aidha, hatua hiyo inaweza kuwa na manufaa mengine ya kiuchumi. Kupungua kwa matumizi ya mafuta katika taasisi za Serikali kunasaidia kupunguza gharama za uendeshaji, kupunguza matumizi ya fedha za kigeni kwa uagizaji wa mafuta na kuchangia juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia upunguzaji wa uzalishaji wa hewa chafu. Historia inaonyesha kuwa katika nyakati za changamoto za kiuchumi, mataifa mengi yamefanikiwa zaidi pale viongozi walipoamua kuanza na wao wenyewe.
Ni wakati pia wa kuangalia upya sera za matumizi ya magari serikalini. Badala ya kubadilisha magari kila baada ya kipindi kifupi, yanaweza kutumika kwa muda mrefu zaidi ikiwa yako katika hali nzuri.
Aidha, inaweza kuwekewa mwongozo unaozingatia gharama, matumizi ya mafuta na mahitaji halisi ya kazi badala ya hadhi ya cheo. Nchi ijikune pale mikono yake inapoweza kufika.
Hatua kama hizi haziwezi kutatua changamoto zote za uchumi kwa wakati mmoja, lakini zina ujumbe mkubwa. Chembe na chembe mkate huwa, zinathibitisha kuwa uongozi ni pamoja na kujinyima pale hali inapohitaji. Zinawaonyesha wananchi kuwa Serikali ipo tayari kushiriki mzigo wa changamoto za kiuchumi badala ya kuupeleka kwa wananchi pekee. Huo ndio msingi wa uongozi unaoweka mbele maslahi ya taifa kuliko hadhi ya viongozi, na huo ndio mfano ambao Watanzania wengi wanaonekana kuutamani.
Mwisho, uamuzi wa Rais kupunguza ukubwa wa msafara wake unaweza kuwa mwanzo wa utamaduni mpya wa uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma.
Endapo utapanuliwa na kujumuisha mapitio ya matumizi ya magari ya kifahari, safari zisizo za lazima na misafara mikubwa ya viongozi, inaweza kuokoa mabilioni ya shilingi kila mwaka. Fedha hizo zinaweza kuelekezwa kwenye miradi.