Kabla ya kutongoa, nakusihi. Jikumbushe kisa cha ‘sizitaki mbichi hizi. na rumba la Madilu System’ Hii, ni kwa wale waliosoma enzi za Mchonga kabla ya UPE na uholela baada ya hapo. Sungura zwazwa, japo aliyejihisi mjanja.

Bila kuzingatia ufupi wake na uwezo wake mdogo wa kuruka, alitaka kula ndizi. Akiwa kwenye mishemishe zake si aliona ndizi mbivu! Alijaribu kukwea mgomba azinyakue na kuzifaidi asifue dafu. Hivyo, japo ndizi zilikuwa mbivu, alisema ‘sizitaki mbichi hizi.’ Juzi, nilimsikia fyatu si sungura aliyenikumbusha kisa hiki na mafunzo lukuki.

Kwanza, sikuamini kuwa mja aweza kuwa kama mnyama achilia mbali mdudu. Hayo, tuyaache. Ni kujiuliza na kujijibu. Je, unawezaje kuwa juha kama sungura zwazwa katika kisa hiki?

Pili, niulize kifyatufyatu, tena kwa unyenyekevu. Je, amelijua hili leo au ni baada ya kupigwa pini kutokana na mazabe na ufyatu vya kufuja hiyo misaada?

Tatu, je, haya yalitoka moyoni au ni rongorongo mdomoni kuwazingua na kuwazuga mafyatu wabebao zigo la misaada au ni ‘sizitaki hizi mbichi’ baada ya kutofikika na kushikika? Mwenzenu nahitaji misaada. Maana, bila misaada, sitaweza kuwatawala mafyatu.

Nne, je, kama yaliyosemwa ni kweli, nini mikakati ya kujitegemea ili kuachana na utegemezi kama si aina fulani ya utegemezi kiakili au kujifyatua ufahamu kwa vitu vilivyo wazi?

Kuongopa ni vibaya; vibaya zaidi ni uongo wenyewe unapokosa mashiko na ushawishi na kukinzana na uhalisia. Bila misaada, mafyatu wanaozaliana kama hawana akili nzuri nitawalisha nini? Naomba maelezo fikirishi na tunduizi yasiyo na utundu na rongorongo uchwara.

Tano, je, mafyatu waliogoma kufyatuka kuwafyatua wanaowafyatua kama huyu wana jeuri, uwezo, na utamaduni wa kujitegemea? Je, kati ya hawa tegemezi wapewa misaada wakaifuja na waitoawao, nani kapitwa na wakati na nani abadilike?

Sita, tuwe wakweli. Je, kwa sanaa na mazingaombwe haya, mhusika atanya kweli au ni kufuruhisha kijiwe au ataramba matapishi yake kama yule aliyewahi kubweka akahoji wasiohojiwa eti ‘nyinyi ni nani’ asijue ni mafyatu?

Saba, je, mafyatu, japo hawafyatuki na kufyatua wapaswao kufyatuliwa kama huyu ni mataahira hadi kuamini upupu utokanao na ulevi wa maulaji na ukosefu wa busara? Nani anaweza kuishi bila misaada wakati misaada ni sera?Je, kati ya walaji na waliwaji nani aishiye kwa misaada?

Nane, wakati tukiwakamia na kuwandia watoa misaada, tujiulizwe swali rahisi tu. Je, nani anamwendea nani kati ya mtoa na mpokea misaada? Ama kweli, wahenga walisema, shibe ni mwana malevya na njaa mwana malegeza!

Tisa, inakuwajekuwaje fyatu mzima anafyatua vitu visivyoingia hata kwenye ubongo wa kuku? Nani anamfyatua nani kwa urongo huu mchana kweupe? Kweli kupe anaweza kusimama na kusema ‘sasa kutegemea damu mwisho kwa vile ng’ombe wamegoma kunyonywa? Tunaambwa dunia imebadilika? Imebadilika vipi na tangu lini na kwanini wakati huu?

Kumi, Fyatu ni muumini wa ukweli hata uwe mchungu kiasi gani. Tuache masihara. Tunaacha utegemezi kwa mipango ipi ya maana na inayoingia akilini?

Tunaachaje utegemezi bila kuacha upigaji njuluku za mafyatu na matumizi ya hovyo? Juzi, fyatu Tarampu kakinukisha pale Ghuba hadi wese likapanda na kuadimika.

Je, mafyatu tumeacha kupenda misafara mirefu ya ndinga hata kwenda kwenye jando na unyago? Je, tumeacha kulindana hasa pale misaada inapopigwa na wapigaji? Je, tunachapa kazi au kuchapa soga kama kudai eti dunia imebadilika, hivyo, nasi tubadilike bila kubadilika zaidi ya kutoa matamko yasiyoingia hata kwenye ubongo wa chawa na funza?

Kumi na moja, tembo japo ana maguvu mengi ya kuweza kuangusha miti na magogo, hana hata kibanda cha kuweka ubavu wake. Anazidiwa na ndege. Pamoja na kuwa na ubongo mdogo usiojaa hata kwenye kijiko, nyuni hujenga kiota chake na akautononoa usingizi na vifaranga vyake. Mamba, pamoja na maguvu yake, humeza kila kiingiacho mdomoni.

Kuku hula asichozalisha na kuzalisha asichokula. Nani huyu fyatu akumbatiaye ukuku na akijiona mjanja kama sungura katika kisa cha sizitaki mbichi hizi?

Kumi na mbili, wakati tukijihadaa na kujiridhisha kuwa tunawahadaa mafyatu kuwa tutaanza kujitegemea, twapaswa kujiuliza. Nini mbadala wa kuishi bila kutegemea misaada wakati tangia kale na kale, tumekuwa tukiishi kwa kutegemea misaada tusijue tutalipa vipi?

Je, kwanini hatuwaelezi mafyatu ni kwanini tuliishi kwa ku misaada ilhali Mwenyezi God alitujalia raslimali lukuki au ni yale ya kuku kuzalisha mayai akaishi kwa nafaa kavu isiyo na virutubisho? Nani huyu tumuone aishie bila kutegemea misaada? Je, ukweli na uhalisia ni vipi katika hili?

Wakati mwingine kunyamaa ni bora kuliko kufyatuka usijue uwafyatuao nao wana akili. Heri alaye kimyakimya kuliko alewaye maulaji hadi akapayuka na kufyatuka visivyofyatulia.

Mnaochukia misaada siwalazimishi kuipenda. Mie na misaada ni kama samaki na maji. Hizi bange! Hivi, naongelea nini? Kumbe najiandaa natunga kitabu cha ‘Hadithi za Fyatu na Fyatuzi!’ Plizi, usisome upuuzi huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *