Wanufaika mikopo ya 10% watakiwa kurejesha kwa wakatiWanufaika mikopo ya 10% watakiwa kurejesha kwa wakati

KILIMANJARO: MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amewataka wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kurejesha fedha hizo kwa wakati ili kuwezesha wananchi wengine kunufaika na mikopo hiyo.

Babu alitoa wito huo jana wakati wa hafla ya kukabidhi mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 1.1 kwa vikundi 82, iliyofanyika katika viwanja vya Uhuru Park, Manispaa ya Moshi na aliwataka wanufaika kuthamini mikopo hiyo kwa kuwa haina riba na inalenga kuwainua kiuchumi.

“Hongereni kwa kupata mikopo ya Sh bilioni 1.1. Nawakumbusha murejeshe fedha hizi kwa wakati ili na wenzenu wapate fursa ya kukopa. Mikopo hii haina riba, hivyo ni wajibu wenu kuwa waaminifu na kuirejesha. Ni tofauti na mikopo ya benki yenye riba,” alisema Babu.

Pia aliwataka viongozi wa Wilaya ya Moshi kuwafuatilia wanufaika wote waliokopa miaka mitatu hadi minne iliyopita bila kurejesha fedha hizo, ili wachukue hatua za kuhakikisha mikopo hiyo inalipwa.

“Wale waliochukua mikopo miaka mitatu au minne iliyopita na hawajairejesha watafutwe wote warejeshe fedha hizo. Vijana wanaohitimu shule na wanaotaka kukopa watapata wapi fedha kama waliokopa hawarudishi?” alihoji.

Alisema Serikali imeanzisha utaratibu wa mikopo hiyo si kwa sababu fedha hazina matumizi mengine, bali kama mkakati wa kuwawezesha vijana na makundi maalumu kujenga uchumi kupitia shughuli za uzalishaji.

Aidha, aliwahimiza wanufaika wa mikopo ya bajaji na bodaboda kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani, pamoja na kurejesha mikopo kwa wakati ili waweze kunufaika tena na fursa nyingine za uwezeshaji.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Mwajuma Nasombe, alisema tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, halmashauri hiyo imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 7.07 kwa vikundi 840 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Alisema kati ya fedha hizo, vikundi 549 vya wanawake vimepokea Sh bilioni 3.8, vikundi 221 vya vijana vimepatiwa Sh bilioni 3.011, huku vikundi 70 vya watu wenye ulemavu vikikabidhiwa Sh milioni 215.5.

Kwa mujibu wa Nasombe, Sh bilioni 1.1 zilizokabidhiwa jana zitanufaisha vikundi 82, ambapo vikundi 42 vya wanawake vitapokea Sh milioni 463.3, vikundi 26 vya vijana Sh milioni 635.9, na vikundi 14 vya watu wenye ulemavu Sh milioni 61.9.

Aliongeza kuwa katika kipindi hicho Manispaa ya Moshi imewawezesha vijana kwa kuwapatia bajaji 50 na bodaboda 20, huku katika hafla hiyo bajaji 23 na bodaboda nane zikikabidhiwa kwa wanufaika mbalimbali ili kuongeza ajira na kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.

“Utoaji wa mikopo hii umeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuanzisha mitaji ya biashara, kuimarisha uzalishaji, kuongeza ajira na kuchochea maendeleo ya uchumi katika halmashauri yetu,” alisema.

Akizungumzia changamoto, Nasombe alisema baadhi ya wanufaika bado hawarejeshi mikopo kwa wakati, hali inayopunguza uwezo wa halmashauri kuwafikia wanufaika wengine. Alibainisha kuwa changamoto kubwa ipo kwenye mikopo ya miaka ya nyuma.

Alitaja pia migogoro ya ndani ya vikundi, mabadiliko ya wanachama bila kufuata taratibu na matumizi ya mikopo nje ya malengo yaliyokusudiwa kuwa ni miongoni mwa sababu zinazoathiri urejeshaji wa fedha.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, aliwataka wanufaika kutumia mikopo hiyo kwa shughuli walizoainisha wakati wa kuomba fedha, akisisitiza kuwa mfuko huo ni wa mzunguko na unategemea urejeshaji wa wakati.

“Fedha hizi ni za kuzunguka. Nendeni mkafanye shughuli mlizoziainisha kwenye maombi yenu. Msiende kununua pochi, hereni, kuposa au kumpa mshikaji wenu. Lengo ni kufanya shughuli za uzalishaji, kurejesha mikopo kwa wakati na kuwawezesha wengine nao kukopa,” alisema.

Aliongeza kuwa halmashauri itaendelea kuwafuatilia wadaiwa wa mikopo ya nyuma ili fedha hizo ziendelee kuwafikia wananchi wengi zaidi, huku akiwahimiza wanufaika kufanya kazi kwa bidii, kukuza mitaji yao na kuajiri wengine kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya uchumi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *