Rais wa Iran na Waziri Mkuu wa India wamesisitiza azma thabiti ya nchi zao ya kukuza na kuimarisha ushirikiano wa pande mbili.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian, amesema kuwa uhusiano kati ya Tehran na New Delhi una uwezo mkubwa wa kupanua ushirikiano wa pande mbili katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kikanda. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo mbili, pamoja na ushirikiano wa pande nyingi, hususan katika mfumo wa kundi la BRICS.

Rais Pezeshkian alitoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo ya simu aliyofanya Jumanne jioni na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, ambapo alieleza kuridhishwa kwake na maandalizi pamoja na uendeshaji wenye mafanikio wa mkutano wa Mawaziri wa Mafuta na Nishati wa nchi wanachama wa kundi la BRICS, ulioandaliwa na India.

Aidha, Rais Pezeshkian alieleza matumaini yake ya kupanuliwa zaidi kwa ushirikiano na mahusiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na India kupitia mifumo ya ushirikiano wa pande nyingi, hususan katika mfumo wa kundi la BRICS.

Akisisitiza dhamira ya Iran ya kuendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano wake na India, Rais Pezeshkian amesema:

“Mahusiano ya pande mbili, yenye msingi wa historia ndefu na urithi wa muda mrefu, yamejengwa juu ya misingi ya kuheshimiana. Aidha, yana uwezo mkubwa wa kuinua kiwango cha ushirikiano kati ya nchi zetu katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, biashara, masuala ya kimataifa na usafirishaji wa bidhaa na mizigo (transit).”

Katika mazungumzo hayo, Rais Pezeshkian alieleza kuwa Tehran na New Delhi zinafanana katika mitazamo yao kuhusu masuala mengi ya kikanda na kimataifa, hususan ndani ya mashirika na majukwaa ya ushirikiano wa pande nyingi. Alisisitiza kuwa maelewano hayo yanaweza kufungua njia ya kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na kupanua uhusiano wa kina kati ya nchi hizo mbili.

Katika sehemu nyingine ya mazungumzo hayo, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alizungumzia hati ya makubaliano ya maelewano iliyofikiwa kwa lengo la kumaliza mapigano na kusitisha vita, akisisitiza umuhimu wa pande zote zinazohusika kutekeleza kikamilifu ahadi zao kama zilivyoainishwa katika makubaliano hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *