
Nairobi. Wanafunzi wanane wa kike wamefikishwa mahakamani nchini Kenya wakikabiliwa na mashtaka ya mauaji, wakituhumiwa kuhusika na moto ulioteketeza bweni la shule na kusababisha vifo vya wanafunzi wenzao 16.
Wasichana hao wamefikishwa mbele ya Mahakama Kuu ya Kibera jijini Nairobi jana Jumatano, ambapo walikana mashtaka yote mbele ya Jaji Diana Kavedza. Hata hivyo, upande wa mashtaka haujatoa maelezo ya kina kuhusu ushahidi unaowahusisha na tukio hilo.
Moto huo ulitokea mwishoni mwa Mei mwaka huu katika bweni la Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Utumishi iliyopo Gilgil, Kaunti ya Nakuru, katika eneo la Bonde la Ufa. Mbali na vifo vya wanafunzi 16, tukio hilo liliacha wanafunzi wengine 79 wakijeruhiwa.
Kwa mujbu wa DW, kesi hiyo imeibua upya mjadala kuhusu usalama wa mabweni na ongezeko la matukio ya moto katika shule za Kenya, huku mamlaka zikiendelea na uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo.
Kwa mujibu wa takwimu zilizowahi kutolewa na mamlaka za Kenya, matukio ya wanafunzi kuchoma moto shule siyo jambo jipya. Ripoti moja ilibaini kuwa mwaka 2018 pekee kulirekodiwa visa 63 vya uchomaji moto katika shule mbalimbali nchini humo.
Mwaka 2001, wanafunzi waliwahi kushtakiwa kwa kuhusika na moto ulioua watu 67 katika shule moja iliyoko Kaunti ya Machakos.
Aidha, mwaka 2024, moto mwingine mkubwa ulitokea katika Shule ya Hillside Endarasha iliyopo Kaunti ya Nyeri, ambapo wanafunzi 21 wa kiume walipoteza maisha baada ya bweni kuteketea.
Matukio hayo yamekuwa yakizua wasiwasi kuhusu usalama wa shule za bweni nchini Kenya, huku serikali ikiendelea kutafuta njia za kuimarisha mifumo ya tahadhari na kukabiliana na majanga ya moto katika taasisi za elimu.