DAR ES SALAAM: Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imewahimiza wananchi kutumia fursa ya Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kujifunza kuhusu uwekezaji na kuanza kuwekeza katika bidhaa mbalimbali za masoko ya mitaji.
Akizungumza katika maonesho hayo, Afisa Uhusiano na Elimu kwa Umma wa CMSA, Stella Anastazi, amesema mamlaka hiyo ndiyo msimamizi wa sekta ya masoko ya mitaji nchini na ina jukumu la kuidhinisha bidhaa mbalimbali za uwekezaji, ikiwemo hisa, hatifungani na mifuko ya uwekezaji wa pamoja.
Amesema CMSA pia hutoa leseni kwa taasisi na kampuni zinazotoa huduma za uwekezaji. Miongoni mwa leseni hizo ni za mameneja wa mifuko ya uwekezaji, ambao huanzisha na kusimamia mifuko inayowawezesha wananchi kuwekeza kwa pamoja, pamoja na leseni za mawakala wa soko la hisa wanaowasaidia wawekezaji kufungua akaunti za uwekezaji, kutoa ushauri wa kitaalamu na kununua au kuuza hisa na hatifungani kwa niaba yao.
Stella amesema kuwa CMSA pia ilianzisha Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), ambalo ni mnada wa kidijitali unaowezesha mazao na bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini kuuzwa kwa wanunuzi wa ndani na nje ya Tanzania. Amesema mfumo huo umeendelea kuwasaidia wakulima na wafanyabiashara kupata soko la uhakika, kuongeza ushindani wa bidhaa zao na kuboresha mapato.

Ameeleza kuwa mwitikio wa wananchi katika banda la CMSA tangu kuanza kwa maonesho umekuwa mkubwa, huku wengi wakifika kupata elimu ya uwekezaji, kufungua akaunti za uwekezaji na kutatua changamoto mbalimbali walizokuwa wakikumbana nazo.
Kwa mujibu wake, huduma zote zinazohusiana na sekta ya masoko ya mitaji zinapatikana katika banda la CMSA kupitia ushiriki wa wadau mbalimbali, wakiwemo Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), mawakala wa soko la hisa, Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) na mameneja wa mifuko ya uwekezaji.
Aidha, Stella amewataka wawekezaji kuhakikisha wanahuisha taarifa zao binafsi, ikiwemo namba za simu na akaunti za benki, ili kuepuka kuchelewa kupokea gawio. Amesisitiza kuwa magawio yaliyoshindwa kulipwa kutokana na taarifa kutokuwa sahihi hayapotei, bali hulipwa yote kwa pamoja mara baada ya mwekezaji kuhuisha taarifa zake, hata kama ni ya miaka kadhaa iliyopita.
Ametoa wito kwa wananchi ambao bado hawajatembelea banda la CMSA lililopo ndani ya banda la Wizara ya Fedha kufanya hivyo kabla ya maonesho hayo kumalizika Julai 13. Amesema wageni watapata fursa ya kuanza uwekezaji, kupata ushauri wa kitaalamu, kutatua changamoto mbalimbali za uwekezaji na kujifunza taratibu za kupata leseni zinazowezesha kushiriki moja kwa moja katika sekta ya masoko ya mitaji nchini.