Watu wakishikilia bango la Ayatollah Ali Khamenei

Chanzo cha picha, Anadolu via Getty Images

Iliyochapishwa

Muda wa kusoma: Dakika 8

Sherehe ya “kuaga na mazishi” ya Ali Khamenei, zaidi ya miezi minne baada ya kuuawa kwake, imepangwa kuanza mjini Tehran siku ya Jumamosi. Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi (IRGC), vyombo vya usalama, na taasisi mbalimbali za serikali zimeagizwa kuandaa sherehe hiyo, huku maafisa wa serikali wakiitaja kuwa “mazishi ya karne.”

Katika siku zilizopita kuelelekea tukio hilo, maafisa walitangaza kuwa maandamano na misafara ya maelfu ya watu imesajiliwa, na kwamba mpango wa malazi kwa zaidi ya watu milioni moja umeandaliwa, na “njia maalum” ya kupitia imewekwa ili kudhibiti umati wa watu katikati ya jiji la Tehran. Baadhi ya maafisa pia wamekadiria kuwa kati ya watu milioni 12 hadi 20 wanatarajiwa kuhudhuria tukio hilo.

Kikosi cha IRGC mjini Tehran ndicho kitakachosimamia shughuli hiyo, huku serikali na taasisi nyingine za kiserikali pia zikishiriki katika maandalizi na utekelezaji wake. Waandaaji wanasema kuwa kiwango cha maandalizi na ukubwa wa sherehe hii haina kifani ikilinganishwa na matukio yaliyopita.

.

Chanzo cha picha, MORE

Utata ulioibuka

Licha ya maelezo ya kina yaliyotolewa kuhusu jinsi sherehe hiyo itakavyofanyika, maswali kadhaa muhimu bado hayajapata majibu. Mojawapo ya maswali muhimu zaidi ni iwapo Mojtaba Khamenei, kiongozi wa tatu wa Jamhuri ya Kiislamu, atahudhuria mazishi ya baba yake au la.

Pia haijabainiki ikiwa watoto wengine wa Ali Khamenei watahudhuria sherehe hiyo. Wanawe hawajaonekana katika hafla yoyote ya hadhara tangu vita vya siku 12 vya mwaka jana, na hakuna taarifa za wazi zilizotolewa kuhusu hali yao wakati wa vita hivyo vya siku 40.

Hali hii ya kutokuwa na uhakika inajitokeza katika mazingira ambapo, wakati wa shambulio la tarehe 21 Machi mwaka jana, mbali na Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu, baadhi ya jamaa zake pia waliuawa, wakiwemo mkwe wake, mjukuu wake, mmoja wa mabinti zake, na mke wa Mojtaba Khamenei.

Hivi karibuni, Hassan Khojasteh Bagherzadeh, shemeji yake Ali Khamenei, aliwataka watu “wamuombee binti wa pili wa kiongozi huyo aliyeuawa” katika kipindi cha televisheni.

Akielezea hali ya “binti wa pili” wa Ali Khamenei, alisema kuwa “ilikuwa kama ya mgeni aliyeanguka jangwani,” na hakutoa maelezo zaidi kuhusu ukubwa wa majeraha yake au hali yake ya kiafya kwa ujumla, jambo linalozidisha suitafahamu kuhusu hali ya afya ya familia ya Ali Khamenei.

Kando na wanawe wanne wa kiume Ali Khamenei, alikuwa na mabinti wawili. Bushra Khamenei aliuawa siku hiyo hiyo ya shambulio la kwanza. Kwa kuzingatia kuwa Bushra Khamenei aliuawa, kauli hiyo inaelekea kuashiria Hoda Khamenei, ambaye ni mkewe, Misbah-ul-Huda Bagheri Kani, aliuawa siku hiyo hiyo.

Katika miezi ya hivi karibuni, ripoti zinazokinzana zimechapishwa kuhusu hali ya afya ya Mojtaba Khamenei na mchakato wake wa matibabu.

Ali Akbar Pourjamshidian, katibu wa kamati ya maandalizi ya mazishi ya Ali Khamenei, alisema katika mkutano na waandishi wa habari mnamo Julai 29, 2021, kwamba suala la kuhudhuria kwa Mojtaba Khamenei katika mazishi hayo “haliko ndani ya mamlaka na taarifa za kamati ya maandalizi ya mazishi.”

Alisema ikiwa kutakuwa na mpango wa Mojtaba Khamenei kuhudhuria sherehe hiyo, “itatangazwa rasmi kwa umma wakati mwafaka na Ofisi ya Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi pamoja na Ofisi ya Kiongozi wa Mapinduzi pekee.”

Kwa upande mwingine, bado haijabainika ni nani atakayeongoza sala ya mazishi ya marehemu Ali Khamenei. Katika desturi za wanazuoni wa Kishia, hasa miongoni mwa viongozi wa kidini, uchaguzi wa mtu atakayeongoza sala ya mazishi unaweza kuwa na umuhimu wa kimaana na kisiasa.

Badhi ya wachambuzi wanaamini kuwa endapo Mojtaba Khamenei atajitokeza hadharani baada ya kutoweka machoni pa watu kwa miezi kadhaa na kuongoza sala ya mazishi, hatua hiyo inaweza kuambatana na tafsiri mbalimbali za kisiasa.

Hata hivyo, kutokana na ukosefu wa taarifa rasmi kuhusu wosia wa Ali Khamenei, ni vigumui kutoa ufafanuzi kuhusiana na suala hili.

Ahmad Alam-ul-Huda, imamu wa sala ya Ijumaa mjini Mashhad, alisema mwezi uliopita: “Hatuna taarifa kuhusu yaliyomo kwenye wosia wa Ali Khamenei, na wosia huo uko mikononi mwa wanawe.”

Hassan Hassanzadeh, Kamanda wa Kikosi cha Mohammad Rasoolullah katika eneo la Tehran, ndiye kimsingi anayeendesha hafla hiyo.

Chanzo cha picha, HAMSHAHRI

Wageni kutoka nje

Mchanganyiko wa maafisa wa kisiasa, kidini, na usalama watakaozuru Tehran kuhudhuria tukio hilo unaweza kuwa mojawapo ya mambo ya kuvutia zaidi katika tukio hilo. Baadhi ya waangalizi wanaamini kwamba kutokuwepo kwa baadhi ya nchi kutakuwa na umuhimu sawa uwepo wa wageni kutoka nje.

Kulingana na katibu wa makao makuu ya kitaifa ya sherehe hiyo, maafisa na watu mashuhuri kutoka nchi kadhaa wamethibitisha kuwa watahudhuria sherehe hiyo.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran Eskandar Momeni amesema kwamba marais, maspika wa bunge, mawaziri wakuu, na mawaziri kutoka nchi tofauti watahudhuria sherehe hiyo.

Maafisa wamedai kwamba waandishi wa habari 800 wa kigeni wamepangwa kuangazia tukio hilo.

Mazishi hufanywaje?

Serikali ya Iran imetangaza kaulimbiu rasmi kuwa “Lazima Tuinuke” na ishara ya “ngumi iliyokunjwa” kama nembo ya mazishi ya Ali Khamenei.

Kwa mujibu wa mpango uliotangazwa na mamlaka husika, shughuli za “kuagwa kwa mwili na mazishi” ya Ali Khamenei zitafanyika katika hatua kadhaa na kwa siku kadhaa mfululizo.

Kwa mujibu wa tangazo la Gavana wa Tehran na kamati ya maandalizi, shughuli hizo zitaanza asubuhi ya Jumamosi, Julai 4, kwa “hafla ya kuuaga” mwili wa kiongozi huyo mkuu aliyeuawa katika “Ukumbi wa Sala wa Imam Khomeini.” Milango ya ukumbi huo itafunguliwa kwa umma saa 12 asubuhi, na watu wanatarajiwa kufika hapo kwa ajili ya “kutoa heshima zao za mwisho” kwa muda wa siku mbili, hadi jioni ya Jumapili, Julai 5.

Hassan Hassanzadeh, kamanda wa Kikosi cha Walinzi cha Mohammad Rasoolullah katika eneo lote la Tehran, ambaye ndiye msimamizi mkuu wa shughuli hizo, amesema kuwa jeneza la Ali Khamenei litawekwa kwenye jukwaa la juu ili liweze kuonekana kutoka maeneo mbalimbali.

Alisema kuwa utaratibu wa kuingia na kutoka kwa umati wa watu katika eneo hilo umeandaliwa ili kila mmoja aweze kuingia, kuaga, na kutoka ndani ya muda wa takriban dakika 15 hadi 20.

Mazishi yatafanyika Tehran mnamo Julai 5. Kamanda huyo wa kikosi cha IRGC cha Mohammad Rasoolullah amesema kuwa gari litakalotumika katika msafara wa mazishi limetengenezwa kwa muundo unaofanana na “Kaburi Tukufu la Imam Reza.”

Maafisa wamesisitiza mara kwa mara kuwa “usalama” ndio kipaumbele chao. Kwa mujibu wao, taasisi mbalimbali za kijeshi, vyombo vya dola, idara za ujasusi, na vyombo vya sheria vinashirikiana katika maandalizi ya shughuli hizo; na kwa kuweka safu mbalimbali za ulinzi kuanzia kwenye milango ya kuingilia Tehran hadi eneo la tukio, jitihada zimefanywa kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika “bila vurugu wala usumbufu.”

Baada ya Tehran, shughuli za mazishi zitaendelea katika mji wa Qom mnamo Julai 6. Inasadikiwa kuwa sala ya mazishi itaongozwa na mmoja wa viongozi wa kidini huko Jamkaran.

Picha kutoka kwenye ibada ya mazishi ya ishara ya Khamenei huko Najaf iliyofanyika siku za hivi karibuni. Sherehe kuu zimepangwa kufanyika Najaf na Karbala tarehe 8 Julai.

Chanzo cha picha, Getty Images

Najaf na Karbala

Ali Khamenei aliwahi kuzuru Iraq mara mbili tu katika maisha yake, akiwa na umri wa miaka saba na kumi na nane, na baada ya hapo hakutembelea tena Najaf au Karbala. Kulingana na ratiba iliyotangazwa, mwili wake umepangwa kupelekwa Iraq tarehe 8 Julai kupitia uwanja wa ndege wa Najaf.

Baada ya ibada ya mazishi katika kaburi la Imamu wa kwanza wa Kishia huko Najaf, shughuli hiyo itaendelea katika jiji la Karbala na kisha mwili utarejeshwa Iran kupitia Najaf.

Maafisa wa Iran wameelezea kufanyika kwa shughuli hiyo nchini Iraq kama mwitikio wa maombi kutoka kwa makundi mbalimbali ya Iraq na kusisitiza vipengele vya kidini na vya kuvuka mipaka ya kitaifa vya tukio hilo.

Huku hayo yakijiri baadhi ya wachambuzi wanaamini kuwa kufanyika kwa ibada hizo huko Najaf na Karbala kunaweza kuonekana kama jaribio la kuangazia hadhi ya Ali Khamenei inayovuka mipaka ya kitaifa miongoni mwa Washia wa eneo hilo.

Baadhi ya wachunguzi wametafsiri hatua hii kama sehemu ya juhudi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kudumisha na kuonyesha ushawishi wake wa kidini na kisiasa katika mojawapo ya vituo muhimu zaidi vya ulimwengu wa Kishia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, ambaye alisafiri hadi Baghdad siku chache zilizopita kuratibu shughuli hiyo, alisema ibada hiyo ina “umuhimu wa kiishara” na kuongeza kuwa kufanyika kwa shughuli hiyo katika miji ya Najaf na Karbala kunaonyesha kuwa nafasi ya Ali Khamenei miongoni mwa Washia inavuka mipaka ya Iran.

Katika muktadha huu, baadhi ya maafisa wa Iran wameelezea tukio hili kama fursa ya kuimarisha “uhusiano wa kina kati ya mataifa hayo mawili” na kuliona kama sehemu ya mzunguko mpana zaidi wa kisiasa na kidini katika eneo hilo.

Serikali ya Iraq ni moja ya waandaaji wakuu wa tukio hilo nchini humo. Kulingana na ripoti, tukio hilo litafanyika kwa uratibu wa moja kwa moja na Ofisi ya Waziri Mkuu wa Iraq kwa ushirikiano na taasisi na wizara mbalimbali za serikali. Baadhi ya maafisa wa Iraq wameelezea kuwa mwenyeji wa tukio hilo ni “heshima ya kihistoria” na wamesema kuwa uwezo wote wa kiutawala, huduma, na usalama utahamasishwa ili kufanikisha tukio hilo.

Shirika la Habari la Mehr liliripoti kuhusu mipango hiyo, likuwanukuu maafisa wa Iraq, limesema kwamba mikoa ya Najaf na Karbala, wizara za uchukuzi, mambo ya ndani, na mambo ya nje za Iraq, Vikosi vya Uhamasishaji wa Umma (PMF), na Ofisi ya Waziri Mkuu wa Iraq ni miongoni mwa taasisi zinazohusika na uratibu wa shughuli hiyo. Baada ya kufanyika kwa sherehe za mazishi jijini Tehran, Qom, Najaf, na Karbala, hatua ya mwisho ya sherehe hizo imepangwa kufanyika katika jiji la Mashhad mnamo tarehe 8 Julai, ambapo Ali Khamenei atazikwa katika kaburi takatifu la Imamu wa nane wa Kishia.

Maafisa wanaoratibu mazishi ya Ali Khamenei wametangaza kuwa, baada ya mazishi hayo, sherehe za kidini na dua zitafanyika katika mikoa mbalimbali kwa muda wa siku arobaini, huku makongamano na sherehe zikitarajiwa kuandaliwa hadi kufikia maadhimisho ya kumbukumbu ya mazishi ya Ali Khamenei.

Umuhimu wa kisiasa wa sherehe hiyo

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Mazishi ya Ali Khamenei yanafanyika wakati ambapo Iran inakabiliwa na changamoto nyingi za kisiasa na kijamii.

Kulingana na baadhi ya wachambuzi, maandamano ya nchi nzima na hatua ya mamlaka kutumia nguvu kubwa kuwadhibiti waandamanaji katika miezi ya hivi karibuni kumezidisha kile wanachoita “mgogoro wa uhalali wa kisiasa.”

Kulingana na wachambuzi hao, mazishi ya viongozi katika mifumo ya kiitikadi haifanyi kazi ya kuomboleza tu, bali inaweza kuwa jukwaa la kuonyesha mshikamano, kutangaza tena misimamo rasmi, na kuwasilisha ujumbe wa kisiasa.

Kwa mtazamo huu, sherehe inayokuja, pamoja na kipengele chake cha kidini, pia ina vipimo vya kisiasa. Baadhi ya waangalizi wanaamini kuwa sherehe hii inaweza kuchukua nafasi muhimu katika mchakato wa ”kukabidhi” mamlaka na kuanzisha utaratibu wa kisiasa baada ya Ali Khamenei.

Baadhi ya wachunguzi pia wanaamini kuwa sherehe hii, pamoja na kuonyesha kiwango cha uhamasishaji na uungaji mkono kwa serikali, inaweza pia kuwa na jukumu katika mchakato wa kuhamisha madaraka na kuleta utulivu wa kisiasa nchini Iran. Sherehe hiyo pia imejulikana kama “kuahidi tena utii” kwa Mojtaba Khamenei.

Hata hivyo, kundi la wachambuzi wanasisitiza kuwa hata kuenea kwa sherehe hizo hakumaanishi kusuluhisha masuala ya kina ya kisiasa na kijamii na hakuwezi pekee kuziba mapengo kati ya serikali na sehemu fulani za jamii.

Wakati huo huo, sherehe hii inafanyika wakati ambapo tahadhari ya waangalizi wengi inazingatia njia ya uhamisho wa mamlaka, usawa wa nguvu za kisiasa, na majibu ya jamii kwa maendeleo ya miezi iliyopita.

Yote tisa kumi ni kuwa umuhimu wa sherehe hii unatathminiwa na wachambuzi wengi kuwa ni zaidi ya ibada ya maombolezo, na wanalichukulia kuwa ni tukio ambalo linaweza kutoa dalili za njia ya kisiasa ya Jamhuri ya Kiislamu katika zama za baada ya Ali Khamenei.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *