Huku taifa la Iran likimuaga kwa hamasa Kiongozi wake wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyeuawa shahidi, tukio hili limeakisi wazi na kwa mara nyingine mandhari ya kuvutia ya umoja, kusimama imara, na mwamko wa kina wa Umma wa Kiislamu.

Tarehe 28 Februari mwaka huu, Marekani na utawala wa kigaidi wa Israel zilitekeleza jinai kubwa zaidi katika karne hii kwa kumuuga kigaidi Ayatollah Seyyed Ali Khamenei, Kiongozi wa pili wa Mapinduzi ya Kiislamu na mamlaka kuu ya kidini katika ulimwengu wa Kishia. Jinai hii haitafutika kamwe katika kumbukumbu ya kihistoria ya taifa la Iran na Umma wa Kiislamu.

Hata hivyo, mauaji haya ya kishahidi—kama yalivyo mauaji ya viongozi na shakhsia wengine mashuhuri wa kidini—yamebadilika kuwa nembo ya umoja na nguvu nchini. Kati ya tarehe 6 na 9 mwezi huu wa Julai, dunia itashuhudia mazishi—makubwa zaidi katika historia ya mwanadamu yatakayohudhuriwa na mamilioni ya waombolezaji—kwa ajili ya kutoa heshima zao za mwisho kwa mwili mtakatifu wa kiongozi huyo aliyeuawa shahidi. Mazishi haya yatafanyika mjini Tehran, katika Haram ya Hazrat Masoumeh mjini Qum, Najaf, Karbala, na hatimaye kuzikwa katika Haram Tukufu ya Imam Ridha (as) mjini Mashhad. Watu walioishi pamoja na Kiongozi wao huyu shujaa sasa wanamuaga kwa heshima kubwa.

Uwepo wa mamilioni ya watu katika mazishi ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu unaidhihirishia jamii ya kimataifa uhusiano imara uliopo kati ya wananchi na uongozi ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran—ukweli ambao adui anauogopa sana. Hasa katika miaka ya hivi karibuni, ambapo adui ametumia kila mbinu, vikiwemo vita vya kushawishi fikra na mitazamo—katika jaribio la kuvunja na kukata uhusiano huo kati ya wananchi wa Iran na uongozi wao. Mahudhurio makubwa ya wananchi katika mazishi ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu yanathibitisha hadharani kuwa adui si tu kwamba ameshindwa kufikia malengo yake, bali pia kwamba mauaji ya kigaidi ya kiongozi huyo yameimarisha zaidi uhusiano huo madhubuti uliopo kati ya serikali na raia.

Adui, hasa katika muongo mmoja uliopita, ameendesha pia kampeni kubwa ya propaganda kwa madhumuni ya kudhoofisha na kuchafua jina la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mhimili mzima wa muqawama katika eneo. Bila shaka, wito wa wananchi na uongozi wa Iraq wa kupelekwa mwili na kufanyika mazishi ya kiongozi huyo shahidi nchini kwao—sambamba na kujitokeza kwa wingi kwa mamilioni ya Wairaqi—kunathibitisha kuwa uhusiano huu hauwezi kuvunjwa wala kudhoofishwa.

Hivyo, ushiriki wa mamilioni ya watu katika marasimu ya mazishi ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu unaweza kuonekana kama kilele cha mfululizo wa vipigo ilivyopata Marekani na utawala wa Kizayuni katika makabiliano yao na mhimili wa muqawama na hasa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiongozwa na Ayatollah Khamenei. Watu shupavu na wasio na mfano wa Iran—ambao wamekuwa na nafasi muhimu katika kuvuruga malengo ya adui kwa kujitokeza mitaani kila siku pembeni ya wanajeshi wanapigana katika mstari wa mbele vitani tangu tarehe 28 Februari—sasa wanaonyesha nguvu ya umma ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupitia ushiriki wao wa mamilioni ya watu katika mazishi ya Kiongozi Shahidi.

Kwa kuhitimisha, ni lazima ieleweke kuwa kujitokeza kwa wingi wananchi katika mazishi ya kiongozi huyo shahidi wa Mapinduzi kunasisitiza umuhimu wa kuendeleza njia ya Imam huyo shahidi na wakati huo huo kutangazwa utiifu kwa Kiongozi wa tatu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatollah Seyyed Mojtaba Khamenei.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *