Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amewaalika wafanyabiashara kutoka Ufaransa kuwekeza nchini Tanzania kwani kuna fursa ya kutengeneza ajira, kuhamisha ujuzi na kujenga uchumi wa viwanda kwa faida ya nchi zote mbili.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu leo, Jumatatu Julai 6, 2026, imesema Dk Mwigulu amesema hayo wakati akizungumza na washiriki wa mjadala wa kibiashara baina ya Tanzania na Ufaransa uliofanyika katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Paris, Ufaransa.
“Leo tumefanya mjadala wa kibiashara na sote tumeshuhudia makubaliano yakisainiwa baina ya Tanzania Private Sector Foundation (TPSF) na International Chamber of Commerce (ICC). Makubaliano haya siyo tu mkataba wa kawaida, bali ni daraja la kutupeleka kwenye mafanikio makubwa huko mbele,” amesema.
“Kwa hiyo ninawahimiza wafanyabiashara wa Ufaransa mtumie vyema fursa hii ya kipekee. Uamuzi utakayofanywa leo ndiyo utakaoamua mwelekeo wa sekta za uchumi za kesho kwa nchi zetu.
“Wale watakaowekeza nchini Tanzania hivi sasa, hawatakuwa tu sehemu ya mageuzi ya uchumi wetu, bali watakuwa washirika wa thamani katika kujenga moja ya uchumi wenye ushindani mkubwa zaidi barani Afrika kwa vizazi vijavyo.”
Dk Mwigulu amesema Ufaransa ina utaalamu wa hali ya juu na wa kiwango cha kimataifa katika teknolojia, uhandisi, nishati, miundombinu, viwanda, masuala ya fedha na huduma za afya.
“Kwa upande wake, Tanzania ina utulivu wa kisiasa, nafasi ya kijiografia iliyo kimkakati, rasilimali nyingi za asili, fursa shindani za uwekezaji, usimamizi thabiti wa uchumi pamoja na nguvu kazi ya vijana wengi na yenye ari kubwa barani Afrika.”
Amesema maeneo hayo yana nguvu na yanakamilishana kwani kwa pamoja yanajenga fursa za kipekee za kukuza maendeleo endelevu na ustawi wenye manufaa kwa pande zote mbili.
“Tunapoanza kwa ujasiri kutekeleza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Serikali yetu itaendelea kuwa thabiti katika kuhakikisha kunakuwepo mazingira yanayotabirika, yenye uwazi na rafiki kwa biashara, ambapo uwekezaji unalindwa, ushirikiano unathaminiwa na mafanikio yanawanufaisha wadau wote,” amesisitiza.
Pia, ameshuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya International Chamber of Commerce (ICC) na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), ambapo Mtendaji Mkuu wa TPSF, Deo Massawe, alibadilishana hati hiyo na Naibu Katibu Mkuu wa ICC, Julian Kassum.
Mapema, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, aliwaeleza washiriki wa mjadala huo kuwa kitendo kilichofanyika leo kinaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inasisitiza ushiriki wa sekta binafsi kwa asilimia 70 katika kuchochea maendeleo ya uchumi.
Kwa upande wake, Rais wa TPSF, Angelina Ngalula amesema Tanzania ipo katika nafasi ya kipekee ya kuwa kitovu cha mageuzi ya uchumi barani Afrika chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akiwa kwenye mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Saidi Yakubu.
“Kwa miaka mingi, Ufaransa imekuwa mshirika muhimu wa Tanzania katika uwekezaji. Hata hivyo, kwa sasa tunapaswa kuelekeza nguvu zetu katika kujenga ushirikiano wa muda mrefu utakaokuza uhamishaji wa teknolojia, kukuza sekta ya utalii, huduma za kifedha pamoja na uchumi wa kidijitali. TPSF iko tayari kuwezesha ushirikiano huo kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na wenzao wa Ufaransa,” alisema.
Baadhi ya kampuni za Ufaransa zilizoshiriki mjadala huo zinajihusisha na usimamizi wa nishati ya jua (ikiwemo mifumo ya taa za barabarani), usafirishaji, maji, nishati, ujenzi, viwanda, mazingira na ufugaji wa viumbe maji (ikiwemo uzalishaji wa mwani wa baharini).
Kampuni nyingine ni waendeshaji wa huduma za satelaiti wanaotoa suluhisho bunifu kwa huduma za utangazaji wa sauti na picha, intaneti ya kasi (broadband), huduma za data, usafiri wa baharini na anga. Aidha, kulikuwa na wazalishaji wa mabomba maalumu yanayotumika katika sekta ya mafuta na gesi.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde; Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi; Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu na Utamaduni (Unesco), Balozi Saidi Othman Yakubu; Mtendaji Mkuu wa MEDEF International, Philippe Gautier; Rais wa Baraza la Biashara la Ufaransa na Afrika Mashariki, Celine Gouveia; pamoja na wajumbe kutoka sekta binafsi ya Tanzania na ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Ufaransa.