Kigoma. Kesi ya uchaguzi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Clayton Chipando, maarufu Baba Levo inatarajiwa kuanza kusikilizwa leo, Jumatatu, Julai 6, 2026, Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, baada ya kukwama tarehe ya awali iliyokuwa imepangwa.

Baba Levo alitangazwa mbunge wa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025,  akimshinda mpinzani wake mkubwa kutoka ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.

Hata hivyo, wananchi wanne, Johary Kabourou, Loum Mwitu, Pendo Kombolela na Luma Akilimali wamefungua kesi dhidi ya Tume Huru ya Uchaguzi, mbunge huyo Chipando na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) wakipinga uchaguzi huo.

Katika kesi hiyo ya uchaguzi namba 28949 ya Mwaka 2025, wadai hao ambao wanajitambulisha wapiga kura katika jimbo hilo wanadai uchaguzi huo uligubikwa na kasoro nyingi.

Wanabainisha kasoro hizo ni pamoja  na ukiukwaji wa taratibu, kanuni na sheria za uchaguzi, vitendo vya rushwa na udini vilivyooneshwa na mlalamikiwa wa pili, Baba Levo.

Hivyo wanaiomba mahakama hiyo pamoja na mambo mengine iamuru ufanyike upekuzi na uhesabuji upya wa karatasi za kupigia kura na kisha ibatilishe na kutengua uchaguzi huo.

Awali, kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Victoria Nongwa ilipangwa kuanza kuunguruma Juni 18, 2026.

Hata hivyo, tarehe hiyo ilikwama kuanza kusikilizwa kutokana na walalamikaji kushindwa kuwasilisha mahakamani maelezo ya maandishi ya mashahidi wanaotarajiwa kufika mahakamani kutoa ushahidi, kama Kanuni za Mashauri ya Uchaguzi wa Wabunge za Mwaka 2025 zinavyoelekeza.

Kanuni ya 21(1) ya kanuni hizo inaelekeza usikilizwaji wa mashauri ya uchaguzi utakuwa kwa njia ya maelezo ya maandishi ya mashahidi badala ya ushahidi wa msingi wa kuhojiwa.

Kanuni ya 21(2) inaeleza baada ya usikilizaji wa awali, na ndani ya saa zisizopungua 48 kabla ya muda uliopangwa na mahakama kusikiliza shauri la uchaguzi, mlalamikaji atawasilisha kwa msajili maelezo ya maandishi ya kila shahidi ambaye anakusudia kumuita wakati wa usikilizaji yakielezea msingi wa ushahidi wake.

Hata hivyo, walalamikaji hawakuweza kuwasilisha maelezo hayo ndani ya muda, badala yake Juni 17, walifungua maombi madogo wakiomba kuongezewa muda wa kuwasilisha maelezo hayo ya mashahidi.

Maombi hayo yalisikilizwa Juni 18, 2026, na wakili wa walalamikaji hao, John Seka aliieleza mahakama walalamikaji walishindwa kuwasilisha maelezo hayo ya mashahidi ndani ya muda uliowekwa kutokana na ufinyu wa muda.

Alidai kwa kuwa usikilizwaji wa awali ulikamilika Juni 15, 2026 saa 12 jioni na usikilizwaji ulipangwa Juni 18, 2026, saa 6:00 mchana, kwa mujibu wa kanuni hizo muda wa mwisho wa kuwasilisha maelezo ya mashahidi kwa Msajili (yaani saa 48 kabla ya muda wa usikilizwaji) ulikuwa ni Juni 16, 2026 saa 6:00 mchana.

Alidai kutoka Juni 15, 2026 saa 12 baada ya kukamilika usikilizwaji wa awali mpaka Juni 16, 2026 kabla ya saa 6 mchana walikuwa na saa 18 tu, zikiwemo saa 12 zisizo za kazi (usiku).

Hivyo alidai walikuwa na siku sita tu  za kazi, ambazo zisingetosha kuwatafuta mashahidi 20, kuwahoji kuandaa nyaraka za kurasa 180 na za kielektroniki yaani picha jongefu (video) zaidi ya 60.

Mawakili wa Baba Levo, Daniel Rumenyela na Thomas Msasa walipinga maombi hayo wakitaka mahakama iyakatae hatua ambayo ingeifanya kesi ya msingi kufa kifo cha kawaida; wakidai kuwa walalamikaji walikuwa na muda wa kutosha kutekeleza jukumu hilo bali walifanya uzembe tu.

Hata hivyo, Jaji Nongwa katika uamuzi wake alikubaliana na hoja za wakili Seka wa walalamikaji, kuwa zina mashiko akawaongezea muda wa kutekeleza jukumu hilo.

Aliahirisha kesi hiyo hadi leo Julai 6, 2026 ili kuwapa walalamikaji muda wa kutosha kuandaa na kuwasilisha mahakamani maelezo hayo ya maandishi ya mashahidi wao.

Kabla ya kufikia hatua hii ya usikilizwaji ushahidi kesi hiyo ilipitia katika mvutano mkali kutokana na mapingamizi ya mara kwa mara yaliyokuwa yakiibuliwa na Serikali na Baba Levo  wakitaka iitupilie mbali wakidai kuwa imekubikwa na kasoro mbalimbali za kisheria.

Hata hivyo, jitihada za wadaiwa hao kutaka kuimaliza kesi hiyo kwa mbinu za kiufundi, kupitia mapingamizi ya awali ya hoja za kisheria zimegonga mwamba, kwani mara kadhaa mahakama hiyo imekuwa ikiyakataa mapingamizi hayo.

Kutokana na mvutano huo, muda wa awali wa usikilizwaji wa kesi za uchaguzi yaani ndani ya miezi sita uliisha kabla haijaanza kusikilizwa.

Hivyo  ilimlazimu Jaji Mkuu, George Masaju kwa mamlaka aliyo nayo kisheria kuongeza muda wa miezi sita ya usikilizwaji wa kesi hiyo.

Baada ya kupenya katika mapingamizi hayo hatimaye Jumatatu, Juni 15, 2026 kesi hiyo iliingia katika hatua ya usikilizwaji wa awali ikiwa ni maandalizi ya usikilizwaji kamili.

Katika hatua hiyo, wadaiwa walisomewa muhtasari wa madai ya kesi hiyo na kisha wakatakiwa kubainisha mambo au hoja wanazokubaliana nazo na zile wasizokubaliana nazo katika maelezo hayo, ambazo hizo ndizo upande wa wadai watakuwa na wajibu wa kuzithibitisha.

Endelea kufuatilia Mwananchi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *