Dar es Salaam. Uamuzi wa Serikali kuzuia mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa umeibua maswali tata, huku baadhi ya wachambuzi wakihoji kwa nini katazo hilo limegusa vyama vya siasa pekee, wakati mikusanyiko mingine ikiendelea kufanyika.

Wanahoji zaidi, iwapo sababu ni viashiria vya matukio ya uvunjifu wa amani, kwa nini tahadhari hiyo isichukuliwe pia kwa matukio mengine yanayokusanya watu, yakiwamo matamasha ya sherehe za ubingwa wa Yanga na Simba.

Maswali ya wadau hao wa siasa yanagusa pia mikutano ya hadhara inayoendelea kufanywa na wabunge na viongozi wa Serikali, akiwemo Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, wakisema wahalifu wanaweza kuitumia hiyo kuathiri usalama.

Kinachoibua maswali hayo ni kuwepo kwa matukio kadhaa yenye sura ya mikutano ya hadhara, na baadhi yake huzungumzia maudhui ya kisiasa, lakini yenyewe yanaruhusiwa wakati vyama vya siasa vikizuiwa.

Hata hivyo, Serikali imejibu maswali hayo ikisema uamuzi wake wa kusitisha utoaji wa vibali vya mikutano hiyo kwa vyama vya siasa umelenga kulinda usalama baada ya kubaini viashiria vya uvunjifu wa amani.

Juni 26, mwaka huu, akiwa bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, alimwelekeza Mkuu wa Jeshi la Polisi kusitisha utoaji wa vibali hivyo kwa mikutano ya vyama vyote vya siasa.

 Akizungumza na waandishi wa habari Julai 3, mwaka huu, Katambi alisema uhuru na haki ya kukusanyika na kushirikiana na wengine itatekelezwa kwa ukamilifu ikiwa masharti yatafuatwa kwa mujibu wa sheria.

“Masharti hayo hasa ni yanayolinda maslahi ya umma, usalama, amani, afya ya jamii na uhuru na haki za wengine,” alisema.

Mbona wengine wanafanya?

Akizungumzia hilo, mchambuzi wa siasa, Dk Elias Mwakibete, amesema hoja si kuhusu nani anaruhusiwa kukutana na wananchi, bali ni usawa wa matumizi ya majukwaa ya hadhara wakati vyama vya siasa vimezuiwa kufanya mikutano yao.

“Kama sababu ya zuio ni usalama wa taifa, basi wananchi wanatarajia kuona kiwango kilekile cha tahadhari kikitumika kwa kila aina ya mkusanyiko, bila kujali unafanywa na nani,” amesema.

Dk Mwakibete ameibua hoja hiyo wakati ndani ya wiki moja tangu kutangazwa kwa zuio hilo kumeshuhudiwa matukio ya sherehe za ubingwa wa Ligi Kuu kwa Klabu ya Yanga Juni 4, mwaka huu, huku Simba nayo ikifanya tukio kama hilo Juni 5, mwaka huu.

Ukiacha hayo, siku moja baada ya zuio hilo, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, aliendelea na ziara yake iliyohusisha mikutano ya hadhara.

Katika maelezo yake, Dk Mwakibete amesema mbaya zaidi viongozi wa Serikali katika mikutano yao huwazungumzia wapinzani ingawa hawawataji majina, jambo linalojenga hisia za kutokuwapo kwa uwanja sawa wa kisiasa.

“Demokrasia haihusiani tu na uhuru wa kuzungumza, bali pia kuwapo kwa haki ya kujibu. Upande mmoja ukipata nafasi ya kuzungumza bila mwingine kujibu, kunakuwa na shida kwenye usawa,” amesema.

Mikusanyiko mingine ni salama?

Mtaalamu wa historia katika siasa, Profesa Benard Mrosso, amesema uamuzi wa kiusalama unapoathiri shughuli za kisiasa ni muhimu mamlaka zitoe maelezo yanayoondoa sintofahamu ili kuimarisha imani ya wananchi.

“Wananchi wana haki ya kuelezwa tofauti kati ya mkutano unaoruhusiwa na unaozuiwa, hasa pale ambapo mikutano yote inafanyika hadharani na inahusisha masuala yanayogusa siasa. Hatari za usalama zinaweza kutoka popote,” amesema.

Amehoji nani ameona mashaka ya usalama katika mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na nani ameona ni salama baadhi ya mikusanyiko kufanyika, kama matamasha ya klabu za mpira wa miguu na mikutano ya viongozi wa Serikali.

“Maswali yanakuwa mengi. Hivi unapimaje hatari kwenye mikutano ya kisiasa ukaona hakuna hatari kwenye mikutano mingine inayokusanya maelfu ya watu? Hivi hao walioonekana hatari kwenye siasa si wanaweza kutumia mikutano inayoendelea kuathiri huo usalama?” amehoji.

Hata kama chama tawala ni miongoni mwa waliokumbwa na zuio hilo, amesema mikutano ya viongozi wa Serikali huchukuliwa kama ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kwa kuwa sehemu kubwa ya kinachozungumzwa ni sera za chama hicho.

Mkazi wa Dar es Salaam, Ibrahim Malume, amesema wakati wa mlipuko wa Uviko-19 Serikali ilizuia mikusanyiko yote bila kuangalia ya vyama vya siasa, Serikali, matamasha wala sherehe.

“Katazo kama lile la wakati wa Uviko-19 lilijitosheleza. Sasa hili limekuja na maelezo nusunusu. Je, hatari za kiusalama zipo kwenye siasa tu, wakati kuna mikusanyiko mingine inayokutanisha watu wengi na inaweza kuleta hatari zaidi?” amesema.

Mashaka ya haki

Mwanafunzi wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Amina Mbonde, amesema utekelezaji wa hatua za kiusalama unapaswa kuonekana wa haki kwa pande zote zinazohusika.

“Tatizo si kuwapo kwa tahadhari za kiusalama. Tatizo ni pale ambapo wananchi wanashindwa kuelewa kwa nini baadhi ya mikutano inaonekana salama na mingine inaonekana si salama,” amesema.

Ameeleza mazingira ya sasa yanaweza kuongeza hisia za kutoridhika miongoni mwa wadau wa siasa na wananchi iwapo hakutakuwa na mawasiliano ya wazi kuhusu sababu na vigezo vinavyotumika kufanya uamuzi huo.

“Njia bora ya kulinda utulivu wa kisiasa ni kuhakikisha hakuna upande unaoonekana kunufaika na vikwazo vilivyowekwa kwa upande mwingine,” amesema.

Serikali yajibu

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohammed Mahmoud, amesema uamuzi wa Serikali kuzuia mikutano hiyo umetokana na matishio ya kiusalama yanayotolewa kupitia majukwaa ya kisiasa.

“Zuio halikulenga CCM wala chama kingine chochote. Limelenga usalama wa nchi, na ubaya wenyewe ni kwamba matamko kuhusu hatari za kiusalama yananasibishwa na tarehe ambazo nchi itakuwa na shughuli kubwa ya uchumi wa wananchi wake,” amesema.

Ayoub amesema unapopanga tukio litakaloathiri usalama wa nchi katika siku ambazo wananchi wanakwenda kupambania biashara zao, kutafuta masoko na kuonesha shughuli zao, unawanyima uhuru wa kiuchumi.

“Siasa tunaweza kufanya siku yoyote, hazina siku maalumu, lakini Julai 7 wananchi huandaa fedha kwa mwaka mzima wakitarajia zile siku 14 za Sabasaba amepata faida na mambo uale yamekwenda,” amesema.

Kuhusu mikutano ya Waziri Mkuu, wabunge

Akijibu hilo, Ayoub amesema Waziri Mkuu ni msimamizi mkuu wa shughuli zote za Serikali, na anapotoa matamko yanayovigusa vyama bila kuvitaja, anatimiza wajibu wake wa kukemea kwa nafasi yake.

“Yeye, kama mtendaji mkuu wa Serikali, lazima avikemee kwa chama chochote kile. Ni wajibu wake; hamlengi kiongozi fulani wa chama,” amesema.

Kuhusu mikutano anayoitumia kuyasema hayo, amesema si ya kisiasa na inahusisha wananchi wote kutoka vyama mbalimbali, hivyo ni majukwaa sahihi kuzungumza anayoyazungumza.

Akizungumzia wabunge, Ayoub amesema mbunge anaporudi jimboni kuzungumza na wananchi hawakilishi chama cha siasa, bali hupeleka mrejesho kwa waliomtuma.

“Jukumu la mbunge anapotoka bungeni ni kurudi kwa wananchi kuwaambia walichokipata kutoka bungeni. Hiyo si siasa. Wameshatekeleza wajibu waliopewa na wananchi wa kusema bungeni, na wanarudi kupeleka mrejesho,” amesema.

Ameeleza kuwa hali hiyo ni tofauti na anapotoka kiongozi wa chama, kwani chochote atakachokizungumza au kukifanya kitakuwa ni siasa.

“Ndiyo maana agizo la Waziri limemwelekeza Mkuu wa Jeshi la Polisi, kwa kuwa ndiye mwenye mamlaka ya kutoa kibali cha mikutano ya kisiasa. Lakini mbunge haombi kibali, labda anaomba ulinzi tu,” amesema.

Alipoulizwa kuhusu mikusanyiko mingine, kama matamasha ya klabu za mpira wa miguu, amesema kilichozuiwa ni mikutano ya kisiasa pekee, si matukio ya kijamii, shughuli za maendeleo ya wananchi, uchumi au biashara.

Ametaka watu wayachukulie maelekezo hayo kwa mtazamo wa umuhimu wa usalama wa Taifa na si kuelekeza mawazo yao kwenye nani anapendelewa.

Kauli ya Polisi

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limesema linaendelea kufuatilia kwa karibu viashiria vya baadhi ya watu wanaodaiwa kuhamasisha vurugu na kupanga kufanya maandamano yasiyofuata taratibu za kisheria na kiusalama.

Akiwa katika Maonyesho ya Sabasaba jana, Jumapili, Julai 5, 2026, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, amesema pamoja na hali ya usalama nchini kuendelea kuwa shwari, vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kufuatilia mienendo ya watu wachache wanaodaiwa kutaka kuvuruga amani na usalama wa nchi.

Amesema uchunguzi unaoendelea umebaini kuwapo kwa uhamasishaji wa vurugu kupitia mitandao ya kijamii na vikundi vya majadiliano mtandaoni, ukiwamo madai ya mipango ya kushambulia viongozi, kuharibu na kupora mali za umma na binafsi, kuchoma shule na kuwashambulia askari wa vyombo vya ulinzi na usalama ili kupora silaha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *