ALIYEKUWA beki wa kulia wa Mtibwa Sugar, Datius Peter, amekamilisha usajili wake wa kujiunga na Geita Gold, baada ya kikosi hicho alichokitumikia misimu miwili kushuka daraja kutoka Ligi Kuu Bara hadi Championship.

Mtibwa imeshuka daraja baada ya kumaliza nafasi ya 15 katika Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-2026 ikikusanya pointi 27, ikishinda mechi sita, sare tisa na kupoteza 15, ikiungana na KMC iliyoburuza mkia na pointi tisa.

Nyota huyo alijiunga na Mtibwa Sugar Julai 1, 2024, akitokea Kagera Sugar na kukitumikia kikosi hicho kwa misimu miwili, ambapo baada ya mkataba wake kuisha msimu wa 2025-2026, ameamua kutafuta changamoto sehemu nyingine.

Alipotafutwa na Mwanaspoti, Datius alisema mkataba wake na Mtibwa Sugar umemalizika baada ya msimu wa 2025-2026 kuisha na sasa amepumzika kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho wa timu nyingine atakayoichezea, licha ya ofa mbalimbali alizonao.

“Ni kweli nina ofa na timu mbalimbali lakini msimu ndio umeisha na ninahitaji kufanya uamuzi mzuri wa kwenda sehemu pia nitayopata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza, nadhani muda ukifika nitaweka wazi vizuri juu ya hilo,” alisema Datius.

Licha ya kauli ya Datius, Mwanaspoti linatambua beki huyo amekamilisha usajili wa kujiunga na Geita Gold ambayo ndio bingwa wa Ligi ya Championship msimu wa 2025-2026, ikirejea Ligi Kuu baada ya kushuka msimu wa 2023-2024.

Geita Gold imerejea Ligi Kuu baada ya kuibuka mabingwa wa Championship msimu wa 2025-2026, ikiwa na pointi 77, ikiungana na Kagera Sugar iliyomaliza nafasi ya pili na pointi 72, kufuatia kushuka daraja msimu wa 2024-2025.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *