Nahodha wa Argentina, Lionel Messi amefichua kwamba tukio la kukosa penalti katika mechi ya jana dhidi ya Misri limemtesa kwa muda mrefu wa mchezo hadi pale timu yake ilipoibuka na ushindi.

Messi alipoteza penalti hiyo katika dakika ya 21 ya mchezo baada ya kuokolewa na kipa wa Misri, Mostafa Shobeir, jambo lililoifanya Argentina ishindwe kupata bao la kusawazisha baada ya kutanguliwa kufungwa bao la Yasser Ibrahim.

Hata hivyo, licha ya baadaye Misri kuongeza bao la pili, Argentina ilirudi mchezoni na kusawazisha kisha klufunga lingine na kufanya iibuke na ushindi wa mabao 3-2.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Messi amesema kuwa alijikuta akibubujikwa na machozi ya furaha kwani kama wangetolewa, anaamini angekuwa amewaangusha wenzake.

“Nililia kwa sababu nilikuwa nimekata tamaa sana kutokana na penalti niliyokosa na namna nilivyoipiga. Ninaamini kwamba kama ningefunga penalti ile, mchezo ungekuwa na muelekeo tofauti, kwa sababu tulikuwa tunacheza vizuri licha ya bao walilotufunga.

“Hata baada ya kukosa penalti, bado tuliendelea kutengeneza nafasi nyingi za wazi za kufunga. Tulikuwa tunacheza vizuri, na hatimaye kufanikiwa kusawazisha kisha kurudi na kushinda kulikuwa nafuu kubwa, kuondoa mzigo mkubwa moyoni, na zaidi ya yote furaha kubwa kwa kuendelea kubaki kwenye mashindano. Hatukutaka kurudi nyumbani, na hatukuweza kuruhusu safari yetu iishe kwa namna hiyo. Kikosi hiki kinastahili kuendelea mbele.

“Nilihisi kwamba katika wakati muhimu nilikuwa nimewaangusha wenzangu kutokana na penalti niliyokosa na jinsi nilivyoipiga. Lakini, namshukuru Mungu, kwa mara nyingine tena alikuwa ameniandalia jambo la pekee mwishoni. Nina furaha sana,” amesema Messi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *