Butiama. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amewataka watumishi wa umma wilayani Butiama kuacha uzembe na kutimiza wajibu wao ipasavyo ili wananchi wapate huduma bora bila kusubiri ziara za viongozi.

Kanali Mtambi ametoa kauli hiyo jana Jumatano, Julai 8, 2026 wakati akizungumza katika kikao maalumu cha baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kilichojadili hoja za ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Amesema amebaini baadhi ya changamoto zinazowakabili wananchi zinasababishwa na kutowajibika kwa baadhi ya watumishi wa Serikali, wakiwemo wakuu wa idara, ambao wanapaswa kuzitatua kwa wakati.

“Yapo mapungufu yanaonekana wazi kuwa yanasababishwa na kutokuwajibika kwa watumishi na watendaji wa Serikali. Hili halikubaliki, haki kama hii sitaki iendelee hapa Mara. Watumishi tunatakiwa kuwajibika na si vinginevyo,” amesema.

Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Butiama wakiwa kwenye kikao cha baraza maalum la kujadili hoja za CAG.  Picha na Beldina Nyakeke

Amesema uwajibikaji kwa watumishi wa umma si jambo la hiari bali ni wajibu unaotokana na nafasi walizonazo, akionya kuwa hataruhusu uzembe unaosababisha wananchi kukosa huduma zinazoweza kutolewa kwa urahisi na ngazi za chini za Serikali.

“Sisi watumishi wa Serikali uwajibikaji ni lazima, si hiari ilimradi umeajiriwa. Kwa yule asiyetaka kuwajibika aachie ngazi. Kuanzia sasa sitaki kusikia uzembe na kutokuwajibika kwa watumishi wa Serikali,” amesema.

Ameitaka pia Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kupitia madiwani wake kusimamia kwa karibu menejimenti ili kuhakikisha watumishi wanafanya kazi kwa viwango vinavyotakiwa.

Katika hatua nyingine, Kanali Mtambi amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Aziza Baruti kuhakikisha utekelezaji wa agizo la Serikali la kusajili vikundi vya vijana unafanyika kwa kasi.

Amesema Serikali imeelekeza kila halmashauri kusajili angalau vikundi 150 vya vijana ili viweze kuunganishwa na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotolewa na Serikali.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya kukabiliana na changamoto za ajira zinazowakabili vijana nchini.

“Serikali imeweka mikakati mbalimbali kuhakikisha changamoto za vijana zinapatiwa ufumbuzi, hivyo usajili wa vikundi ni sehemu muhimu ya kuwasaidia kupata fursa,” amesema.

Kwa upande wake, Baruti amesema hadi sasa halmashauri hiyo imesajili vikundi 11 vya vijana na kwamba zoezi hilo linaendelea ili kufikia lengo lililowekwa.

Kanali Mtambi pia amewataka madiwani kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili ikamilike kwa wakati na kutoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi.

Amesema miradi hiyo inapaswa kuzingatia thamani ya fedha na kuendana na malengo ya Serikali ya kuboresha maisha ya wananchi.

“Utekelezaji wa miradi uzingatie thamani ya fedha na ikamilike kwa wakati ili kutoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi. Hii itatafsiri kwa vitendo falsafa ya Rais Samia ya kuleta tabasamu kwa wananchi,” amesema.

Awali, Kaimu Mweka Hazina wa halmashauri hiyo, Wumbe Haruni alisema Halmashauri ya Wilaya ya Butiama imepata hati safi kwa mwaka wa fedha 2024/25, ikiwa ni mara ya tano mfululizo kupata hati hiyo kutoka kwa CAG.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *