Maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), yamekuwa zaidi ya kumbukizi ya mafanikio ya taasisi hiyo. Yameibua mjadala mpana kuhusu nafasi ya kodi katika maendeleo ya taifa na umuhimu wa kuwathamini wananchi na wafanyabiashara wanaotekeleza wajibu wao kwa uaminifu.

Tuzo ya Rais kwa Walipa Kodi Bora ni hatua inayostahili pongezi kwa kuwa inaleta motisha kwa walipa kodi na kuimarisha utamaduni wa uwajibikaji.

Miongoni mwa waliotambuliwa mwaka huu ni mfanyabiashara mashuhuri, Said Salim Bakhresa. Kwa miongo kadhaa, amekuwa miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa nchini na amejijengea sifa ya kuchangia maendeleo ya uchumi kupitia uwekezaji, ajira na ulipaji wa kodi.

Aidha, amekuwa akihusishwa na shughuli mbalimbali za kijamii, zikiwemo misaada kwa wenye uhitaji, utoaji wa zaka na sadaka, mara nyingi bila kutafuta umaarufu wa vyombo vya habari.

Kutambuliwa kwa walipa kodi bora kunapaswa kuwa ujumbe kwamba mafanikio ya biashara hayaishii kwenye faida pekee, bali pia yanajumuisha uwajibikaji kwa taifa.

Kodi ndiyo chanzo kikuu cha fedha zinazowezesha Serikali kutoa huduma za afya, elimu, maji, miundombinu na huduma nyingine muhimu kwa wananchi. Hivyo, kila anayelipa kodi kwa uaminifu anashiriki moja kwa moja katika kuijenga Tanzania.

Katika hotuba yake kwenye maadhimisho hayo, Rais Samia Suluhu Hassan aliwapongeza TRA kwa kazi kubwa ya ukusanyaji wa mapato na kuwashukuru walipa kodi wote wanaotekeleza wajibu wao kwa uaminifu.

Alisisitiza kuwa kaulimbiu ya maadhimisho, “Kulipa Kodi ni Uzalendo na Ushujaa kwa Maendeleo na Kujitegemea,” ina maana pana kuliko ukusanyaji wa mapato pekee.

Rais alieleza kuwa uzalendo huo unapaswa kuwa wa pande zote. Mwananchi na mfanyabiashara walipe kodi kwa uaminifu, TRA ikusanye kodi kwa haki na weledi, huku Serikali ikitumia mapato hayo kwa uadilifu kwa manufaa ya wananchi. Alikumbusha kuwa, ‘Imani huzaa imani.’

Kauli hiyo ina maana kuwa mlipa kodi akiona anatendewa haki na kodi zake zikirejeshwa kwa maendeleo ya wananchi, atakuwa na sababu zaidi ya kuendelea kutekeleza wajibu wake.

Mafundisho ya dini pia yanasisitiza umuhimu wa uwajibikaji katika masuala ya kodi. Katika Ukristo, Yesu Kristo alisema, “Basi, vya Kaisari mpeni Kaisari na vya Mungu mpeni Mungu,” akionesha kuwa kutekeleza wajibu wa kiraia ni sehemu ya maadili ya mwamini.

Kwa upande wa Uislamu, mafundisho mbalimbali yanahimiza haki katika ukusanyaji wa mali na matumizi yake kwa manufaa ya jamii, huku yakikataza dhuluma kwa pande zote.

Rais Samia alisisitiza kuwa dini zinakataza aina mbili za dhuluma: kodi ya dhuluma, pale mamlaka zinapomtoza mlipa kodi kiwango kisichoendana na uhalisia na dhuluma ya kodi, pale mlipa kodi anapoficha mapato au kukwepa kulipa kodi anayostahili. Mfumo bora wa kodi unapaswa kujengwa juu ya haki, uaminifu na uwazi.

Kwa mtazamo wangu, kutambua walipa kodi bora kunapaswa kwenda sambamba na kuendelea kuimarisha uwazi katika mfumo wa kodi.

Kadiri walipa kodi wanavyoona haki inatendeka kwa wote, ndivyo imani yao kwa taasisi za ukusanyaji mapato inavyoongezeka.

Hilo litasaidia kuongeza hiari ya kulipa kodi na kupanua wigo wa mapato ya Serikali.

Baada ya miaka 30 ya TRA, Tanzania ina sababu ya kutafakari mafanikio yaliyopatikana na kujenga msingi imara zaidi wa ushirikiano kati ya Serikali, TRA na walipa kodi.

Uchumi wenye nguvu haujengwi kwa sheria pekee, bali pia kwa uaminifu, uwajibikaji na imani ya wananchi kwamba mchango wao unatumika kwa manufaa ya taifa.

Ni vema tukaendelea kutambua kuwa tuzo zinazotolewa kwa walipa kodi bora zisiishie kuwa heshima kwa washindi pekee.

Ziwe chachu ya kujenga utamaduni mpya unaohamasisha uadilifu, uzalendo na uwajibikaji katika ulipaji wa kodi. Huo ndio msingi wa maendeleo endelevu na taifa linalojitegemea.

Mungu ibariki Tanzania. Mungu ibariki Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *