Matokeo ya 0-0 yameihakikishia Mbeya City kubaki Ligi Kuu ya NBC kwa msimu ujao wa 2026-2027 kufuatia awali kushinda mabao 2-0 dhidi ya Tanzania Prisons.

Wakati Mbeya City ikichekelea matokeo hayo, Tanzania Prisons itasubiri dakika 180 zingine kujiuliza dhidi ya Polisi Tanzania kutoka Ligi ya Championship katika hatua ya mtoano mwingine.

Tanzania Prisons na Mbeya City zilimaliza Ligi Kuu msimu wa 2025-2026 nafasi ya 13 na 14. Tanzania Prisons ilikusanya pointi 32, huku Mbeya City ikivuna pointi 30 na kuangukia mtoano wa kupambania kubaki.

Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Julai 5, 2026, Mbeya City ikiwa mwenyeji ilishinda 2-0 na leo Julai 8, 2026 kumalizika kwa suluhu.

Katika mchezo wa leo uliopigwa uwanja wa Sokoine jijini Mbeya huku Tanzania Prisons ikiwa mwenyeji, timu zote zilionesha ushindani lakini hakuna iliyoweza kupata bao.

Tanzania Prisons ilihitaji kubadili matokeo haswa kupata ushindi wa angalau 3-0 ili kubaki salama, ilhali Mbeya City ikilinda ilichovuna awali, hadi mwamuzi, Ramadhan Kayoko anamaliza dakika 90, ndugu hao waliondoka patupu, lakini ikawa faida kwa Mbeya City.

Polisi Tanzania iliyoshuka daraja Ligi Kuu msimu wa 2022-2023, inaisubiri Tanzania Prisons baada ya kushinda kwa jumla ya mabao 7-1 dhidi ya Mbeya Kwanza katika mchezo wa mtoano wa Ligi ya Championship kuwania kupanda faraja.

Tanzania Prisons ni mara ya pili kucheza mtoano ikikutana na timu ya Ligi ya Championship ikifanya hivyo msimu wa 2021-2022 ilipokutana na JKT Tanzania na kushinda mabao 2-1.

Kocha Mkuu wa Mbeya City, Salum Mayanga, amesema pamoja na furaha yake kubakiza timu Ligi Kuu, lakini haikuwa kazi nyepesi kutokana na ugumu wa ligi akieleza kuwa kipo cha kujifunza kwa matokeo ya msimu huu.

“Niwapongeze wachezaji kwa kujituma, haikuwa kazi nyepesi lakini waliamua kunielewa na ni funzo kwetu kwa msimu ujao kuhakikisha haturudii hiki,” amesema Mayanga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *