
Julai 9,2026, wenzetu Zanzibar wametiliana saini tamko la pamoja la maridhiano ya kisiasa baina ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na chama kikuu cha upinzani cha ACT – Wazalendo na kuleta utulivu wa kisiasa, amani na mshikamano.
Ninawaonea wivu sana Wazanzibar kwa kutanguliza maslahi mapana ya nchi yao baada ya kumaliza uchaguzi mkuu Oktoba 2025, lakini ninajiuliza sisi Tanzania Bara, nani ametuloga kiasi kwamba hatuoni umuhimu wa maridhiano ya kisiasa?
Ukisoma taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu Zanzibar, Ragey Mohamed na ile iliyotolewa na ACT – Wazalendo iliyosainiwa na Salim Bimani, wote wanazungumza lugha moja hadi raha.
ACT – Wazalendo wanasema Zanzibar ni kubwa kuliko vyeo na madaraka ya viongozi na kwamba Zanzibar ni kubwa kuliko ACT- Wazalendo na ndio maana wameamua kufuata njia ya maridhiano, ukweli, haki, uwajibikaji na umoja wa kitaifa.
Ni kweli, Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 toleo la 2010, Ibara ya 9(3) inasema muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utakuwa wa Umoja wa Kitaifa, sisi tunaweza kuja na maridhiano ya kikwetu kwetu kama Watanzania Bara.
Chimbuko la Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar ni kura ya maoni ya mwaka 2010 iliyoruhusu vyama pinzani kugawana madaraka, lakini ilisukumwa zaidi na kile kilichotokea baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000.
Wananchi, wengi wakiwa wafuasi wa CUF waliandamana Januari 2001 ambapo vyombo vya usalama vikiongozwa na Jeshi la Polisi viliyazima maandamano hayo kwa risasi za moto na kusababisha vifo, majeruhi na kuzalisha wakimbizi.
Hali hii ilizalisha uhasama mkubwa Zanzibar kiasi kwamba ilifika mahali watu hawasalimiani wala kuzikana ndio maana CCM na CUF kilichokuwa chama kikuu cha upinzani wakati ule, kikaona dawa ya kukomesha uhasama ni maridhiano.
Maridhiano ya 2010 ndio yalisaidia makubaliano ya kubadili Katiba, wananchi wakapiga kura ya maoni na chama kinachoshika nafasi ya pili hupata nafasi ya makamu kwa kwanza wa Rais na kupewa uwakilishi Katiba Baraza la Mawaziri.
Nitakuwa mnyimi wa fadhila nisipowapongeza kwa dhati waliokuwa marais wa Zanzibar, Aman Abeid Karume na Mohamed Shein, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na Wazanzibar kwa ujumla kwa kutanguliza mbele masilahi ya nchi yao.
Mazingira ambayo Zanzibar ilipitia baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 hayatofautiani sana na ambayo Tanzania Bara tumeyapitia baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Kwa mara ya kwanza katika nchi yetu tulishuhudia maandamano yasiyo na baraka za Jeshi la Polisi na ghasia katika mikoa mbalimbali nchini, yaliyosababisha vifo vya watanzania 518, majeruhi 2,390 na uharibifu wa mali zenye thamani Sh125 bilioni.
Lakini tangu kipindi hicho, hali haijatulia, kumekuwepo na matishio ya mara kwa mara ya maandamano yasiyofuata utaratibu wa kisheria, lakini kumeibuka chuki kubwa kutoka kwa baadhi ya Watanzania dhidi ya Serikali na vyombo vyake.
Ukitaka kujua nchi yetu inavimba, angalia siku imewekwa taarifa ya kiongozi yoyote wa Serikali au CCM au ofisa wa chombo chochote cha dola hasa Polisi au hata Mbunge wa CCM, uone maoni ya baadhi ya Watanzania wakifurahia madhila yao.
Yaani tumefika mahali tumepoteza kabisa utu, lakini tumefikaje hapo, hili ndio swali la msingi ambalo wengi hatutaki kusema ukweli na najiuliza, hivi nani ambaye hataki maridhiano ya kitaifa wakati nchi inavimba?
Ni nani, ni wahafidhina ndani ya CCM wasiotaka mabadiliko? Ni baadhi ya wana CCM wanaonufaika na mfumo? Ni viongozi wa vyama vya upinzani? Ni wanaharakati? Ni Watanzania? Ni nani hasa ambaye haoni faida ya maridhiano.
Bahati nzuri tunapo pa kuanzia kwa sababu tume iliyoundwa na Rais Samia Suhuhu Hassan chini ya Jaji mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman kuchunguza yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi imekuja na pendekezo hili.
Jaji Chande katika muhtasari wa ripoti ya Tume anasema matukio ya Oktoba 2025 na siku zilizofuata pamoja na changamoto ambazo zimekuwepo kwa muda mrefu ikiwamo Katiba mpya vimesababisha nyufa na majeraha kwa Taifa.
Hivyo, Tume ikasema maridhiano na muafaka wa Kitaifa ni hatua muhimu katika kuponya majeraha na kurejesha amani, kuaminiana, mshikamo na utengamano ndani ya jamii na taifa kwa ujumla na hapa ndipo nami napawekea mkazo.
Kwa mujibu wa Tume, maridhiano yanapaswa kuwa mtambuka yakijumuisha nyanja za kisiasa, kijamii na kiuchumi ili kutathmini zaidi ukweli, kuponya majeraha, kutafuta suluhisho na kufikia muafaka wa kisiasa, kukubaliana juu ya msingi wa Katiba Mpya na kurejesha umoja na mshikamano wa kitaifa.
Bahati nzuri, Jaji Chande na Tume yake wametuambia viini au chimbuko la changamoto zilizotufikisha hapa, ambazo hazikutatuliwa kwa muda mrefu na wala si mambo mageni masikioni mwetu. Tunazijua.
Baadhi ya changamoto hizo ni madai ya Katiba Mpya, demokrasia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, malalamiko ndani ya vyama vya siasa, madai ya maboresho ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na mfumo mzima wa uchaguzi.
Yapo pia masuala ya kijamii yanayojumuisha mmomonyoko wa maadili na kushuka kwa uzalendo, kutopatiwa ufumbuzi na majibu stahiki kwa kero katika jamii kama vile rushwa, ubadhirifu na madai ya wimbi la utekaji na kupotea kwa watu.
Rais katika mikutano yake ya kampeni uchaguzi uliomwingiza madarakani kwa kipindi cha pili 2025, aliahidi kuwa ndani ya siku 100 angeanzisha mchakato wa Katiba Mpya na kuunda Tume ya Maridhiano, ni wakati sasa wa kumhimiza.
Hata wakati akizindua Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Novemba 14,2025, Rais Samia aliwakaribisha wadau wa kisiasa kukaa meza moja kwa ajili ya kupata maridhiano ili kujenga mazingira ya mwafaka kwa maendeleo ya Taifa.
Nikimnukuu Rais Samia alisema; “Sitachoka kunyoosha tena mkono wa maridhiano. Ni matumaini yangu kuwa wadau wa kisiasa wataupokea kwa dhati mkono wa maelewano kupitia Tume ya Usuluhishi na Maelewano ili kwa pamoja tujenge mazingira ya muafaka kwa maendeleo ya Taifa letu.”
Sasa nani anakwamisha dhamira hii nje ya Rais wetu, ni baadhi ya wasaidizi wake? wahafidhina ndani ya CCM wasiotaka mabadiliko au ni nani?
Bahati nzuri tunazo 4R alizoziasisi Rais Samia ambazo ni Reconciliation (Maridhiano), Resilience (Ustahimilivu), Reforms (Mabadiliko na Rebuild (Kujenga upya), sasa tujiulize nani ni mchawi wetu aliyekwamisha utekelezaji wa hizo 4R?
Hivi vile viini au chimbuko la hasira za Watanzania ambazo Tume ya Jaji Chande amezisema tunashindwa kuzitafutia majawabu hadi nchi yetu ianze kunyimwa fedha za misaada au hata kutishia kuwawekea vikwazo viongozi wetu?
Kama Baba wa Taifa alivyowahi kusema, tusitatue matatizo yetu kwa kujifanya hayapo, nami nasema nchi iko kwenye mtanziko mkubwa wa kisiasa na kijamii, tunahitaji utashi wa kisiasa wa viongozi wetu kutunasua hapa tulipo.
Majawabu ya kututoa hapa tulipo tunayo, ila hatujaamua kuyatumia. Kwa hiyo leo tunapompongeza Rais Hussein Mwinyi na CCM kwa upande mmoja na ACT – Wazalendo kwa upande wa pili, hakika tunalo la kujifunza na si vibaya kama tukaiga hili walilolifanya ili kuleta utulivu wa kisiasa Tanzania Bara.
Na asijitokeze mwanasiasa au mtu kusema ameshinda endapo tutaamua kufuata nyayo za Zanzibar, bali sote kwa pamoja tuseme “Tanzania Imeshinda.” Nyerere alipata kusema ‘It can be done, play your part’, nami nasema inawezekana.
Daniel Mjema ni mwandishi wa habari na mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Anapatikana kwenye simu namba 0656600900 au Barua Pepe [email protected]