Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mansura Mossi Kassim amesema tamko la pamoja la maridhiano ya kisiasa kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo limeweka mbele maslahi ya nchi badala ya maslahi ya vyama vya siasa, vikundi au watu binafsi.

Mansura amesema hayo leo Julai 9, 2026, wakati akisoma tamko la pamoja katika hafla iliyofanyika Ikulu, Zanzibar, akieleza kuwa tukio hilo linaonesha azma ya pande zote mbili kuendelea kufanya kazi pamoja katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili Zanzibar kisiasa, kijamii na katika uendeshaji wa shughuli za jamii.

“Tukio hili la pamoja liaanisha azma ya pande zote mbili kuendelea kufanya kazi pamoja ili kupata ufumbuzi wa kudumu na endelevu wa changamoto zinazoikabili Zanzibar kisiasa, kijamii na katika uendeshaji wa shughuli za jamii,” amesema.

Amesema pande zote mbili zimekubaliana kuchukua hatua stahiki kuendeleza imani kwa wananchi pamoja na wadau wa uchumi, biashara na uwekezaji wa Zanzibar, huku mchakato wa utekelezaji wa makubaliano hayo ukiwa shirikishi kwa wananchi.

Ameongeza kuwa chombo maalumu kitaanzishwa kwa mujibu wa sheria ili kuratibu utekelezaji wa tamko hilo la pamoja, huku utekelezaji wake ukianza baada ya kutolewa kwa tamko hilo.

“Kwa upande wa viongozi wanahakikishia wananchi wa Zanzibar kwamba watasimamia mchakato kwa dhati na kuweka mbele maslahi mapana ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla,” amesema.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *