
BAADA ya Kocha wa Fountain Gate, Fredy Felix ‘Minziro’ kuibakisha timu hiyo kwenye Ligi Kuu Bara msimu ujao wa 2026-2027, mabosi wa kikosi hicho wamepanga kumuongezea tena mkataba mpya wa mwaka mmoja kutokana na kazi kubwa aliyoifanya.
Minziro aliyewahi kuzifundisha timu mbalimbali za Geita Gold, Pamba Jiji na Tanzania Prisons, alijiunga na Fountain Gate Aprili 10, 2026, akitokea Bigman FC inayoshiriki Championship ili kurithi mikoba ya Mohamed Ismail ‘Laizer’ aliyeondoka klabuni hapo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Rais wa Fountain Gate, Japhet Makau alisema licha ya Minziro kuiongoza timu hiyo kwa kipindi cha muda mchache, ila kumekuwa na mabadiliko makubwa ya kiuchezaji kwa nyota mbalimbali, jambo ambalo limewafurahisha.
“Malengo yetu ni kuona Minziro tunaendelea naye tena kwa msimu ujao, kwa sasa kuna vitu tunaendelea kuvifanyia kazi kwa haraka na muda wowote tutamuongezea mkataba mpya wa kuendelea kuifundisha Fountain Gate kwa msimu ujao,” alisema Makau.
Tangu ajiunge na Fountain Gate, Minziro ameiongoza timu hiyo katika mechi 13, za Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2025-2026 na kati ya hizo ameshinda tano, sare mbili na kupoteza sita, huku kikosi hicho kikifunga mabao 17 na kuruhusu 22.
Kiujumla timu hiyo kwa msimu wa 2025-2026, imecheza mechi 30, za Ligi Kuu Bara ambapo kati ya hizo imeshinda tisa, sare sita na kupoteza 15, ikimaliza nafasi ya 12 na pointi 33, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 25 na kuruhusu 44.
Timu hiyo ilianza kufundishwa na Mnigeria Ortega Deniran ambaye hata hivyo, aliondoka mapema tu kabla ya msimu wa 2025-2026, kuanza na nafasi yake kuchukuliwa na Denis Kitambi aliyeondoka kwa makubaliano ya pande mbili, Septemba 28, 2025.
Kuondoka kwa Kitambi, timu hiyo ikaongozwa na kocha msaidizi, Mohamed Ismail ‘Laizer’, ambaye msimu wa 2024-2025, ndiye aliyeinusuru kushuka daraja, japo alivunjiwa mkataba wake rasmi, Aprili 10, 2026 na nafasi yake kukabidhiwa Minziro ambaye alipambana na kuibakiza timu hiyo kwenye ligi.