
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewachukulia hatua viongozi wake wa Mkoa wa Morogoro na Jimbo la Bumbuli, mkoani Tanga, baada ya kumtuhumu hadharani makamu mwenyekiti wa chama hicho bara, John Heche na kutaka achukuliwe hatua za kinidhamu.
Hatua hizo zimemkumba Katibu wa Jimbo la Bumbuli, Abubakari Mashambo, aliyevuliwa wadhifa wake na Katibu wa Chadema Mkoa wa Morogoro, Barnabas Okola, aliyesimamishwa uongozi wake.
Viongozi hao pia wametakiwa kuwasilisha uthibitisho wa tuhuma walizozitoa dhidi ya Heche ndani ya siku 14.
Kwa nyakati tofauti, Mashambo na Okola walidai kuwa Heche hupokea michango ya fedha kutoka kwa wadau, lakini huitumia kwa masilahi binafsi badala ya kuielekeza kwa shughuli za chama.
“Tumeona ni vyema kulifikisha jambo hili kwa waandishi wa habari ili Heche ajitathmini, kwa sababu fedha hizo hazisaidii chama. Tunaona hafai kuendelea na nafasi ya makamu kwa kipindi hiki,” amesema Mashambo.
Baada ya kauli hizo, Chadema Kanda ya Kaskazini imetoa taarifa ikieleza kuwa kuanzia Julai 8, 2026, Mashambo amevuliwa wadhifa wake kwa tuhuma za kukiuka kanuni za chama kwa kupeleka malalamiko kwenye vyombo vya habari badala ya kutumia vikao halali vya chama.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosainiwa na Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Yohana Kaunya, Mashambo ametakiwa, kwa mujibu wa Ibara ya 6.3.6(c) ya Katiba ya Chadema ya mwaka 2006, kuwasilisha uthibitisho wa tuhuma zake ndani ya siku 14 tangu kupokea taarifa rasmi.
Kaunya amesema kusimamishwa kwake ni kwa mujibu wa Ibara ya 6.3(c) na (d), na kutadumu hadi Kamati ya Utendaji ya Kanda yenye mamlaka ya nidhamu itakapokamilisha uchunguzi na kutoa uamuzi wa mwisho.
Katika hatua nyingine, Chadema Kanda ya Kati, inayojumuisha mikoa ya Morogoro, Dodoma na Singida, imetangaza kumsimamisha uongozi Katibu wa Mkoa wa Morogoro, Barnabas Okola, kwa madai ya kukiuka maadili ya chama kwa kumtuhumu Heche hadharani.