Iringa. Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima, amewataka wazazi na walezi nchini kutambua umuhimu wa kuwapeleka watoto katika vituo vya kulelea watoto wadogo na elimu ya awali.

Akizungumza leo Julai 10, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi sita inayotekelezwa na BRAC Maendeleo katika Manispaa ya Iringa, Dk Gwajima amesema watoto wanapaswa kuwa katika mazingira salama wanapokuwa wazazi wao wako kazini badala ya kubaki mitaani.

“Tusijiulize ukatili dhidi ya watoto utaishaje. Jibu ni kuwekeza katika vituo vya kulelea watoto na elimu ya awali. Huko ndiko tunakowajengea watoto usalama, malezi bora na msingi wa mafanikio yao,” amesema Dk Gwajima.

Amesema watoto wanaolelewa katika mazingira yenye malezi bora hukua wakiwa na maadili, afya njema na uwezo wa kufikia mafanikio, huku akiitaka jamii kuona gharama za malezi ya watoto ni uwekezaji muhimu kama ilivyo kwa shughuli nyingine za kijamii.

Dk Gwajima amewahimiza wananchi kujitokeza kuunga mkono jitihada za kuanzisha na kuendeleza vituo vya kulelea watoto, akisema jamii haiwezi kupambana na ukatili bila kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto.

Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Iringa, Saida Mgeni, amesema mkoa umeendelea kuhuisha majukwaa ya uwezeshaji kiuchumi na kwa sasa una mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) 180 yanayoshirikiana na Serikali katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Moja ya kituo cha kulelea watoto na wanafunzi wa awali kilichopo kata ya Mtwivila. Picha na Christina Thobias

Mkurugenzi Mkuu wa BRAC Maendeleo nchini, Joydeep Sinha, amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kutekeleza miradi inayolenga kuinua ustawi wa wananchi, hususan wanawake, vijana na watoto.

“Ushirikiano wetu na Serikali unalenga kuhakikisha wananchi wanapata fursa za maendeleo kupitia elimu, uwezeshaji wa kiuchumi na huduma za malezi ya watoto,” amesema Joydeep.

Meneja wa BRAC Maendeleo Tanzania Mkoa wa Iringa, Theresia Manyahi, amesema hadi sasa watu zaidi ya 140,000 nchini wamenufaika na programu mbalimbali zinazotekelezwa na taasisi hiyo.

Amesema katika awamu inayofuata wanawake 725,230 wenye umri kati ya miaka 12 na 30 wanatarajiwa kunufaika kwa kupata msaada wa kurejea shuleni, mafunzo ya stadi za maisha, vifaa vya kujifunzia na ujuzi wa kujitegemea.

Aidha, amesema shule 400 nchini zitashirikiana na BRAC Maendeleo Tanzania katika kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujitegemea, huku wahudumu wa vituo vya malezi wakipatiwa mafunzo maalumu na vikundi vya maendeleo ya jamii vikitarajiwa kunufaika na mikopo.

Katika Kituo cha Malezi cha Mgera, mlezi Rose Kalinga amesema kituo hicho kilianza Februari 2026 kikiwa na watoto wawili, lakini sasa kinahudumia watoto 16 kutokana na ongezeko la uelewa wa jamii.

Rose amesema changamoto kubwa inayokikabili kituo hicho ni uelewa mdogo wa baadhi ya wazazi kuhusu umuhimu wa vituo vya malezi, pamoja na ukosefu wa usafiri kwa watoto wanaotoka maeneo mbalimbali.

“Eneo tulilonalo, pia, ni dogo. Watoto wakiongezeka tutahitaji nafasi kubwa zaidi ili kuendelea kutoa huduma bora,” amesema Rose.

Kutokana na changamoto hizo, Dk Gwajima amemtaka Mkuu wa Wilaya pamoja na Halmashauri kuangalia namna ya kushirikiana na wadau katika kuboresha mazingira ya vituo hivyo, akisisitiza kuwa uwekezaji kwa watoto ni uwekezaji wa Taifa.

Pia, amewataka wahudumu wa vituo vya malezi kuwa waadilifu na wenye maadili mema ili kujenga imani kwa jamii, akisema uaminifu ndio mtaji mkubwa wa maendeleo ya huduma hizo.

Diwani wa Kata ya Mkwawa, Kalinga, amesema maelekezo yaliyotolewa na Waziri yatafanyiwa kazi kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali za mitaa na wananchi.

Zainabu Juma, mkazi wa Kata ya Mgera, amesema vituo vya malezi vinawapa wazazi utulivu wanapokuwa kazini wakijua watoto wao wapo sehemu salama, huku Frank Nyangwa na Suzana Mofuga wakisema tangu watoto wao waanze kuhudhuria vituoni wameonyesha mabadiliko chanya ya kitabia na kujifunza.

Katika ziara hiyo, Dk Gwajima alikagua mradi wa kilimo cha nyanya, mradi wa ufugaji wa nguruwe, Kituo cha Mwautwa Community Based Centre pamoja na vikundi viwili vya maendeleo vinavyosimamiwa na BRAC Maendeleo Tanzania katika Manispaa ya Iringa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *