Dar es Salaam. Serikali imesema itaendelea kuwashirikisha wawekezaji katika utungaji na mapitio ya sera, sheria, kanuni na miongozo ili kuhakikisha sekta ya nishati inakuwa na sera zinazotabirika na zinazovutia uwekezaji.
Ahadi hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Nishati, Petro Lyatuu, wakati akifunga Kongamano la Siku ya Nishati 2026 lililofanyika sambamba na Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Lyatuu amesema sekta binafsi ina mchango mkubwa katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, hususan katika kufikia lengo la kujenga uchumi wa dola trilioni moja.
“Karibu asilimia 70 ya ufadhili wa sekta ya nishati ifikapo mwaka 2050 unatarajiwa kutoka sekta binafsi, kwa hiyo ni muhimu kuhakikisha sera zetu zinatabirika na tunawashirikisha wawekezaji wakati wote,” amesema.
Amesema Serikali pia imepokea maoni ya wadau kuhusu umuhimu wa kuimarisha upatikanaji wa fedha kwa miradi ya nishati, ikiwemo kujenga mazingira yatakayowezesha taasisi za fedha, wawekezaji na Serikali kushirikiana katika kutoa dhamana na kupunguza hatari za uwekezaji.
Baadhi ya wadau walioshiriki katika hitimisho la Kongamano la Siku ya Nishati 2026 lililofanyika sambamba na Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Akizungumzia matumizi ya magari yanayotumia umeme, Lyatuu amesema Serikali iko tayari kufanyia kazi changamoto zozote za kisera au kiudhibiti zinazoweza kujitokeza ili kuhakikisha teknolojia hiyo inakua na kuwa sehemu ya mabadiliko ya sekta ya usafiri nchini.
Katika kongamano hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli Tanzania (Pura), Charles Sangweni, amesema Tanzania inaendelea kujijengea nafasi kama moja ya nchi zenye fursa kubwa za uwekezaji katika sekta ya nishati barani Afrika, ikichochewa na uwepo wa rasilimali nyingi za asili na sera zinazolenga kuvutia uwekezaji.
“Nchi inaendelea kusonga mbele katika utekelezaji wa miradi mikubwa, ikiwemo mradi wa Gesi Asilia Kimiminika (LNG), huku gesi asilia ikiendelea kutambulika kama nishati muhimu ya mpito inayoiwezesha Tanzania kuelekea kwenye matumizi makubwa ya nishati safi na uchumi wa kijani,” amesema.
Mhandisi Mkuu kutoka Wizara ya Nishati, Christopher Nyondo, amesema wakati Serikali inalenga kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme hadi kufikia megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030, kufanikisha lengo hilo kunahitaji uwekezaji mkubwa kutoka sekta binafsi.
“Kutokana na gharama kubwa za miradi ya nishati, Serikali imeweka mkakati wa kuihusisha sekta binafsi katika uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme, huku ikilenga asilimia 70 ya uwekezaji wa sekta hiyo ifikapo mwaka 2050 kutoka kwa wawekezaji binafsi,” amesema.
Mhandisi Peter Kigadye kutoka Wizara ya Nishati amesema pamoja na kuongeza uzalishaji wa umeme, Serikali inawekeza kwa kiasi kikubwa katika upanuzi wa miundombinu ya usafirishaji wa umeme ili kuhakikisha nishati inayozalishwa inawafikia watumiaji.
“Pia, tutajiandaa kutumia teknolojia ya gridi janja (smart grids) na kuimarisha miunganiko ya kikanda ya umeme ili kuongeza uhakika wa upatikanaji wa nishati na kufungua fursa za biashara ya umeme,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), Hassan Said, amesema mafanikio ya sekta ya nishati hayapaswi kupimwa kwa idadi ya vijiji vilivyofikiwa na umeme pekee, bali kwa namna umeme huo unavyozalisha ajira, biashara na viwanda.
“Rea imeelekeza nguvu katika kufikisha umeme kwenye maeneo yenye shughuli za uzalishaji kama kilimo cha umwagiliaji, viwanda na migodi, huku ikiendelea kutekeleza miradi ya ruzuku na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuhakikisha umeme unakuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi vijijini,” amesema.