KUNA taarifa za ndani kutoka TRA United kwamba, klabu hiyo ipo hatua za mwisho kukamilisha usajili wa kiungo Greyson Gwalala kutoka Coastal Union ya Tanga.

Gwalala aliyezaliwa Novemba 16, 1993 (umri miaka 32), chanzo cha taarifa kutoka kwa mtu wake wa karibu, kilisema TRA United imebakiza hatua za mwisho kumalizana naye.

“Ni vitu vichache vimesalia na atasaini mkataba wa miaka miwili kwa ajili ya kuitumikia TRA United kwa msimu ujao,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“TRA imevutiwa na kiwango alichokionyesha akiwa Coastal, viongozi wameona awe sehemu ya kikosi hicho kwa ajili ya ligi ya msimu ujao inayoanza mapema mwezi Agosti.”

Alipotafutwa mchezaji huyo ili kuthibitisha ukweli wa taarifa hizo amesema: “Sipo tayari kulizungumzia hilo kwa sasa.”

Endapo Gwalala akijiunga na TRA United, nafasi anayocheza anakwenda kukutana na ushindani wa namba dhidi ya Mzamiru Yassin ambaye imeelezwa amesaini mkataba wa miaka miwili na timu hiyo aliyoitumikia kwa kipindi cha miezi sita kwa mkopo akitokea Simba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *