KATIKA kujiimarisha kuelekea msimu mpya na mashindano ya kimataifa, KVZ imefanikiwa kukamilisha usajili wa mshambuliaji kutoka Junguni United, Nature Mwakilembe.

Straika huyo anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji watakaoongeza nguvu katika kikosi hicho, huku usajili wake ikiwa ni sehemu ya mkakati wa mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Zanzibar kuunda timu yenye ushindani zaidi.

Akizungumza na Mwanaspoti, mshambuliaji huyo amesema kabla ya dili hilo kukamilika, timu tatu alikaa nazo mezani zikihitaji huduma yake ambazo ni Kipanga, Uhamiaji na KVZ zote zikiwa na ofa nzuri kwake.

Bila ya kutaja dau walilokubaliana, mshambuliaji huyo amesema baada ya timu hizo kumfuata alichagua KVZ kwasababu anaamini itatimiza malengo aliyojiwekea.

“Nimefungua ukurasa mpya wa maisha ya soka na dhamira yangu ni kuchangia mafanikio katika timu yangu,” amesema.

Amesema, ujio wake unapaswa kuwa matumaini kwa benchi la ufundi na mashabiki wa KVZ, ambao wanatarajia kuona timu ikiendelea kufanya vizuri katika mashindano ya ndani na nje ya Zanzibar.

KVZ iliyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar msimu wa 2025-2026, hivi sasa inajiandaa na amshindano ya Kagame yanayotarajiwa kuanza Julai 24 hadi Agosti 8 mwaka huu jijini Kigali nchini Rwanda, huku pia ikiwa na tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2026-2027.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *