
Matokeo ya utafiti huo yamewekwa wazi leo mbele ya viongozi kutoka nchi mbalimbali wanaohudhuria Mkutano wa Mageuzi ya Elimu TES+4 unaofanyika Paris, Ufaransa ili kufuatilia utekelezaji wa maazimio ya mkutano wa kwanza wa Mageuzi ya Elimu uliofanyika mwaka 2022 na pia ili kusongesha zaidi ufikiaji wa Lengo namba 4 la Maendeleo Endelevu linalohusu Elimu Bora.
Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Khaled El-Enany, amesema, “elimu ndiyo uwekezaji wenye nguvu zaidi ambao nchi zinaweza kufanya, lakini inaendelea kukosa ufadhili wa kutosha kwa kiwango kikubwa. Makadirio yetu yanaonesha kuwa misaada ya kimataifa kwa elimu itapungua kwa hadi asilimia 30 kati ya mwaka 2023 na 2027, jambo litakaloendeleza mzunguko wa uwekezaji mdogo, ukosefu wa usawa na kudorora kwa maendeleo. Mbinu bunifu za ufadhili, kama kubadilisha deni kuwa uwekezaji katika elimu, tayari zipo; kinachohitajika ni utashi wa kisiasa ili zitekelezwe kwa kiwango kikubwa zaidi.”
UNESCO inakadiria kuwa nchi zenye kipato cha chini na cha chini cha kati zinakabiliwa na pengo la ufadhili wa elimu la dola za Marekani bilioni 97 kila mwaka, na pengo hilo linaendelea kuongezeka.
Mbinu zinazotoa matumaini
Ili kusaidia nchi kukabiliana na changamoto hizi, UNESCO imezindua mwongozo wa kiufundi kuhusu kubadilisha deni kuwa uwekezaji katika elimu.
Mpango huo unaziwezesha nchi kubadili sehemu ya madeni yao ya nje na kuyaelekeza katika uwekezaji maalumu wa sekta ya elimu. Mwongozo mpya wa UNESCO unaeleza mazingira ambayo mfumo huo unaweza kuwa na mafanikio na unatoa zana za vitendo kwa nchi wadaiwa na wadai.
Mifano ya mafanikio
Makubaliano yaliyofikiwa na Ufaransa mwaka 2023 yaliiwezesha Côte d’Ivoire kuachilia rasilimali zilizotumika kujenga zaidi ya shule 30 katika maeneo yaliyokuwa na huduma duni, na kuwafikia wanafunzi wapatao 30,000.
Mwaka 2024, makubaliano ya kubadilisha deni yenye thamani ya euro milioni 29 kati ya Ujerumani na Misri yalisaidia kuimarisha programu za lishe shuleni, huduma za lishe na upatikanaji wa huduma za msingi.
Aidha, kati ya mwaka 2006 na 2017, mpango wa kubadilisha deni kati ya Uhispania na Peru ulibadilisha deni lenye thamani ya dola za Marekani milioni 20 kuwa miradi 50 ya elimu ya muda wa kati katika maeneo manane yaliyo hatarini, na kuwafikia takribani wanafunzi, walimu na wanajamii 174,000.