
Saddam Haftar Naibu Kamanda Jeshi la Mashariki mwa Libya amesema kuwa viongozi wakuu wa kijeshi kutoka mashariki na magharibi mwa Libya wamekutana katika mji wa Sirte katikati mwa nchi hiyo kujadili kuunganisha vikosi vya jeshi vilivyogawanyika nchini humo.
Mkutano huo uliwakutanisha Mkuu wa Jeshi la Mashariki Khaled Haftar na mwenzake wa Magharibi Salah al-Din al-Namroush pamoja na wajumbe wa Tume ya Pamoja ya Kijeshi (5+5), Kamati ya Pamoja ya Usalama na Kijeshi (3+3) na wawakilishi wa Ujumbe wa Usaidizi wa Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNSMIL).
Mazungumzo hayo ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za kuunganisha tena uanzishwaji wa jeshi la Libya na kuhitimisha mgawanyiko wa kitaasisi uliodumu kwa miaka kadhaa.
Naibu Kamanda wa Jeshi la Mashariki mwa Libya ameyataja majadiliano hayo kuwa yenye kujenga lakini hakusema iwapo kumefikiwa makubaliano yoyote katika mazungumzo hayo au la.
Vikosi vya ulinzi vya Libya vimegawanyika kati ya askari jeshi wa mashariki vinavyoongozwa na Kamanda Khalifa Haftar na wale wanaoiunga mkono Serikali ya Umoja wa Kitaifa yenye makao yake makuu katika mji mkuu Tripoli.
Libya imeendelea kugawanyika kisiasa kwa miaka kadhaa kati ya tawala hasimu Mashariki na Magharibi, huku juhudi za mara kwa mara za kuandaa uchaguzi wa kitaifa zikigonga mwamba. Hyo ni kutokana na kuwepo hitilafu mivutano kuhusu msingi wa katiba na vigezo vya stahiki vya wagombea.