Kipindupindu chaenea huku mfumo wa afya ukilemewa

Kwa mujibu wa WHO:

  • Wagonjwa  1,330 wa kipindupindu vimethibitishwa nchini Sudan.
  • Watu 114 wamefariki dunia kutokana na ugonjwa huo.
  • Majimbo ya Darfur na Kordofan ndiyo yaliyoathirika zaidi.
  • Kiwango cha vifo miongoni mwa wagonjwa kimefikia asilimia 13.7.
  • WHO inaonya kuwa msimu wa mvua unaweza kuongeza kasi ya maambukizi.

Mwakilishi wa WHO nchini Sudan, Dkt. Shible Sahbani amesema hali hiyo inahitaji hatua za haraka. “Kipindupindu kimerudi na kinaathiri majimbo kadhaa, hasa sehemu za magharibi mwa nchi, maeneo ya Darfur na Kordofan.”

© WHO Wanawake wakichota maji kutoka kisimani huko Kordofan Magharibi, Sudan.

Vita vinachochea kuenea kwa ugonjwa

WHO imesema mapigano yanayoendelea kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na kikosi cha Rapid Support Forces (RSF) yamesababisha mamilioni ya watu kukimbia makazi yao, jambo linaloongeza hatari ya maambukizi.

Kwa mujibu wa shirika hilo:

  • Zaidi ya watu milioni 33 wanahitaji msaada wa kibinadamu.
  • Watu milioni 21 wanahitaji huduma za afya.
  • Takriban watu milioni 13.4 wamekimbia makazi yao, wakiwemo milioni tisa walioko ndani ya Sudan na milioni 4.6 katika nchi jirani.

WHO pia imeonya kuwa idadi halisi ya wagonjwa na vifo huenda ikawa kubwa zaidi kutokana na changamoto za ukusanyaji wa taarifa katika maeneo ya mapigano.

El-Obeid yakabiliwa na hatari kubwa

WHO imeeleza wasiwasi wake kuhusu uwezekano wa mlipuko kusambaa katika mji wa El-Obeid, jimbo la North Kordofan, ambako mashambulizi ya kila siku na mfumo dhaifu wa afya vinaendelea kuzuia utoaji wa huduma.

“Tunatiwa wasiwasi mkubwa na uwezekano wa kipindupindu kuenea hadi El-Obeid katika jimbo la North Kordofan, ambako upatikanaji wa misaada ni mdogo sana na mfumo wa afya ulio dhaifu unaendelea kulemewa. Vituo vya afya vimeelemewa na upatikanaji wa huduma ni mdogo sana.” WHO imesema tayari imeweka akiba ya vifaa vya afya vinavyoweza kuhudumia zaidi ya watu 25,000 mjini El-Obeid. Wiki hii pia ilisafirisha tani 8.5 za vifaa vya tiba kwenda Kadugli na Dilling katika jimbo la South Kordofan, ikiwa ni msaada wa kwanza kufika Kadugli tangu Desemba 2024 kutokana na vikwazo vya upatikanaji.

WHO yatoa wito wa msaada zaidi

WHO imetoa wito kwa washirika wa maendeleo na wafadhili kuongeza msaada ili huduma za afya na vifaa vya tiba viwafikie wananchi walio katika hatari, huku ikionya kuwa Sudan pia inakabiliwa na milipuko mingine ya dengue, malaria, homa ya uti wa mgongo, homa ya ini aina E na surua.

Dkt. Sahbani amesema, “Tunatoa wito kwa washirika na wafadhili wetu kutusaidia ili kwanza tuweze kufika maeneo hayo na pili tuweze kupeleka vifaa na huduma za kutosha El-Obeid. Tunafahamu hali huko ni mbaya sana na inaendelea kuzorota, huku hatari ya milipuko ya magonjwa, utapiamlo, vurugu, ikiwemo ukatili dhidi ya wanawake na watoto, ikiongezeka.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *