
Shirika la Amnesty International mapema jana Alhamisi lilitoa wito wa kufanyika uchunguzi kuhusu mashambulizi matatu yaliyofanywa na utawala wa Israel kusini mwa Lebanon mwezi Machi, likiyataja mashambulizi hayo kuwa ni uhalifu wa kivita.
Shirika hilo limesema katika ripoti kwamba mashambulizi hayo yalisababisha mauaji ya raia 24, wakiwemo watoto 12, na kuangamizwa familia nzima.
Mashambulizi hayo matatu yalilenga nyumba za raia katika miji ya Tyre na Nabatieh na mji wa Arkay karibu na Sidon kati ya Machi 6 na 13.
“Katika wiki moja tu, jeshi la Israel liliangamiza familia nzima nchini Lebanon, wakiwemo watoto 12, na kuonyesha jinsi utawala huo usivyojali maisha ya raia,” amesema Kristine Beckerle, naibu mkurugenzi wa kikanda wa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini wa Amnesty International.
“Ni familia ngapi zaidi zitalazimika kutoa sehemu za miili ya watoto wao chini ya vifusi kabla ya mzunguko huu mbaya wa uhalifu wa kivita kuisha?” ameuliza afisa huyo wa Amnesty International. Beckerle ametoa wito kwa nchi mbalimbali kuweka “vikwazo vya haraka vya silaha dhidi ya Israel” na kuzitaka nchi kuchunguza na kuwashtaki wale waliohusika kwa kutumia mamlaka ya ulimwengu panapohitajika.
Pia ameonya kuwa jitihada za kimataifa zinazolenga kupunguza mvutano hazipaswi kufuta uwajibikaji. Miongoni mwa mashambulizi ya kihalifu ya Israel yaliyosajiliwa na Amnesty International ni pamoja na shambulio la Machi 6 kwenye nyumba ya familia ya Saleh katika wilaya ya Tyre. Shambulio hilo liliua raia wanane, wakiwemo watoto watatu na mwanamke mjamzito, na kuharibu makazi ya familia hiyo bila onyo la awali.
Hussein Saleh, baba wa familia ambaye alinusurika kwa sababu alikuwa ameondoka nyumbani kwa muda mfupi kununua mboga kabla ya futari, ameelezea alichokutana nacho baada ya kurudi na kukuta familia yake imezikwa chini ya kifusi. “Hakukuwa na alama yoyote iliyobaki ya nyumba, hakukuwa na kuta, hakukua na vitalu, na vipande vya miili (ya familia yangu) vilikuwa vimetawanyika chini … Nilitumia siku tatu kukusanya sehemu za miili ya familia,” amesema Hussein Saleh.
Raia huyo ambaye alikuwa akizungumza kwa masikitiko na huzuni kubwa amesema: “Hakukuwa na shabaha yoyote ya kijeshi. Wote walikuwa wanawake na watoto … Israel imeharibu maisha yangu yote”. Amnesty imesema uchunguzi wake na ushahidi wa watu haukuonyesha kwamba nyumba hiyo ilikuwa ikitumika kwa madhumuni ya kijeshi.