
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema, mashambulizi yaliyofanywa na jeshi la Marekani dhidi ya maeneo kadhaa katika mikoa ya pwani ya kusini mwa nchi pamoja na madaraja mawili yaliyopo katika mikoa ya mashariki kwenye njia ya reli inayoelekea mji mtakatifu wa Mashhad, yanajumuisha uhalifu mkubwa wa kivita.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali mashambulizi ya jeshi la Marekani yaliyofanyika alfajiri ya Alhamisi ya leo dhidi ya maeneo kadhaa katika mikoa ya pwani ya kusini mwa Iran pamoja na madaraja mawili yaliyopo katika mikoa ya mashariki kwenye njia ya reli inayoelekea mji mtakatifu wa Mashhad.
Wizara hiyo imesema mashambulizi hayo, ambayo imeeleza kuwa bila shaka ni uhalifu mkubwa wa kivita, ni kitendo kinachokiuka sheria za kimataifa. Aidha imesisitiza azma thabiti ya wananchi wa Iran ya kulinda ukamilifu wa ardhi yao, mamlaka ya taifa na usalama wa nchi.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeongeza kuwa mashambulizi ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi cha saa 48 zilizopita, yaliyofanywa kwa kisingizio cha kujibu matukio yanayodaiwa kuhusisha baadhi ya meli zilizokiuka sheria wakati zikivuka Mlango wa Hormuz siku ya Jumanne, si tu kwamba yanakiuka wazi kifungu cha 4 cha Ibara ya 2 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, bali pia ni ukiukaji mkubwa wa vifungu vya kwanza na vya tano vya hati ya makubaliano ya kusitishwa vita. Wizara hiyo imesema hatua hiyo pia ni kisingizio kinachotumiwa kuhalalisha kutotekeleza Marekani makubaliano hayo ya kusitisha vita.
Katika kujibu uchokozi huo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) limeshambulia miundombinu muhimu katika kambi nne za Marekani huko Kuwait na Bahrain katika awamu ya kwanza ya majibu yake dhidi ya ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha vita unaofanywa na Marekani.